Saturday, July 18, 2020

NO GAINS WITHOUT PAINS---HAKUNA FARAJA / FURAHA / FAIDA BILA MAUMIVU

Mpendwa msomaji wa MAISHA NA  MAFANIKIO  BLOG (  LIFE  AND YOU) , napenda nianze kwa kusimulia jinsi nilivyokosa FARAJA kwa kuandika makala hii: 
“Leo nimeamka usiku saa tisa na nusu, na tayari nimeanza kuandika makala hii ambayo upo unaisoma. Lakini NIMEKOSA FARAJA kutokana na uwepo wa mbu wengi wanaonisumbua sana, achilia mbali hatari ya kuambukizwa ugonjwa wa malaria. Niko tayari KUKOSA FARAJA, kwasababu ni kwa njia hii nitaweza KUPATA FARAJA kama ambavyo imekuwa ikitokea pale wasomaji wa mtandao wa MAISHA  NA  MAFANIKIO BLOG ( LIFE  AND  YOU ) wanaponitumia ujumbe kuwa makala zangu zina mchango mkubwa kwenye maisha yao”. . 
Kisa hiki cha mbu walionisumbua kinatuonyesha kwamba, FARAJA ni kitu kizuri sana kwa binadamu na kwa wengine ni kichocheo kikubwa kwao kufanya kile wanachokifanya. 

Niseme tu, FARAJA ni ile hali ya kujisikia vizuri na huru kutoka kwenye maumivu, matatizo au msongo wa mawazo. 

Ukweli ni kwmba watu wengi wanapenda FARAJA. Matokeo yake FARAJA imekuwa ni kizingiti kikubwa katika kuyafikia maisha ya mafanikio na utajiri. 

Watu wengi wemejikuta wakishindwa kuchangamkia fursa kwasababu fursa nyingi ambazo ni kubwa zinakutaka huwe tayari kukosa FARAJA kwa muda Fulani ndio upate tena. 

Kutokana na tabia hiyo ya kupenda sana FARAJA, wengi wamejikuta wakifanya vitu vidogo vidogo sana na vya kawaida ILIMRADI tu haviwaondoi kwenye FARAJA yao ya awali. 

Ni vizuri kutambua kwamba FARAJA endelevu itapatikana kwa wale ambao wako tayari kukosa FARAJA kwa muda. 

Ukweli ni kwamba, vitu vingi vyenye kuleta FARAJA ENDELEVU vinafanyika katika mazingira ya kukosa FARAJA. 

Mfano ukitaka kuwa na afya nzuri, lazima uwe tayari kuacha kula vyakula Fulani hata kama ni vitamu sana, lazima uwe tayari kupunguza sukari, lazima kuamka mapema na kufanya mazoezi—hapa lazima uwe tayari kukosa raha ya usingizi wa asubuhi n.k, 

Wengi wetu katika kusaka mafanikio huwa tunapenda njia iliyonyooka. Martin Luther King aliwahi kusema kuwa;
“Kipimo kizuri cha binadamu siyo mahali aliposimamia wakati wa FARAJA, bali pale anaposimamia wakati wa changamoto na ubishani.”
Binadamu tuna tabia ya asili ya kuegemea zaidi kwenye HADHI tuliyonayo na tunapinga kile tusichokijua, ili tuweze kuendelea kukaa na FARAJA yetu. 

Tabia ya kupenda FARAJA inafungamana na tabia ya mababu zetu ya kuhofia kuhatarisha maisha. Tunaogopa kujaribu vitu vipya. Tunataka tukwepe mabadiliko. 

Kwahiyo, hatujisukumi mbele kwenda katika kiwango kingine cha maisha mazuri. Katika dunia ya sasa ya usumbufu na inayobadilika kwa kasi, inasaidia wewe kubadilisha mahusiano yako na mabadiliko na kuwa tayari kufurahia KUKOSA FARAJA. 

Wengi tunafikiri maisha ni kutafuta ulinzi na usalama na FARAJA peke yake. 

Hivi vitu ni muhimu na ni sehemu ya maisha ya kila siku, LAKINI maisha yamejaa RAHA na MAUMIVU, KURIDHIKA na KUTESEKA, URAHISI na UGUMU. 

Kwa kuangalia tu! upande mmoja wa sura ya FARAJA, tunajitenga na safu kamili ya uzoefu wa maisha ya binadamu—na maarifa, ujuzi na huruma itokanayo na upande mwingine wa (KUKOSA FARAJA). 

Kama haujisikii vizuri KUKOSA FARAJA, bilashaka huwa unakaimbia mabadiliko. Katika dunia ya sasa, huwezi kukimbia mabadiliko! 

Kila kitu kiko katika hali ya kubadilika mara kwa mara. Ngozi yetu ubadilika, majani ubadilika, watu ubadilika. Kwahiyo suala la kubadilika linatokea kila mahali muda wowote. 

