Showing posts with label SAIKOLOJIA NA MAISHA. Show all posts
Showing posts with label SAIKOLOJIA NA MAISHA. Show all posts

Friday, June 7, 2019

NJIA ZA KUONDOKANA NA MSONGO NA KUWA NA MAISHA TULIVU.

  1. Acha tamaa.

Chanzo kikuu cha msongo ni tamaa. Pale tunapotamani kuwa na vitu ambavyo vipo nje ya uwezo wetu kwa wakati huo, tunazalisha msongo kwenye miili yetu.

Maisha ya sasa yamejengwa kwenye mashindano ya kijinga. Mashindano ya kutaka kitu kwa sababu kila mtu anacho. Mashindano haya yamepelekea wengi kuingia kwenye madeni ili kupata wanachotaka. Wanaweza kupata wanachotaka, lakini madeni wanayobaki nayo yanakuwa chanzo cha msongo mkubwa kwao.

Acha tamaa, acha kushindana na wengine na ishi maisha yako kwa ukamilifu, fanya kile unachoweza kufanya kwa pale ulipo sasa, na kama kuna kitu kipo nje ya uwezo wako usijilazimishe nacho.

  1. Dhibiti taarifa zinazoingia kwenye akili yako.

Taarifa tunazoruhusu ziingie kwenye akili zetu zina madhara makubwa kwenye miili yetu. Pale ambapo taarifa zinazoingia ni hasi na za kukatisha tamaa, tunaingiwa na hofu na hapo mwili unaingia kwenye msongo.

Tumezungukwa na taarifa nyingi hasi na za kutisha na hata wale waliotuzunguka wana kila njia ya kutukatisha tamaa. Unapaswa kuwa makini ni aina gani ya taarifa unaruhusu ziingie kwenye akili yako na aina gani ya watu unaowasikiliza ili kuepusha kuingia kwenye msongo usio na umuhimu.

Epuka sana kufuatilia habari na pia waepuke sana watu ambao ni wakatishaji wa tamaa na wanaoona magumu mara zote.

  1. Ishi wakati uliopo.

Sababu nyingine kubwa ya msongo ni pale ambapo mtu anashinda kuishi wakati uliopo. Kuna nyakati tatu kwenye maisha yako, wakati uliopita, wakati uliopo na wakati ujao.

Unapojikuta kwenye msongo, kwa hakika utakuwa unaishi wakati uliopita ambapo mambo yameshapita na huwezi kuyabadili au utakuwa unaishi wakati ujao, ambao bado hujaufikia na hivyo huwezi kubadili chochote.

Huwezi kuwa na msongo kama unaishi wakati uliopo, kama mawazo yako yote yapo kwenye kile kitu unachofanya sasa, msongo hauwezi kupata nafasi kabisa. Jifunze kuweka akili yako yote kwenye kitu unachofanya kwa wakati huo, linapokuja wazo la kitu cha nyuma au kijacho liandike pembeni na jilazimishe kurudisha akili kwenye kile unachofanya. Kwa njia hii utaondokana kabisa na msongo.

  1. Ondokana na vilevi.

Wengi wamekuwa wanatumia vilevi kama njia ya kuondokana na msongo, lakini wote tunajua vilevi vinasogeza msongo mbele, unajisahaulisha kwa muda lakini ulevi unapoisha msongo unarudi pale pale.

Vilevi vinazidi kuuchosha mwili na kutengeneza msongo mpya. Hivyo epuka kutumia njia ya vilevi kama sehemu ya kukabiliana na msongo.

Epuka matumizi ya kahawa au sigara, vitu viwili ambavyo watu hutumia sana wanapokuwa na msongo. Kemikali zilizopo kwenye vitu hivi vinauweka mwili kwenye hali ya msongo zaidi.

  1. Fanya mazoezi.

Mazoezi ni njia bora ya asili ya kukabiliana na msongo. Mwili unapokuwa kwenye mazoezi, unazalisha homoni tofauti na za msongo, homoni ambazo zinafanya mtu ajisikie vizuri.

