Monday, January 14, 2019

UFUNGUO MKUU WA MAFANIKIO.

  1. Huhitaji kutafuta nguvu nje yako, nguvu tayari zipo ndani yako. Unachohitaji ni kujua nguvu ulizonazo na kuweza kuzitumia. Kila binadamu ana nguvu kubwa ya kiroho ndani yake, na nguvu hii ya kiroho ipo ndani ya fikra zake. Kama akiweza kuzitumia vizuri fikra zake, zitampa chochote anachotaka.
  2. Magumu tunayokutana nayo kwenye maisha ni kwa sababu ya kutokujua nini hasa tunachotaka na pia kutokujua kile kilichopo ndani yetu. Ukishajua kilichopo ndani yako na ukajua kwa hakika nini unataka, na ukapeleka fikra zako kwenye hayo, hakuna kitakachokushinda.
  3. Usilalamikie chochote kinachotokea kwenye maisha yako, kwa sababu umekisababisha mwenyewe na nguvu ya kukibadili ipo ndani ya fikra zako. Fikra zako ndiyo kisababishi, na yale yanayotokea kwenye maisha yako ni matokeo. Hivyo kama hujayapenda matokeo, badili kisababishi ambacho ni fikra zako.
  4. Dunia inaendeshwa kwa upacha, kwenye dini kuna Mungu na shetani, kwenye sayansi tuna chanya na hasi, kwenye falsafa tuna wema na uovu. Lakini yote haya ni hali ya fikra zetu. Kama fikra zikisimamiwa vizuri zinaleta matokeo mazuri, kama zisiposimamiwa zinaleta matokeo mabaya.
  5. Tunaishi kwenye zama za fikra, zama za ubunifu. Wanaofanikiwa ni wale ambao wanaweza kutumia fikra zao vizuri. Kwa sababu dunia imekuwa na vitu vile vile miaka yote, bali wale waliotumia fikra zao vizuri ndiyo wamenufaika zaidi na dunia. Kwa mfano umeme tulionao sasa duniani hauna tofauti na umeme uliokuwepo miaka 200 iliyopita. Lakini leo tuna vitu vingi zaidi vinavyotumia umeme kuliko miaka 200 iliyopita kwa sababu watu wametumia vizuri fikra zao na kuja na vitu vipya.
  6. Zipo njia kuu mbili za kuendeleza na kutumia vizuri fikra zetu. Njia hizo ni umakini na msisitizo. Unaposisitiza fikra zako kwenye kitu kimoja, na umakini wako wote ukawa pale, fikra zina nguvu ya kukupa kile unachotaka. Ukikosa sifa hizo mbili, fikra zako zitakuwa zinahamahama na hutapata unachotaka.
  7. Baada ya kuweka umakini na msisitizo wa fikra zako kwenye kile unachotaka, unapaswa kuwa na taswira ya unachotaka na kuiweka taswira hiyo kwenye fikra zako. Pata picha ya kile unachotaka, kama vile tayari umeshakipata, jione ukiwa ndani ya kitu hicho. Kwa kutengeneza taswira hii, akili yako ya ndani itaona ndiyo maisha yako na kutengeneza maisha ya aina hiyo zaidi.
  8. Kusudi kuu la maisha ni kukua na kuongezeka. Na dunia nzima kwa asili inakua na kuongezeka. Angalia kila kiumbe, kuanzia miti, wanyama na hata samaki, wanaendelea kuzaliana na kukua zaidi. Hivyo ili kufanikiwa kwenye maisha, unapaswa kuwa na fikra za ukuaji.
  9. Tabia uliyonayo siyo kwa bahati mbaya, bali umeijenga wewe mwenyewe kwa juhudi kubwa sana. Umekazana wewe mwenyewe kujenga tabia zote ulizonazo, kwa kuanzia kwenye fikra zako, kwa namna unavyojitambulisha ndani yako. Hivyo ili kubadili tabia, anza kubadili fikra zako na weka juhudi kujenga tabia mpya.