Kuishi kikamilifu, lazima uwe tayari kukanyaga kwenye visivyojulikana, sasa hivi kuliko siku zote. Mfumo wetu wa kufanyakazi kidigitali na utandawazi unakuhitaji kufanyiakazi hata vile usivyojulikana pale unapoanza. 

Lazima uwe tayari kujipa changamoto ili kukua na kubadilika. Na mabadiliko huwa yana harufu ya KUKOSA FARAJA kwa wengi wetu. Woga na wasiwasi na kukosa FARAJA ni asili ya mapambano ya kimaisha kwa binadamu. 

Kujifunza namna ya kuwa na FARAJA kwa KUKOSA FARAJA, pengine ni mojawapo ya somo muhimu sana ambalo nimejifunza kama mjasiriamali. 

Anza leo kujiandaa na uzoee wakati Fulani KUKOSA FARAJA ili kupata FARAJA ENDELEVU hasa wakati huu unapoanza safari yako ya mafanikio. 

Kuendelea kujipatia ujuzi na maarifa juu ya pesa, kazi, biashara, ujasiriamali, afya, uongozi na suala zima la uchumi wa kaya; jaribu kuendelea  kusoma  na  kujifunza  katika  MAISHA  NA  MAFANIKIO  BLOG ( LIFE  AND  YOU )

MILIKI MUDA WAKO SASA , MUDA USIKUMILIKI.

Nimesikia mara nyingi sana watu wakilalamika kuwa hawana muda. Kupitia malalamiko haya, nimejikuta nikijiuliza maswali mengi kama haya;”kwamba muda huwa unatoka wapi? Nani huwa anagawa muda? Nani ni mmiliki wa muda? Je mimi ndiye mmiliki wa muda? Au muda unanimiliki mimi. 

Katika kutafakari maswali yote haya nimegundua kwamba... MUDA ni dhana ambayo ilitengenezwa na binadamu hasa baada ya kutambua kuwa kuna kifo. 

Hii inasaidia katika kupima utendaji wa shughuli za kimaisha kwa lengo la kuuambia mwili wako kuwa unatakiwa kukamilisha vitu Fulani kwa muda Fulani. 

Katika dhana hii ya muda, tunapata kufahamu kuwa kuna makundi ya watu aina mbili; kundi la kwanza ni lile LINALOMILIKI MUDA na kundi la pili wale WANAOMILIKIWA NA MUDA – yaani watu wanamilikiwa na muda. 

Kundi la wale WANAOMILIKI MUDA, ni watu wanaojua kuwa wana wajibu wa kuwa wachoyo wa muda wao. 

Yeyote anayemiliki muda inamlazimu kuwa mchoyo wa muda wake ili kuutumia kuzalisha thamani ambayo wanaweza kufaidi hata wale ambao uliwanyima muda wako mwanzoni. 

Kuwa mchoyo wa muda wako ni busara ilimradi unawagawia watu wengine kile kitokanacho na matumizi ya muda wako. 

Acha ku-manage muda na badala yake anza KUUMILIKI, 

MUDA ni mali ghafi ya kupata kitu chochote cha thamani. MUDA ni kitu pekee duniani ambacho huwezi kirudisha kikishapotea. 

Poteza pesa lakini unaweza kutengeneza pesa nyingi. Poteza ajira lakini unaweza kupata ajira nyingine. Lakini poteza muda na hautaupata tena. 

Kuna masaa 168 katika wiki. Na una wastani wa dakika 2,400 kila wiki. Huu ni muda mwingi sana. Unaweza kwenda wapi? Au muda huu wote unautumia wapi? 

Mambo makubwa yanaweza kufanyika kwa siku kama ukijua ni nini cha kufanya kwa muda husika. 

Pindi ukiacha kusimamia MUDA na badala yake chukua umiliki wa muda wako, ni rahisi sana kuongeza uzalishaji na kuacha kufanya vitu ambavyo huvipendi. 

“Kuna njia nne za kutumia muda wako: Kuwaza, mazungumzo, kutenda na usumbufu”- Chagua kwa busara 

Wewe peke yako unaweza kuchukua umiliki wa MUDA WAKO na uamue ni muda gani utatumia kwenye KUFIKIRI, MAZUNGUMZO, KUTENDA na hata USUMBUFU WA MAKUSUDI mbao utakupelekea kufikia mafanikio. 

Kama hujaajiriwa na mtu, maana yake unamiliki masaa yote 24. Lakini kama wewe uko kwenye ajira maana yake unamiliki masaa 16, yaani.. (masaa 24 KUTOA Masaa 8). 

