Monday, July 15, 2019

JINSI YA KUPATA WAZO LA TOFAUTI NA WENGINE NA KUFANIKIWA

Katika kupata wazo bora, zingatia mambo yafuatayo;
Moja; anza na chochote unachojali sana.
Watu wengi wamekuwa wanafikiria kwamba ili uweze kuleta mabadiliko makubwa kwako na kwa wengine basi inabidi uwe na wazo kubwa na la kipekee sana. Wazo ambalo wengine hawajawahi kuwa nalo. Huo siyo ukweli, unaweza kuanza na wazo lolote na ukaweza kulijenga kwa utofauti na ukajitofautisha sana.
Anza na chochote unachojali, unachopenda, unachoamini, unachojua, ulichozoea au ambacho umesomea. Chochote kile ambacho unaona kinaweza kuwa bora zaidi ya kilivyo sasa, unaweza kukichukua kama wazo lako la kufanyia kazi.
Mbili; uliza maswali ambayo hayaulizwi.
Watu wamekuwa wanafanya mambo kwa mazoea kwa sababu wanafanya kile ambacho kila mtu anafanya, na hawathubutu kujaribu vitu vya tofauti. Sasa kwa wazo unalotaka kufanyia kazi kuliboresha zaidi, anza kwa kuuliza maswali ambayo watu wengine hawaulizi.
Maswali hayo yanaweza kuwa, vipi kama.... vipi kinyume cha... Hapa unajaribu kupata picha ya tofauti na wengi walivyozoea, kwa kuona upande wa pili wa vitu au kwa namna ya tofauti.
Tatu; angalia uzoefu wako binafsi.
Baada ya kujiuliza maswali ya tofauti kwenye wazo unalotaka kufanyia kazi, angalia uzoefu wako binafsi kwenye wazo hilo. Usijidharau kwa sababu labda huna elimu kubwa au uzoefu mkubwa kwenye jambo hilo. Labda siku za nyuma umewahi kujaribu kufanya tofauti na ukapata matokeo ya tofauti, hiyo inatosha kukuonesha kwamba kuna uwezekano wa kupata matokeo tofauti na ambayo watu wanapata sasa.
Nne; chagua eneo la ubobezi kwenye wazo lako.
Wazo unalokuwa nalo linaweza kuwa pana, sasa unahitaji kuchagua eneo ambalo utabobea kwenye wazo hilo ili kujitofautisha kabisa na wengine. Badala ya kutaka kufanya kila kitu, unachagua eneo moja ambalo utaweka muda na nguvu zako na kuweza kutengeneza ubobezi mkubwa. Ni kupitia ubobezi huu ndiyo unaweza kupiga hatua kubwa kwenye wazo hilo.
Tano; fanya utafiti.
Watu wengi wamekuwa wanapata mawazo mapya ya kuboresha zaidi, lakini hawanufaiki nayo kwa sababu huwa hawaweki kazi inayopaswa kuwekwa ili mtu kubobea kwenye kitu hicho. Moja ya kazi kubwa unayopaswa kuweka ni kufanya utafiti. Siyo kusoma tafiti, badala yake kufanya utafiti mpya, kwa kuangalia yale maeneo ambayo unataka yawe bora kisha kuja na njia bora za kuyaboresha kutoka kwenye tafiti mbalimbali zinazogusa wazo hilo.
Sita; unganisha mawazo.
Kuna maeneo mengine ambayo yameweza kupiga hatua kubwa, ambayo ni tofauti na wazo unalofanyia kazi wewe. hii haikuzuii wewe kujifunza kutoka maeneo hayo. Jifunze kupitia maeneo mbalimbali kwa hatua ambazo watu wameweza kupiga, kisha unganisha mawazo hayo na wazo unalofanyia kazi kuweza kuona jinsi gani ya kuboresha wazo unalofanyia kazi. Kumbuka misingi ya mafanikio kwenye kila eneo inafanana, hivyo kwa kuangalia jinsi ambavyo mawazo mengine yamefanikiwa, utaweza kufanikisha wazo lako pia.
Saba; tengeneza nguzo ya kubeba wazo lako jipya.
Baada ya kuchagua wazo unalotaka kuboresha, ukauliza maswali ya tofauti, ukatumia uzoefu wako, ukafanya utafiti na hata kujifunza kutoka maeneo mengine, unakuwa umejifunza mambo mengi sana kuhusiana na wazo lako jipya. Hapa unakuwa na maarifa na taarifa nyingi ambazo mtu mwingine siyo rahisi kuyaelewa. Hivyo ili wazo lako la kuboresha liweze kueleweka na kutumiwa na wengine, unahitaji kutengeneza nguzo ya kubeba wazo lako. Hapa unatengeneza mfumo unaobeba wazo lako jipya, kwa namna ambayo watu wengine wanaelewa jinsi linavyofanya kazi na matokeo ya tofauti yanavyopatikana.
Kwa hatua hizo saba, unakuwa umekamilisha wazo lako la tofauti, ambalo linaleta matokeo bora kuliko yale ambayo yamezoeleka. Baada ya hapo sasa unakwenda kwenye hatua ya pili ambayo ni kujenga wafuasi kwenye wazo lako.

No comments:

Post a Comment