  10. Hakuna uhaba kwenye dunia, bali kuna utele. Dunia ina kila kitu kwa wingi kadiri watu wanavyohitaji. Na hata vikipungua basi itatengeneza zaidi kadiri watu wanavyohitaji. Hivyo hupaswi kufikiri kwenye uhaba bali kwenye wingi, hupaswi kuona mwingine akifanikiwa basi wewe unashindwa. Dunia ina rasilimali za kumtosha kila mtu kufanikiwa.
  11. Maisha yanaendeshwa kwa sheria na kanuni fulani, ukizijua na kuziishi utafanikiwa. Lakini usipozijua basi zitakuumiza. Kwa mfano dunia ina nguvu ya mvutano, ambayo inavuta kila kitu kwenye dunia. Kama hujui kanuni hii na ukajaribu kuruka kama ndege, utaanguka kwenye dunia na kuumia sana. Kanuni ipo pale na kama huijui inakugharimu.
  12. Unahitaji vitu vitatu ili kuweza kunufaika na nguvu ya fikra iliyopo ndani yako. Moja unahitaji kujua kwamba una nguvu ndani yako, mbili, unahitaji kuwa na uthubutu wa kujaribu kuitumia nguvu hiyo na tatu unahitaji kuwa na imani ya kutumia nguvu hiyo.
  13. Sisi binadamu siyo viumbe wa mwili ambao tuna roho, bali sisi ni viumbe a kiroho ambao tuna mwili. Roho ndiyo inayoongoza maisha yetu na ndiyo yenye nguvu ya fikra. Mtu anapofariki, kinachoondoka ni roho, mwili unabaki pale na unakuwa hauna nguvu ya kufanya chochote. Hivyo kama unataka kujiendeleza, endeleza roho yako, endeleza fikra zako na hizi zitakupa unachotaka.
  14. Ulimwengu mzima ni kitu kimoja na tunaongozwa na nguvu moja. Kila kitu kwenye ulimwengu, ukikiangalia kwa undani unagundua ni nguvu ama nishati. Jua ni nishati ya mwanga na jito, ambayo ikifika kwenye mimea inabadilika na kuwa nishati ya kikemikali, mimea ikiliwa na wanyama nishati hiyo inahamia kwa wanyama. Kila kitu kwenye dunia ni nishati, hata sisi binadamu, ukivunja miili yetu mpaka kwenye ngazi ya seli, unagundua sisi ni nishati. Hivyo ulimwengu mzima ni kitu kimoja, nishati.
  15. Kukua ni kupoteza, kupata kipya ni kupoteza cha zamani, hii ni kanuni muhimu sana kwenye mafanikio. Hakuna kiumbe anayekua na kubaki na vitu vya zamani, na huwezi kupata kitu kipya kama bado unang’ang’ana na vya zamani. Ili ukue unahitaji kupoteza kile ambacho tayari unacho sasa. Matatizo mengi ambayo watu wanayapata ni kutokana na kung’ang’ana na vitu vya zamani.
  16. Ipo kanuni kuu ya maisha kwamba kila kitu kinazaliwa, kinakua, kuzalisha na kufa. Na kanuni hii inaenda kwa mzunguko. Kwa mfano kwetu sisi binadamu, kila baada ya miaka saba, maisha yetu yanabadilika kabisa na kuwa mapya. Miaka saba ya kwanza ni ya utoto, miaka saba inayofuatia ni ya kuanza kujifunza majukumu, saba inayofuata ni ya kuanza ukuaji wa utu uzima. Miaka saba mingine ni kufikia ukuaji kamili, inayofuatia ni ya kuzalisha na kuwa na mali na familia. Miaka saba inayofuata, 35 mpaka 42 ni kipindi cha mabadiliko makubwa kimaisha. Inafuatiwa na miaka saba mingine ya kujijenga upya kwenye utu uzima.