Kwa mwajiriwa tunatoa masaa 8 kutoka kwenye masaa 24, nikiwa namaanisha yale masaa 8 yalishauzwa kwa mwajiri na thamani yake ni huo mshahara unaoupata kila mwisho wa mwezi. 

Kwahiyo, ulinde sana muda wako kama uwekezaji wa thamani. Upangia kazi MUDA wako kila wakati. 

Kila shughuli ya siku lazima ikamilishwe kwa muda uliopangwa. Na kikubwa zaidi kila shughuli lazima iwe ni ile inayochangia kwenye ndoto yako kwa siku, mwezi au mwaka. Ufinyu wa muda utakusukuma kuzingatia na kuwa mwenye ufanisi katika kile unachokifanya. 

Bila wewe kujali mambo yaliyo mbele yako, jitahidi kuwa wazi, ili ujue ni kipi cha kuzingatia na kimsingi ujue ni kipi cha kufanya pale unapopata muda wa ziada! 

Kumiliki muda wako siyo kuwa na muda wa kukaa bure; BALI ni kujua unataka nini na kutumia muda wako kufanya vitu vyenye tija na vinavyokusogeza au kukufikisha kwenye ndoto yako. 

Unahitaji kuanza leo kumiliki MUDA wako na kama suala la kumiliki muda wako ni jambo la kipaumbele kwako, basi endelea kufuatilia tandao huu wa MAISHA   NA   MAFANIKIO  BLOG ( LIFE   AND  YOU )

SIRI ( 09 ) ZA MAISHA NA MAFANIKIO ZA KUPATA CHOCHOTE UNACHOTAKA KWENYE MAISHA.

Ukiwachukua watu 100 kutoka eneo lolote lile, kumi watakuwa na mafanikio makubwa kuliko 90 na mmoja kati yao atakuwa na mafanikio makubwa kuliko wote.
Ni namba hizi ndiyo zimekuwa zinawachanganya watu, wasielewe kwa nini wachache sana ndiyo wafanikiwe huku wengi wanaopenda kufanikiwa wakiwa hawafanikiwi.
Kiu ya kutaka kupata siri za mafanikio siyo ya zama hizi tunazoishi, imekuwepo tangu enzi na enzi.