Mazoezi pia ni njia ya kuurudisha mwili kwenye asili yake, kwa sababu sisi binadamu hatukuumbwa kukaa kwa muda mrefu, shughuli za watangulizi wetu zilikuwa za kuhusisha viungo vyote vya mwili. Lakini hali ya sasa tunajikuta tunakaa kwa muda mrefu, kitu ambacho kinachochea msongo zaidi. Unapofanya mazoezi unauondoa mwili kwenye hali ya msongo.

  1. Ongeza ukomavu wako kwenye msongo.

Sababu nyingine kubwa ya msongo kuwa tatizo kwa wengi zama hizi ni kwamba miili yetu haijazoea kabisa mazingira magumu. Tumeishi kwenye kipindi ambacho ni rahisi kupata kila tunachotaka, na hivyo mwili unabweteka na kuwa laini, usioweza kupambana hata na vitu vidogo.

Ondokana na hali hii kwa kuukomaza mwili wako. Unaweza kufanya hivi kwa kuupa mwili msongo wa muda mfupi ambao unakukomaza zaidi. Njia za kufanya hivyo ni kama kufanya mazoezi makali sana ambayo yanakuletea maumivu, lakini unayafanya kwa muda mfupi. Kuoga maji ya baridi kali sana wakati wa asubuhi pia ni njia nyingine ya kukomaza mwili kwenye msongo. Na pia kufunga ni njia ya kuufanya mwili kutokutegemea chakula muda wote.

  1. Tahajudi ya kuondoa msongo.

Njia bora kabisa ya kuondokana na msongo ni kufanya tahajudi (meditation) ya kuondoa msongo. Kwa sababu msongo unaendelea kuwa na sisi kila wakati, ni muhimu kujua jinsi ya kufanya na kuifanya tahajudi hii kila mara na tutaweza kuwa na maisha tulivu sana.

Maandalizi ya kufanya tahajudi ya kuondoa msongo.

Katika kufanya tahajudi hii, unapaswa kutenga sehemu tulivu ambapo unaweza kukaa na kufanya tahajudi bila ya kusumbuliwa. Unapaswa kutenga dakika 5 mpaka kumi za kufanya tahajudi hii. Pia unapaswa kuzima simu yako au kuiweka kwenye utulivu wakati ambao unafanya tahajudi.

Jinsi ya kufanya tahajudi ya kuondoa msongo.

Kaa wima, mgongo ukiwa umenyooka na macho ukiwa umeyafunga.

Pumua kwa kina kwa kuingiza na kutoa hewa kupitia pua, vuta pumzi kwa kuielekeza tumboni, chini kidogo ya kitovu.

Weka mkono wako wa kushoto kwenye goti la kushoto, kiganja kikiangalia juu na kidole gumba kugusana na kidole kidogo.

Tumia mkono wako wa kulia kufunga matundu ya pua yako, tundu moja kwa wakati.

Ingiza pumzi ndani kwa kutumia tundu la pua la kushoto huku ukiwa umeziba tundu la kulia. Toa hewa nje kwa kutumia tundu hilo hilo la kushoto.

Rudia kuingiza pumzi na kutoa kwa kutumia tundu la kulia, huku ukiwa umeziba tundu la kushoto.

Endelea kurudia zoezi hili, tundu la kushoto na tundu la kulia mpaka muda uliotenga wa kufanya tahajudi kuisha (hapo unakuwa umeweka alamu itakayoita baada ya muda uliotenga kuisha).

Muda unapoisha, maliza kwa kupumua kwa kina kawaida kwa matundu yote mawili ya pua na mdomo na hapo unarudi kwenye hali yako ya kawaida.

Hii ni tahajudi rahisi sana kufanya, ambayo itaweza kukusaidia kuondokana na msongo wowote unaokuwa nao. Lakini pia unaweza kuifanya ukiwa popote na kwa muda mfupi na ukapata manufaa makubwa.

