Saturday, July 18, 2020

MILIKI MUDA WAKO SASA , MUDA USIKUMILIKI.

Nimesikia mara nyingi sana watu wakilalamika kuwa hawana muda. Kupitia malalamiko haya, nimejikuta nikijiuliza maswali mengi kama haya;”kwamba muda huwa unatoka wapi? Nani huwa anagawa muda? Nani ni mmiliki wa muda? Je mimi ndiye mmiliki wa muda? Au muda unanimiliki mimi. 

Katika kutafakari maswali yote haya nimegundua kwamba... MUDA ni dhana ambayo ilitengenezwa na binadamu hasa baada ya kutambua kuwa kuna kifo. 

Hii inasaidia katika kupima utendaji wa shughuli za kimaisha kwa lengo la kuuambia mwili wako kuwa unatakiwa kukamilisha vitu Fulani kwa muda Fulani. 

Katika dhana hii ya muda, tunapata kufahamu kuwa kuna makundi ya watu aina mbili; kundi la kwanza ni lile LINALOMILIKI MUDA na kundi la pili wale WANAOMILIKIWA NA MUDA – yaani watu wanamilikiwa na muda. 

Kundi la wale WANAOMILIKI MUDA, ni watu wanaojua kuwa wana wajibu wa kuwa wachoyo wa muda wao. 

Yeyote anayemiliki muda inamlazimu kuwa mchoyo wa muda wake ili kuutumia kuzalisha thamani ambayo wanaweza kufaidi hata wale ambao uliwanyima muda wako mwanzoni. 

Kuwa mchoyo wa muda wako ni busara ilimradi unawagawia watu wengine kile kitokanacho na matumizi ya muda wako. 

Acha ku-manage muda na badala yake anza KUUMILIKI, 

MUDA ni mali ghafi ya kupata kitu chochote cha thamani. MUDA ni kitu pekee duniani ambacho huwezi kirudisha kikishapotea. 

Poteza pesa lakini unaweza kutengeneza pesa nyingi. Poteza ajira lakini unaweza kupata ajira nyingine. Lakini poteza muda na hautaupata tena. 

Kuna masaa 168 katika wiki. Na una wastani wa dakika 2,400 kila wiki. Huu ni muda mwingi sana. Unaweza kwenda wapi? Au muda huu wote unautumia wapi? 

Mambo makubwa yanaweza kufanyika kwa siku kama ukijua ni nini cha kufanya kwa muda husika. 

Pindi ukiacha kusimamia MUDA na badala yake chukua umiliki wa muda wako, ni rahisi sana kuongeza uzalishaji na kuacha kufanya vitu ambavyo huvipendi. 

“Kuna njia nne za kutumia muda wako: Kuwaza, mazungumzo, kutenda na usumbufu”- Chagua kwa busara 

Wewe peke yako unaweza kuchukua umiliki wa MUDA WAKO na uamue ni muda gani utatumia kwenye KUFIKIRI, MAZUNGUMZO, KUTENDA na hata USUMBUFU WA MAKUSUDI mbao utakupelekea kufikia mafanikio. 

Kama hujaajiriwa na mtu, maana yake unamiliki masaa yote 24. Lakini kama wewe uko kwenye ajira maana yake unamiliki masaa 16, yaani.. (masaa 24 KUTOA Masaa 8). 

Kwa mwajiriwa tunatoa masaa 8 kutoka kwenye masaa 24, nikiwa namaanisha yale masaa 8 yalishauzwa kwa mwajiri na thamani yake ni huo mshahara unaoupata kila mwisho wa mwezi. 

Kwahiyo, ulinde sana muda wako kama uwekezaji wa thamani. Upangia kazi MUDA wako kila wakati. 

Kila shughuli ya siku lazima ikamilishwe kwa muda uliopangwa. Na kikubwa zaidi kila shughuli lazima iwe ni ile inayochangia kwenye ndoto yako kwa siku, mwezi au mwaka. Ufinyu wa muda utakusukuma kuzingatia na kuwa mwenye ufanisi katika kile unachokifanya. 

Bila wewe kujali mambo yaliyo mbele yako, jitahidi kuwa wazi, ili ujue ni kipi cha kuzingatia na kimsingi ujue ni kipi cha kufanya pale unapopata muda wa ziada! 

Kumiliki muda wako siyo kuwa na muda wa kukaa bure; BALI ni kujua unataka nini na kutumia muda wako kufanya vitu vyenye tija na vinavyokusogeza au kukufikisha kwenye ndoto yako. 

Unahitaji kuanza leo kumiliki MUDA wako na kama suala la kumiliki muda wako ni jambo la kipaumbele kwako, basi endelea kufuatilia tandao huu wa MAISHA   NA   MAFANIKIO  BLOG ( LIFE   AND  YOU )

No comments:

Post a Comment