Mwaka 1912 mwandishi Orison Swett Marden alikusanya pamoja ushuhuda wa wale waliofanikiwa, kwa namna walivyoeleza wao wenyewe na kuja na kitabu alichokiita; How They Succeeded: Life Stories of Successful Men Told by Themselves. Kitabu hicho kimesheheni hadithi za watu waliokuwa na mafanikio makubwa sana kipindi hicho, kwa namna ambavyo walieleza wenyewe.
Ni kitu kimoja kusoma hadithi ya mafanikio ya mtu inayoelezwa na wengine na ni kitu kingine tofauti kabisa kusoma hadithi hiyo ikielezwa na mtu mwenyewe.
Upekee wa kitabu hiki, unatufanya tuwasikie wenyewe wanasemaje kuhusu mafanikio yao.
Mmoja wa watu waliofanikiwa ambaye hadithi yake inapatikana kwenye kitabu hiki ni aliyekuwa mwandishi Amelia E. Barr (March 29, 1831–March 10, 1919). Ambaye pamoja na kupoteza mume wake pamoja na watoto wake watatu kati ya sita aliokuwa nao, aliweza kufikia mafanikio makubwa sana kwenye uandishi.
Kwenye insha yake iliyo kwenye kitabu hiki, ameshirikisha siri 9 za mafanikio kutokana na uzoefu wake binafsi.
Hapa tunakwenda kujifunza siri hizo kama alivyoeleza mwenyewe, kisha nitaongeza hatua ya wewe kuchukua ili kuweza kufanikiwa sana.
( 01). KUWA   TAYARI   KWA  MAUMIVU
Amelia; watu wanafanikiwa kwa sababu wako tayari kupokea maumivu wanayopitia ili kufanikiwa. Juhudi na uvumilivu ni muhimu na wote waliofanikiwa walifanya maamuzi na kung’ang’ana nayo. Wanajua kusudi lao na wanafanya maamuzi ya kulifikia.
Somo; jua hasa nini unachotaka kwenye maisha yako, amua kwamba utapata kitu hicho na chukua hatua kukipata. Usikate tamaa hata kama unapitia maumivu makali kiasi gani, hakuna aliyewahi kufanikiwa bila ya kupitia maumivu.
( 02 ). WEKA  KAZI  KILA  SIKU.
Amelia; mafanikio ni zawadi kwa wale ambao wanaweka kazi kila siku. Hii ndiyo siri kuu ya mafanikio, kuweka juhudi kuliko wengine wanavyoweka. Kama kuna kitu hujui, utajifunza kwa kufanya. Na hata pale unapopata matokeo usiyotegemea, usiache kuweka juhudi mpaka umepata unachotaka.
 (03 ). USISUMBUKE  NA  WANAOKUPINGA.
Amelia; safari yako ya mafanikio haitakuwa rahisi, utakutana na vikwazo na moja ya vikwazo hivyo ni watu watakaochagua kuwa maadui wako na kukupinga kwenye kile unachofanya. Usiumizwe na upingaji wa wale wanaokupinga, badala yake utumie kupiga hatua zaidi. Ukinzani una nguvu ya kukusukuma zaidi.
Somo; usitegemee kila mtu akubaliane na wewe, wengi watakupinga, kukukosoa na kukukatisha tamaa. Lakini kumbuka kitu hiki kimoja, wote hao hawajui nini unataka na uko tayari kujitoa kiasi gani kukipata. Hivyo usiumizwe na ukosoaji wao, kama kuna kitu chenye manufaa wanakigusia kifanyie kazi, kama hakuna wapuuze na endelea na safari yako.
(04 ). BAHATI  INAUZWA.
Amelia; kosa kubwa kwenye mafanikio ni kufikiria kwamba ni jambo la bahati, kwamba wanaofanikiwa wanakuwa wamepata bahati. Dunia inaendeshwa na sheria kali ambazo hazitoi nafasi kubwa kwa bahati kufanya kazi. Asili huwa inauza vitu vyake, huwa haivitoi bure, hivyo hata bahati, utainunua, hutapewa bure.
Somo; ni kweli waliofanikiwa wanakutana na bahati fulani, lakini bahati hizo huwa haziwafuati wakiwa wamelala kitandani, bali zinawakuta wakiwa wanaweka kazi kwenye kile wanachotaka. Hivyo kama unataka kukutana na bahati, lazima ulipe gharama ya kuwa tayari kuweka kazi. Kama ambavyo tumekuwa tunajifunza, bahati ni pale maandalizi yanapokutana na fursa.
(05 ). PASHA  CHUMA  MOTO.
Amelia; kwa miaka tumekuwa tunaambiwa tuziangalie fursa, kupiga wakati chuma ni cha moto. Ni vizuri, lakini itakuwa bora kama tutakifanya chuma kuwa cha moto kwa kupiga, badala ya kusubiri chuma kiwe cha moto ndiyo tupige.
Somo; usisubiri mpaka fursa ije ndiyo uanze kuchukua hatua, badala yake anza kuchukua hatua na utakutana na fursa. Ukiwa kwenye kuchukua hatua inakuwa rahisi kuziona na kuzitumia fursa kuliko ukiwa unasubiria mpaka fursa ije huku hauchukui hatua. Usisubiri chuma kiwe cha moto ndiyo upige, kipige chuma mpaka kiwe cha moto.
(06 ). UNAHITAJI  MUDA.
Amelia; kila kitu kizuri kinahitaji muda, usiwe na haraka kwenye kazi yako. Weka muda na zama ndani kwenye kazi yako, kadiri unavyoweka muda zaidi ndivyo inavyokulipa zaidi. Kazi za hovyo hufanywa kwa haraka, akili kubwa ni kujipa muda wa kufanya vizuri kile ambacho wengine wanafanya vibaya.
Somo; hakuna njia ya mkato ya kufikia mafanikio makubwa, yeyote anayekuambia njia hiyo ipo anataka kukutapeli. Jipe muda, kama ukiwahi sana jua itakuchukua miaka 10, lakini mara nyingi ni zaidi ya hapo. Acha papara za kutaka mafanikio ya haraka, hayapo. Jipe muda, weka muda wa kutosha kwenye kazi yako, jua kwa kina kile unachokifanya na kazana kuwa bora, kila unachoweka kitakulipa zaidi.
(07 ). KUWA  NA  MPANGILIO.
Amelia; kazi inayofanywa bila mpangilio siyo kazi nzuri, ni uzembe au mtu anayefanya ana matatizo ya akili. Siwezi kuamini kati ya mtu ambaye hana mpangilio, kazi ambayo ni ya hovyo, duni na isiyoeleweka.
Somo; kuwa na mpangilio kwenye kila eneo la maisha yako, tenga muda wako kwa mambo sahihi na utumie hivyo, pangilia vizuri eneo lako la kazi na kila eneo la maisha yako pia. Usiwe mtu wa kukurupuka na kufanya kila kinachokuja mbele yako. Tenga muda wa kazi na fanya kazi, tenga muda wa kupumzika na pumzika. Kazi yako ifanye kwa namna ambayo mtu akiona anajua kweli umeweka juhudi kwenye kuifanya.
(08 ). HESHIMU  KAZI  YAKO.
Amelia; usijione wewe ni bora kuliko kazi au biashara yako. Kuwa mnyenyekevu, heshimu kile unachofanya na kipe heshima na umakini wa kutosha. Hata kama kuna vitu vingine unafanya, usichukulie kitu hicho kama ni cha pembeni. Kama ni mwandishi na pia ni daktari, usichukulie uandishi kama kitu cha pembeni, bali kipe heshima kama kitu kikuu kwako.
Somo; weka moyo wako wote, akili yako yote na umakini wako wote kwenye kile unachokifanya. Kwa maana hiyo, unahitaji kuchagua vitu vichache ambavyo utavifanya vizuri kwa kuweka kila kitu chako kwenye vitu hivyo na kupuuza vitu vingine vyote. Acha kuhangaika na kila kitu, kutawanya nguvu na umakini wako, maana hilo litakuzuia wewe kufanikiwa.
(09). USIWE   NA  HASIRA.

