Tuesday, August 13, 2019

KAMA UNATAKA PESA UZA ZAIDI ---------------Elimu Ya Msingi Ya Fedha

Kama kipato chako ni kidogo na hakitoshelezi, tatizo lako kubwa ni moja, unauza kidogo. Na ili kuondoka kwenye hali hiyo ya kipato kidogo na kisichotosheleza unahitaji kuchukua hatua moja; KUUZA ZAIDI.

Usiniambie wewe umeajiriwa na hivyo huwezi kuuza zaidi, kumbuka kuna kitu ambacho unamuuzia mwajiri wako, sasa muuzie hicho zaidi. Mfano moja ya vitu unamuuzia mwajiri wako ni muda wako. Hivyo kuna muda wa makubaliano wa kufanya kazi kwa siku na kwa juma. Sasa wewe muuzie mwajiri wako muda zaidi, kwa kuweka muda wa ziada kwenye majukumu ambayo ni muhimu kwa mwajiri lakini yanakosa muda wa kufanyika. Kadhalika kwenye ujuzi na uzoefu wako, ambavyo ni vitu vingine unavyomuuzia mwajiri wako, jiulize ni wapi mwajiri ana uhitaji au changamoto na wewe unaweza kusaidia zaidi, kisha mshawishi akupe nafasi hiyo kwa mbinu za mauzo ambazo umejifunza.

Kila mtu anaweza kuuza zaidi, na hilo ndiyo suluhisho la kifedha kwa kila aliyekwama.

Unaweza kuuza zaidi kwa wateja ulionao sasa, hapa unawapa bidhaa au huduma ambayo hukuwa nayo awali. Ni njia rahisi kuanzia kwa sababu wateja ulionao tayari wanakujua hivyo hawana wasiwasi sana na wewe.

Lakini pia unaweza kuuza zaidi kwa kuwafikia wateja wapya. Hapa unatafuta wateja ambao bado hawajanufaika na bidhaa au huduma zako kisha unawashawishi wanunue, hivyo unaongeza wateja na mauzo pia.

Kwa vyovyote vile, kila wakati kazana kuuza zaidi, kwa wateja ulionao sasa wauzie zaidi ya wanavyonunua sasa na pia wafikie wateja wapya ambao hawajawahi kununua kwako.

No comments:

Post a Comment