Pata
picha, unataka kuwa na safari, unaondoka nyumbani umebeba mizigo yako
na kuelekea kituo cha mabasi. Unakaribishwa na kuulizwa unaenda wapi,
unasema popote basi linapokwenda. Je unafikiri basi hilo litakupeleka
wapi?
Unaweza
kushangaa na kujiuliza inawezekanaje mtu mwenye akili timamu aende
kituo cha basi kwa ajili ya safari halafu hajui anakokwenda!
Kabla
hujaendelea kushangaa, hebu jiulize kwanza maswali haya muhimu;
unakwenda wapi na maisha yako? unakwenda wapi na biashara unayofanya?
Unakwenda wapi na kazi uliyonayo? Unakwenda wapi na mahusiano uliyonayo?
Kwa
maneno mengine, miaka 5, 10, 20 na zaidi ijayo unajiona wapi? Kama
huwezi kutoa jibu moja kwamba unajiona wapi katika vipindi hivyo, kwa
hakika huna tofauti na anayeenda kwenye kituo cha mabasi huku akiwa
hajui anakwenda wapi.
Na
hivi ndivyo watu wengi wanavyoendesha maisha yao, wanakazana sana
kufanya chochote wanachofanya, lakini hawajui wanakwenda wapi, hivyo
wanafanya leo kama walivyofanya jana, huku kesho ikiwa haipo kwenye
mawazo yao kabisa.
Kama
mpaka sasa maisha yako huyaelewi, kama umeshajaribu kazi na biashara
nyingi lakini bado huoni matokeo mazuri, tatizo lako ni moja, hujui nini
hasa unachotaka, hujui wapi hata unakotaka kufika.
Na
kama hutachukua hatua ya kwanza muhimu ya kujua kwanza nini unachotaka
na wapi unapotaka kufika, hutaweza kuwa na maisha bora. Kila siku
utaishia kuyumbishwa kama bendera inayopeperushwa na upepo. Watu
watakuja kwako na kila aina ya fursa mpya na utahangaika nazo, na hakuna
hata moja itakayokusaidia kufanikiwa.
Jua
kwanza ni nini hasa unachotaka, jua ni wapi unakotaka kufika, kisha
weka juhudi zako zote katika kufika kule unakotaka kufika. Kuwa kiziwi
na kipofu kwa vitu vingine vyote visivyohusiana na kile unachotaka.
Usiwe mtu wa kukimbizana na kila aina ya fursa mpya, badala yake weka
nguvu kubwa kufika kule unakotaka kufika.
Kujua unachotaka na kuweza kukipata, anza kwa kujiuliza maswali haya muhimu sana;
- Mimi ni nani?
- Ni nini ninachotaka?
- Ni nini kinanipa furaha?
- Nini hakinipi furaha?
- Uimara wangu uko wapi?
- Udhaifu wangu uko wapi?
- Ni mchango gani mkubwa naweza kutoa kwa wengine kupitia maisha yangu, kazi yangu, biashara yangu na mahusiano yangu?
Ukijiuliza
na kujipa majibu sahihi kwenye maswali hayo saba, na kufanyia kazi
majibu hayo, utaweza kupata chochote unachotaka kwenye maisha yako.
No comments:
Post a Comment