Amelia; usiangukie kwenye hasira na hisia nyingine hasi pale unapokutana na majaribu. Mara zote kuwa na furaha na moyo mkunjufu, ifanye kazi yako kwa moyo mmoja na amua kuweka kila kikwazo pembeni. Na zaidi ya yote kuwa na furaha huku ukijua utapata unachotaka kama hutakata tamaa.
Somo; mambo hayatakwenda kama ulivyopanga, utakutana na vikwazo vya kila aina, wakati mwingine watu watakuzuia au kukukwamisha kwa makusudi kabisa. Hali hiyo itaibua hisia hasi ndani yako, hasira, chuki, kinyongo na nyingine. Epuka kuruhusu hisia hizo kukutawala, badala yake ziondoe na tawaliwa na hisia chanya ya furaha na matumaini. Endelea kuweka juhudi huku ukijua kila kikwazo kitashindwa kama wewe hutakata tamaa.
Angalizo; Amelia anatoa angalizo hili kuhusu siri hizi za mafanikio; kuna watu unaweza kuwaona wamefanikiwa kwa kutumia njia ambazo siyo sahihi, lakini jua hili, mafanikio yao hayatadumu kwa muda mrefu. Asili huwa haiibiwi, huwa inalipa kila ambacho mtu anafanya. Anayepata mafanikio kwa njia zisizo sahihi atalipa kwa kuyapotea. Na wewe unayetumia njia sahihi, hata kama utachelewa, utafikia mafanikio makubwa kama unavyotaka.
Amelia pia anashirikisha kwamba msingi wa mafanikio yake ulijengwa miaka mingi kabla hajafanikiwa. Alianza kuyaona mafanikio baada ya miaka 45 ya kazi bila ya kuchoka ndiyo alipata alichokitaka. Anasema mara nyingi akili yake ilikwamisha, mikono yake ilimkwamisha, miguu yake ilimkwamisha, lakini anashukuru roho yake haikuwahi kumwamisha.
Na hicho ndiyo unachohitaji ili ufanikiwe, roho ambayo haitakukwamisha, imani na matumaini kwamba licha ya kupitia magumu, bado utafanikiwa kama tu hutakata tamaa.

Thursday, July 9, 2020

JE , WAHITAJI KUFANIKIWA SANA NA KUFIKA MBALI ? ZINGATIA MAMBO HAYA .


Kama unataka kujenga maisha yako ya mafanikio, na ukajikuta mbali sana, unaweza ukazingatia sana mambo haya mawili tu. Haya ni mambo ambayo yamewasaidia sana wengi kufanikiwa;-

 #1. Linda kazi yako ya siku na anzisha biashara ya muda.
Kama umeajiriwa anza na kulinda kazi yako kwanza, na kama umejiajiri, chunga sana kipato chako, hiyo inakusaidia sana, kujifunza biashara, na kuchukua uzoefu mkubwa wa biashara. Pia inakusaidia kuchukua umiliki wa maisha yako ya baadae, ya kwamba utakuwa wapi mara baada ya muda fulani.
Kwa kadri unavyokuwa kwenye ajira au biashara yako na huku unafanya biashara nyingine ya pembeni itakusaidia sana kujifunza mengi ambayo usingeweza  kujifunza kama usingeanza kabisa biashara hiyo.

 #2. Wekeza katika nyumba.
Ukiwekeza katika nyumba, ama "real estate" ni rahisi kwa benki kukupa mkopo na ukasonga mbele sana kimafanikio. Hivyo kazana kujenga nyumba hata kama ni ndogo ndogo tu, kwa ajili ya mikopo.
Wawekezaji wengi, wanafanikiwa kwa sababu ya kutumia mikopo ya nyumba. Unasubiri nini, anza kuwekeza kidogo kidogo kwenye nyumba ili ikusaidie kuchukulia mkopo, ila hakikisha isiwe nyumba yako ya kuishi.

JINSI YA KUENDANA NA MABADILIKO YA KIDUNIA YANAYOTOKEA KILA SIKU.