  17. Vitabu vya dini vinatuambia kwamba binadamu tumeumbwa kwa mfano wa Mungu. Na hili lina maana kwamba tunazo sifa za uungu ndani yetu. Sifa hizi zipo kwenye fikra, mungu ana sifa ya kuumba na fikra zetu pia zina sifa ya kuumba. Kadhalika kwenye nguvu na ujuzi, fikra zetu zinajua mengi na zina nguvu kubwa. Tukiweza kuzitumia tunaweza kufanya makubwa sana.
  18. Usichotumia unakipoteza. Wengi hujiuliza kama fikra zetu zina nguvu sana kwa nini wengi hawazitumii. Sababu kubwa ni kwamba wengi hawajui kama wana nguvu kubwa kwenye fikra zao, na usichokijua huwezi kukitumia, na usichotumia unakipoteza. Hivyo hatua ya kwanza ya kutumia nguvu zako ni kujua zipo, na kuanza kuzitumia.
  19. Hofu ni matumizi mabaya ya nguvu ya fikra zako. Kwa kuwa na hofu unatumia fikra kutengeneza yale ambayo hutaki yatokee na kwa kuwa fikra zina nguvu, zinaleta hayo hayo unayofikiria. Hivyo unapaswa kuondokana kabisa na kila aina ya hofu, kwa kujua nguvu kubwa iliyopo ndani yako ya kukuwezesha kufanya chochote.
  20. Jukumu lako kuu kwenye maisha, na biashara pekee ambayo inalipa ni kufikiri. Wale wanaoweza kufikiri kwa kutumia akili zao ndiyo wanaokuja na vitu vipya na njia mpya za kufanya vitu na wananufaika sana. tumia nguvu yako ya fikra kufikiri na utaweza kufanya makubwa.
  21. Unapofikiri, unapaswa kufikiri mawazo makubwa sana. Ukifikiri kidogo nguvu iliyopo ndani yako inaleta matokeo madogo. Ukifikiri makubwa nguvu hiyo inaleta makubwa. Usiogope kufikiri makubwa, una nguvu ndani yako ya kupata chochote unachofikiri.
  22. Kinachotutofautisha ni kanuni ya mtetemo (law of vibration). Tumeona kwamba kila kitu duniani ni nishati, je nini kinakutofautisha wewe binadamu na mti? Ni kanuni ya mtetemo. Wewe ni binadamu kwa sababu seli zako zina mtetemo tofauti na za mti. Na hata nishati inapobadilika kutoka mfumo mmoja kwenda mwingine, kinachobadilika ni mtetemo wake. Hata baina ya watu, wale wanaofanikiwa ziadi wana mtetemo wa juu kuliko wale wanaoshindwa. Fikra zetu zinaendana na mtetemo, hivyo tunapokuwa na fikra za juu tunavutia mtetemo wa juu. Unaweza kufananisha nguvu hii ya mtetemo na kutafuta mawimbi ya redio, unasikia redio fulani pale unapofikia kwenye mawimbi yake.
  23. Kanuni kuu ya mafanikio ni HUDUMA. Tunafanikiwa kwa kadiri tunavyowahudumia wengine, tunapata kadiri ya tunavyotoa. Hivyo kama unataka zaidi, unapaswa kutoa zaidi, kama unataka kufanikiwa zaidi unapaswa kuwahudumia wengi zaidi na kwa ubora zaidi.
  24. Ili kuwa huru na ili kupata chochote unachotaka, unapawa kuujua ukweli. Kumbuka kauli inayosema IJUE KWELI NAYO ITAKUWEKA HURU. Watu wengi hawapo huru kwa sababu hawajui ukweli, na usipokuwa huru huwezi kuwa na mafanikio. Ujue ukweli kwa kujua nguvu kubwa iliyopo ndani yako na pia kwa kujua umoja wa dunia, kwamba kila kitu ni nishati na tunavuta vile vitu ambavyo vipo kwenye mtetemo wa fikra zetu.

No comments:

Post a Comment