Rafiki
yangu mpendwa, moja ya vitu ambavyo nimekuwa nakusisitizia sana wewe
rafiki yangu ni kuwa na vyanzo mbadala vya kukuingizia kipato. Hii ndiyo
njia pekee kwako kuweza kupata uhuru kamili wa maisha yako.
Kama
kipato chako kinategemea mtu mmoja au wachache basi haupo huru,
utalazimika kufanya kile ambacho anayedhibiti kipato chako anakutaka
ufanye, hata kama hutaki kukifanya au unaona siyo sahihi kufanya.
Mfano
unapokuwa umeajiriwa na chanzo pekee cha kipato chako ni mshahara
unaopata kwenye ajira hiyo, unajikuta unakuwa chini ya mwajiri wako,
kufanya chochote anachotaka hata kama kwa upande wako siyo kitu sahihi
au muhimu kufanya.
Hivyo
ili kupata uhuru kamili, ili kupata mafanikio makubwa kwenye maisha
yako, unapaswa kuwa na vyanzo tofauti, kipato chako kusitegemee mtu
mmoja au watu wachache.
Zipo
njia nyingi sana za kuongeza njia za kuingiza kipato na hatimaye
kuongeza kipato chako. Lakini njia zote hizi tunaweza kuzigawa kwenye
hatua mbili, ambayo inarahisisha sana uchukuaji hatua wa mtu katika
kuongeza kipato.
Hatua ya kwanza; ongeza thamani zaidi pale ulipo sasa.
Hatua
ya kwanza ya kuongeza kipato chako ni kuongeza thamani zaidi pale ulipo
sasa. Hapa huhitaji kuanza kufanya kitu kipya, bali unaendelea kufanya
kile unachofanya sasa, lakini kwa viwango vya juu zaidi ambavyo
vinakuwezesha kutengeneza kipato zaidi.
Kama
una biashara hapa unakazana kuwahudumia vizuri zaidi wateja ambao
tayari unao, kuongeza wateja wapya na kuwapa vitu vipya ambavyo wateja
wanahitaji lakini kwako havipatikani.
Kama
upo kwenye ajira ni kuongeza thamani unayotoa kwenye ajira hiyo, kwa
kuchukua majukumu mengi na makubwa, kufanya kazi kwa muda mrefu zaidi na
kufanya kazi yako kwa viwango vya juu zaidi. Japokuwa kwenye ajira kuna
ukomo, bado ni sehemu ya kuanzia ili kuondoka kwenye utumwa huo.
Hatua
hii ni muhimu sana kwa kila mtu kuitumia kwa sababu haihitaji uwe na
rasilimali za ziada. Mfano watu wengi wamekuwa wanasema wangekuwa na
fedha wangeanzisha au kukuza zaidi biashara walizonazo. Kwa kuwa
hawapati fedha wanazotaka, basi wanabaki vile walivyo. Kama kila mtu
angefanyia kazi hatua hii ya kwanza na kufanya zaidi pale alipo sasa,
wangeweza kutengeneza kipato zaidi na kwenda kufanya kile hasa
wanachotaka kufanya.
Hatua ya pili; fanya kitu cha tofauti.
Hatua
ya pili kwenye kuongeza kipato chako ni kufanya kitu cha tofauti na
unachofanya sasa. Hapa ndipo unakwenda kuanza biashara mpya kama huna
biashara au kuanza biashara ya tofauti na ile unayofanya sasa au kwenye
eneo tofauti na unalofanyia biashara sasa.
Hii
ni hatua muhimu na unayopaswa kuichukua kwa umakini, kwa sababu
inahitaji maamuzi unayokwenda kuyasimamia kwa muda mrefu. Wengi wamekuwa
wanachukua hatua hii bila ya kujitathmini vizuri na kujikuta
wametengeneza gereza zaidi kwa kile kipya wanachokwenda kufanya.
Mfano
mtu anakwenda kuanzisha biashara mpya wakati biashara anayofanya sasa
bado hajaweza kuiendesha vizuri, kinachotokea ni biashara zote mbili
kufa. Au mtu anatoka kwenye ajira moja na kwenda kwenye ajira nyingine,
kitu ambacho hakibadilishi sana hali yake ya maisha.
Kama
unataka kuongeza kipato chako, anzia hapo ulipo sasa na chagua kitu cha
kufanya zaidi. Kama ni biashara fikiria wateja wapya unaoweza kuafikia,
huduma na bidhaa mpya unazoweza kuwapatia na ubora wa huduma unazotoa.
Kama ni kwenye ajira angalia majukumu makubwa zaidi unayoweza kufanyia
kazi, muda zaidi unaoweza kuweka kwenye kazi zako na thamani kubwa zaidi
unayoweza kuzalisha. Ukishaweka juhudi kubwa kwenye kile unachofanya
sasa, ndipo sasa unaweza kufanya kitu cha tofauti.
Kila
mtu ana fursa nyingi za kufanya zaidi kwenye kile anachofanya sasa,
hebu anza kutumia fursa hizi ili kuongeza kipato chako zaidi.
No comments:
Post a Comment