Wakati mwingine unapaswa kuelewa kwamba kile ambacho unakijua leo baada ya miaka mitano ijayo kinaweza kisiwe na faida tena au kinaweza kisilete matokeo yale ambayo mwenyewe unayapata kwa sasa. Nimesema hayo kwa sababu kwa hivi sasa mambo yanabadilika sana.

Ile dunia ya jana si dunia ya leo. Mambo kila kukiacha yanabadilika sana, watalamu nao hawalali kutwa wanaumizwa vichwa vyao kuweza kugundua mbinu mpya ambazo ni rahisi kwa mwanadamu kuweza kumrahisishia kazi mbalimbali.
Kama nilivyosema hapo awali kwamba dunia inakwenda kasi hivyo  ili kuendana sawa na mabadiliko hayo ni kwamba hata wewe unapaswa kubadilika pia. Na njia pekee ambayo itakayokusaidia kwa namna moja ama nyingine kuwa bora zaidi kwenye kila eneo unalofanyia kazi ni kwamba unatakiwa kujiimarisha wewe mwenyewe kila siku.

Na njia pekee itakayokusaidia kuweza kujiimarisha ni kwamba unatakiwa kuhakikisha kwamba unaenda na mabadiliko yanayotokea kila siku, ni  kujifunza mambo mapya kila wakati kwa sababu usipojifunza mambo mapya ni kwamba utapitwa na vingi.

Ni muhimu kuelewa kwamba kwenye kila sekta unayoifanyika kazi unapaswa kujifunza namna ambavyo utakuwa bora  kila wakati.  Kumbuka kujifunza hakuna mipaka hivyo ni muhimu sana kwako kuweza kujifunza mambo mbalimbali yatakayokusaidia kwa namna moja ama nyingine kuwa bora zaidi kwenye kile unachokifanya kila wakati kwani pindi utakaposhindwa kufanya hivyo ni kwamba hata wewe utapitwa na utashindwa kuendana na kasi ya mabadiliko ya kidunia yanayotokea.

Kwa muktadha huo, unapaswa kila wakati uwekeze muda mwingi kwenye kujifunza vitu vipya kila siku. Kama wewe ni mkulima basi ni  jifunze mbinu mpya kila siku zitakazokuwezesha kufanikiwa zaidi katika kilimo hicho, kama wewe ni mtalamu wa jambo fulani basi yakupasa kuweza kujipambanua zaidi kwa kujiwekeza kwenye kupata maarifa sahihi juu ya jambo hilo.
Ni muhimu kupata maarifa fulani kila  wakati  kwa sababu kwa sasa dunia inakwenda kasi sana hivyo bila kuwa na maarifa mapya ni kwamba utazidi kuwa mtu wazamani kila siku , kwani kila kitu ambacho kitakuwa kinafanywa na watu wengine kwako kitakuwa kigeni.

Mwisho naomba nitamatishe kwa kusema ya kwamba kila wakati ongeza ubobezi kwenye kila eneo unalofanyia kazi kwa sababu ubobezi humsaidia mtu kuweza kufanya jambo lililo bora zaidi, pia kila wakati unapaswa kuelewa kwamba ubobezi hupatikana kwa kuweza katika kujifunza vitu vipya kila siku ili uweze kuendana na mabadiliko ya kidunia.

JE , WAHITAJI KUFIKIA NDOTO ZAKO ? FANYIA KAZI MAMBO HAYA :--


Kila mtu anatamani kuzifikia ndoto za maisha yake ya mafanikio. Kwa sababu hiyo kila mtu huchukua hatua anazoziona yeye zinamfaa ili kutimiza malengo hayo. Je, ni wangapi wanajua kuwa huwa wanachukua hatua sahihi au la.?
Katika makala haya, ni lengo langu ni kukumbusha wewe, mambo ya msingi na kama utayazingatia mambo haya yatakusaidia wewe kuweza kukufikisjha kwenye ndoto zako za mafanikio. Je mambo hayo ni yapi?


1. Andika malengo yako.
Najua malengo yako unayajua vizuri tu, lakini kuna sababu muhimu sana kwa wewe kuyaandika malengo yako tena. Chukua kalamu na karatasi, na andika vitu vyote unavyotaka kuvifikia kwenye maisha yako.
Fikiria juu ya kitu ambacho unataka kufanya au unahitaji kukifanya. Inaweza kuwa kitu chochote kama malengo ya afya au malengo ya biashara yako. Orodhesha vitu vingi iwezekanavyo, lakini viwe vile unavyotaka kuvifanikisha.

