“There
is only one excuse for a speaker's asking the attention of his
audience: he must have either truth or entertainment for them.” ― Dale
Carnegie
Kama unataka watu wakusikilize unapoongea, unapaswa kuwa na moja au vyote kati ya vitu hivi viwili; ukweli au burudani.
Watu
wanapenda kusikiliza ukweli, ukweli ambao unawawezesha kufanya maamuzi
sahihi na kupiga hatua kwenye maisha yao, ukweli unaowafanya waone wapi
walikuwa wanakosea na hatua sahihi za kuchukua ni zipi. Unapokuwa na
ukweli, watu wanakusikiliza, hasa pale unapokuwa na ushahidi wa ukweli
huo. Japokuwa wakati mwingine ukweli huwa unaumiza na watu wengi
kuukataa, lakini unapousimamia unapata watu wa kukusikiliza. Hii ndiyo
inayosababisha tunawasikiliza waalimu, washauri, au viongozi mbalimbali,
ambao tunajua wana ukweli ambao tunauhitaji.
Watu
wanapenda burudani, watu wanapenda kusahau changamoto zao za maisha kwa
muda na kucheka kidogo. Na hapa ndipo wasanii na wachekeshaji
wanapopata nafasi ya kuwafikia wengine kupitia sanaa zao. Watu
watamsikiliza mtu kama wanaburudika kwa kumsikiliza.
Hivyo
rafiki, kama unataka kuwa mnenaji mzuri, kazana kuweka vitu hivi viwili
kwenye unenaji wako, ukweli na burudani. Kila unapopata nafasi ya
kuongea mbele ya wengine, jua ni ukweli gani ambao unataka watu hao
wajue, labda kuhusu wewe, kuhusu mada unayozungumzia au kuhusu bidhaa au
huduma unayotaka kuwauzia. Ukweli huu uwafanye waondoke na kitu ambacho
hawakuwa wanakijua awali na wawe na hatua za kuchukua ambazo hawakuwa
wanachukua awali. Pia waburudishe watu kupitia unenaji wako, kuwa na
hadithi, mifano au visa ambavyo vinaufukisha ukweli huo kwa njia ambayo
inawaburudisha watu. Unahitaji kuwa na maandalizi ya mifano au hadithi
utakazotumia kwenye unenaji wako, ambavyo vitafikisha ukweli na
kuwaburudisha watu pia.
Zingatia vitu hivyo viwili katika unenaji, ukweli na burudani na watu watapenda kukusikiliza kila wakati bila ya kuchoka.
No comments:
Post a Comment