Friday, August 9, 2019

JINSI YA KUWA KIONGOZI BORA

Mpendwa rafiki yangu, Mdau  wangu Jamii yoyote ile iliyostarabika lazima iwe  na kiongozi anayewaongoza. Uongozi ni kitu muhimu sana, kuanzia katika familia zetu mpaka ngazi ya taifa. Eneo ambalo hakuna kiongozi huwa linajulikana kwa sababu wanakuwa hawana mwelekeo.

Kumbe basi, kiongozi ni muhimu kwa sababu anaonesha mwanga au uelekeo wa kule jamii inapotaka kufika. Jamii au watu ambao hawana uelekeo huwa uelekeo wowote unawachukua hii ina maana kwamba hakuna tofauti na bendera fuata upepo.
Ni muhimu sana kila mmoja wetu kujifunza mambo ya uongozi, hata kama huna unaowaongoza basi unajiongoza mwenyewe. Jichukulie wewe ni kiongozi mkubwa na anza kufanya mambo ambayo viongozi wakubwa wanafanya.


JE , NI  NAMNA   GANI   UNAWEZA   KUWA  KIONGOZI  BORA ? 
(1).  Onesha mfano; kiongozi bora ni yule ambaye anakuwa anaongoza kwa mfano.  Kama wewe ni kiongozi eneo lako la kazi unatakiwa kuwa mfano. Kama unasisitiza kuwahi, basi mtu wa kwanza kuwahi atakuwa uwe wewe. Na ukifanya hivyo utashangaa wote wanakuwa wanawahi kazini. Hata siku moja usitegemee kupata kile ambacho hukitoi kwa wengine.
Unapohamasisha juu ya jambo fulani basi hakikisha uwe kinara wa kuwa kwanza katika utekelezaji wa jambo hilo. Usiwe tu mtu wa kuongea bali kuwa mtu wa kuonesha njia, ili na watu wengine wapiti. Utakapoweza kuonesha njia hata wengine nao watakuwa rahisi kupita. Kama kiongozi ukiwa mwoga usitegemee unaowaongoza watakuwa tofauti na wewe.

( 2 ). Uwe mtu makini. Kadiri unavyoonesha umakini katika mambo yako ndivyo watu nao wanakuwa kama wewe. Binadamu wanatabia ya kumsoma mtu ni mtu wa namna gani, wakishajua wewe ni mtu wa namna gani, wala hawawezi kujisumbua tofauti na wewe unavyotaka. Kiongozi unatakiwa kuonesha umakini juu ya yale unayosema.
Kama wewe hujali yale yale unayosema unafikiri naye atajali? Anza kujali kwanza wewe kuonesha kuwa jambo hilo ni muhimu na akiona kiongozi wake yuko makini anajali lazima na yeye atajali. Akili ya binadamu inasetiwa ukishawaseti watu utawaongoza vile unavyotaka wewe na siyo vile wanavyotaka wao.

( 3 ). Uwe mfuatiliaji kweli; kuna viongozi wengine huwa wanaishia kusema tu. Ni bora usiseme kuliko unasema halafu unashindwa kuchukua hatua. Kusema halafu hapana utekelezaji ni sawa na kujidharau. Unamaliza nguvu zako bure tu.
Uwe unafuatilia mambo yako yote jua kile kinachoingia na kinachotoka. Jua kila kitu kuhusu kazi au biashara yako na wale ambao wako chini yako hakikisha wanafuata mwongozo wa kazi. Usitegemee kupata watu makini kama wewe siyo mtu makini. Watu wanakuwa makini kama wewe ukiwa makini.
Hakuna mtu ambaye atakuchezea kama wewe hutaki kuchezewa. Jinsi utakavyojichukulia ndivyo na watu watakavyokuchukulia.
Hatua ya kuchukua leo; kuwa kiongozi wa mfano, kuwa makini, kuwa mfuatiliaji na jali yale unayosema. Ukiishia kusema na watu unaowaongoza wataishia kusikia na kutokufanya.
Hivyo basi, kama unataka mambo yako yaende kama unavyotaka wewe, anza kuwa mtekelezaji wa kwanza wa jinsi vile unavyotaka mambo yako yaende. Utakuwa kiongozi bora kama utakuwa mwaminifu, mwadilifu, mwajibikaji kwenye yale unayosema.

No comments:

Post a Comment