2. Weka vipaumbele vya malengo yako.
Ndio, najua umeandika malengo mengi, lakini ukweli ni kwamba huwezi kuyatimiza yote. Ili uweze kuyafikia malengo hayo,  yagawawe kwa kuzingatia vipaumbele. Unapaswa kujua, malengo yapi uanze nayo na yapi uyaache.
Kwa kuweka vipaumbele itakupa nguvu wewe, ya kuweza kuyafikia malengo yako kwa urahisi. Na ukishaweka vipaumbele, usibabaishwe na malengo mengine yatakayotokea hapa katikati, vipaumbele vyako vinatosha, vitekeleze kwanza.

3. Vunja vunja malengo yako.
Vunja kila lengo kuwa dogo ambapo unajua unaweza kutimiza kwa urahisi. Hakikisha pia unajipa muda wa wewe kutekeleza malengo yako kulingana na wakati uliokadiriwa wa mradi huo uliojiwekea.
Kwa mfano, ikiwa lengo lako ni kusoma kitabu. Usijilazimishe kusoma kurasa mia moja, kwa mara moja, soma kurasa chache na zielewe. Fikiri kama unataka kujifunza kuogelea, je! Ungeingia ndani ya bahari au ungeanza kwanza kujifunza katika dimbwi?

4. Amua kuwajibika.
Lengo kuu ni kuishi maisha bora ya kufikia malengo yetu na kufanya hivyo lazima tuchukue hatua moja kwa wakati mmoja na kwa hiyo tunahitaji msimamo thabiti. Je! Unahakikisha vipi malengo yako yanatimia?
Hapa hakuna ujanja, unatakiwa kuwajibika. Fanya kila linalowezekana kwa wewe kuamua kuwajibika ili kuhakikisha malengo yako yanatimia. Ukikubali kuwajibika nakupa uhakika unaweza kufanikiwa na kufika mbali kimafanikio.
Fanyia kazi mambo hayo na hakikisha unachukua hatua kuona ndoto zako zinatimia.

JE , UNATAKA KUACHA KAZI YA AJIRA ? KABLA YA KUFANYA HIVYO ZINGATIA HAYA KWANZA.



  Jambo #1. Kabla hujaacha kazi, unatakiwa ujue, jinsi ya kubadilisha bahati mbaya na kuwa bahati nzuri.

Kama hujui jinsi ya kubadilisha bahati mbaya, na kuwa bahati nzuri, usijaribu kuacha kazi utajiumiza sana. Ujasiriamali una mambo mengi sana ya changamoto.
Hivyo kwa kadri unavyokutana na changamoto ngumu kabisa, unatakiwa ujue jinsi ya kuzibadilisha changamoto hizo na kuwa bahati nzuri. Kama ukishindwa, basi tulia na ajira.

 Jambo # 2. Kabla hujaacha kazi, unatakiwa kujua, ni shughuli zipi zinatengeneza biashara ya mafanikio.

Biashara haihusishi mauzo tu peke yake. Kama ndio umetoka kwenye ajira na una akili ya kuwaza mauzo peke yake, utakwama. Unatakiwa ujue biashara inahusisha mambo mengi.
Zipo shughuli nyingi zinazotengeneza mafanikio ya biashara kama huduma kwa wateja, usafi, au mawasiliano mazuri na wateja. Kabla hujaacha kazi, unatakiwa kuzingatia haya kwanza.


Jambo  #  3.  Kabla  hujaacha kazi,  unatakiwa  ujue,  umuhimu  wa kujiendeleza binafsi.
Kama utaingia kwenye ujasiriamali na umegoma kujiendeleza, utashindwa sana, kwa sababu kwenye ujasiriamali zipo changamoto nyingi na zinazotaka kichwa chako kiwe kizuri.
Na kwa sababu ya changamoto hizo inatakiwa muda wote uwe bora na pia wanaokuzunguka wawe bora. Yote haya utayapata kwa wewe kuamua kujifunza na kujinoa.

 Jambo # 4. Kabla hujaacha kazi, jifunze kidogo elimu ya uhasibu.


Kwa kujifunza elimu hii, itakusaidia sana kujua mtiririko wa pesa katika biashara, pia itakusaidia kujua bajeti ya biashara na yako kitaalamu zaidi, tofauti na ungekuwa hujui.
Kama kwako ni ngumu kujifunza elimu hii, basi, biashara ikikua kidogo, ajiri angalau mhasibu anayejua vizuri na uwe unamlipa. Hii itakusaidia kujenga biashara yako kwa mafanikio.

 Jambo la #5. Kabla hujaacha kazi, kumbuka kuwa safari yako ya mafanikio inaanzia ndani ya moyo na roho yako.

Hapa kabla hujaacha kazi unatakiwa ujiulize, ndani mwako unaona mafanikio? Hii ikiwa na maana kwamba mafanikio yako lazima uyaone ndani kwanza kabla hayajaonekana kwa nje.
Hata kwa hatua unazochukua inatakiwa zidhihirishe kile kilicho moyoni mwako. Kama mafanikio moyoni huyaoni usijaribu kuacha kazi, maana hata kwenye ujasiriamali hutafanikiwa pia.

 Jambo #6. Kabla hujaacha kazi, unatakiwa ujue, kitu chochote unachotaka kukiuza, kina bei tatu za msingi. Bei ya chini, bei ya kati na bei ya juu.

Kama utachagua kuuza kitu hicho kwenye bei ya chini, unatakiwa ujue pia dakika yoyote ataibuka mtu wa kushindana na wewe. Ili uwe mshindi katika kuuza kwa bei ya chini unatakiwa uwe na njia nzuri sana ya kuuza bidhaa yako.
Kama utachagua kuuza bidhaa zako kwa bei ya juu, pia jifunze kutoa huduma bora. Kama huelewi hili vizuri, nenda kwenye hotel zinazotoa huduma kwa bei ya juu uone vizuri kile wanachokifanya ni nini kwenye biashara zao.

  Jambo #7. Kabla hujaacha kazi, unatakiwa kujua na kukumbuka, mauzo=kipato.

Kama utakuwa unataka kuacha kazi na ukajigundua kwenye mauzo haupo vizuri., nikwambie tu, jifunze kuuza kwanza, halafu ndo uache kazi. Kama huwezi kuuza, hiyo ni shida kwako kufanikiwa.
Tunaambiwa asilimia kubwa ya watu wengi huwa tunazaliwa hatujui kuuza. Hata hivyo unaweza kujifunza kuuza ili uwe mjasiriamali mzuri, vinginevyo utakwama. Anza kujifunza kuuza, utafanikiwa.

 Jambo # 8. Kabla hujaacha kazi, unatakiwa kujua vizuri jinsi ya kutumia pesa zako vizuri.

Ni wazi wajasiriamali walio wengi, hawajui jinsi ya kutumia pesa zao vizuri. Wanajikuta wanatumia tu pesa hawajui zitarudi vipi. Sasa usiingie kwenye mtego huo.
Ili uwe mjasiriamali mwenye mafanikio, unatakiwa kujua kila shilingi ya pesa yako inakwenda wapi. Ukiona unafika sehemu unashangaa pesa zako zimeenda wapi, bado hujajua jinsi ya kuzitumia.

  Jambo #9. Kabla hujaacha kazi, anzisha biashara ya pembeni kwa ajili ya kujifunza ujasiriamali.

Hakuna ambae anaweza akaendesha baiskeli pasipo kujifunza. Hata kwenye biashara mambo yako hivyo, unatakiwa uwe na biashara ya mazoezi kabla hujaacha kazi na kuingia kwenye ujasiriamali.
Usije ukafanya kosa la kuacha kazi, wakati hata hujui ABC za ujasiriamali ziko vipi. Ukiwa unafanya biashara huku umeajiriwa, itakupa ukomavu wa wewe kufanikiwa kibiashara.

 Jambo   #10.   Kabla   hujaacha   kazi,    tafuta   mshauri   wa mafanikio/mentor.

Ni ngumu sana kwa wajasiriamali wengi, kuwa na mshauri wa mafanikio, lakini kabla hujaamua kuacha kazi, hakikisha una mshauri huyu wa mafanikio ambae atakuongoza katika njia sahihi.
Kama unaona kumpata mshauri wako wa mafanikio ni ngumu, basi amua kufanya vitabu viwe ndo mshauri wako. Kwenye vitabu unatakiwa kujifunza sana na itakusaidia kufanikiwa.

  Jambo #11. Kabla hujaacha kazi, tafuta mtandao wa wajasiriamali.

Usije ukakimbilia kwenye ulimwengu wa ujasiriamali, kama huna mtandao wa ujasiriamali. Kitendo cha kuwa na mtandao huu, kitakusaidia sana wewe katika safari yako ya kimafanikio.
Inakubidi utafute mtandao, ambao kwako unaona unakufaa na kukusaidia. Kila wakati jumuika katika mikutano yao ili kupata uzoefu utakaokujenga, kukulea na kukusaidia kufikia malengo.

   Jambo #12. Kabla hujaacha kazi, tazama mtazamo wako.

Ikiwa mtazamo wako unaona tu kwamba ukiingia kwenye ujasiriamali unapata mafanikio ya moja kwa moja, unajidanganya. Inakubidi ujue kwamba zipo changamoto na unatakiwa kuzifanyia kazi.
Ukijua hili, au ukaamua kuingia na mtazamo huu, wa kutambua changamoto za ujasiriamali, utakusaidia kupambana na changamoto zinazojitokeza.
Mwisho; kabla hujaacha kazi, unatakiwa uwe na imani sahihi kwenye ujasiriamali na kuielewa vizuri, misingi sahihi ya ujasiriamali.