Friday, May 24, 2019

UNAPOSHIKWA NA HASIRA , JIPE MUDA WA KUTAFAKARI.

 Ukishagundua kwamba upo kwenye hasira, basi kaa kimya, jipe muda wakutafakari na kutulia na utajiepusha na makosa makubwa unayoweza kufanya ukiwa na hasira.
 
Hasira ni moja ya hisia zenye nguvu sana, na hisia zinapokuwa juu uwezo wetu wa kufikiri unakuwa chini. Hivyo unapokuwa na hasira, unakuwa umetawaliwa na hisia na siyo fikra. Na ni wakati mbaya sana wa kufanya chochote, kwa sababu unaposukumwa na hisia, hujui kipi sahihi kufanya, kwa kuwa hufikiri sawasawa.
 
Hivyo rafiki, unapogundua kwamba una hasira, usifanye chochote.
 
Kama kuna mtu amekukosea na umepatwa na hasira usimjibu wakati una hasira hizo.
 
Kama kuna mtoto wake amekosea usimwadhibu ukiwa na hasira.
 
Ukiwa na hasira usifanye chochote, jipe muda wa kukaa mbali na kile kinachokupa hasira na akili zako zitarudi.

Thursday, January 17, 2019

EPUKA MABISHANO KWA KUFANYA HIVI.

Hakuna kitu kinachochukua muda wako na nguvu zako kama mabishano.

Mabishano ya aina yoyote ile ni gharama kwako na hakuna chochote unachonufaika nacho.

Na ipo njia rahisi sana ya kukuwezesha kuepuka kila aina ya mabishano.
 
Njia hiyo ni kukubaliana na watu waliojiandaa kubishana. Waambie wapo sahihi na kile wanachoamini na kusimamia ndiyo kweli. Hapo hawatakuwa tena na cha kubishana na wewe na kila mtu ataendelea na yake.
 
Lakini kama unataka ubishani uibuke, ambao hautaisha, mwambie mtu hayupo sahihi, mwambie amekosea na hapo utaibua ubishani usio na kikomo. Tena pale unapogusa kile ambacho mtu anaamini kweli, atatafuta kila njia ya kukitatua.
 
Kubaliana na watu haraka na endelea na mambo yako ambayo ni muhimu zaidi kuliko mabishano ambayo hayana manufaa yoyote kwako.
 
Kubaliana na watu na hawatakuwa na sababu ya kubishana na wewe. Na unapokubaliana nao haimaanishi kwamba wapo sahihi, ila hutaki kusumbuana nao. Ndani yako unaweza kujua kabisa kwamba hawapo sahihi, lakini huwaambii hilo maana ubishi utakaoanza hautakuwa na kikomo.

SHERIA YA ASILI: ( LAW OF NATURE )--UTAVUNA ULICHOPANDA.

Asili ina tabia ya kutoa hukumu yake hapo hapo, inatoa majibu mara moja.
Unapotenda dhambi, au kufanya kile ambacho wewe mwenyewe unajua siyo sahihi, utaanza kujisikia vibaya wewe mwenyewe. Na chochote utakachopata, hutaweza kukifurahia kama kitu ulichopata kwa uhalali.
Na zaidi ya hayo, asili lazima itakufanya ulipe kila unachofanya. Kanuni ya asili ni kulipa kila kinachofanywa, kwa kiwango kile kile.
Ukifanya wema, wema unarudi kwako kwa kiwango kile kile. Ukifanya uovu, uovu unarudi kwako kwa kiwango kile kile. Huwezi kutoroka hili, huwezi kuizidi asili akili.
Chagua kuishi kwa misingi sahihi, chagua kufanya kilicho sahihi mara zote, siyo kwa sababu unaogopa moto baadaye, bali kwa sababu unajua kila kitu kitalipwa sasa bila ya kuchelewa.

Wednesday, December 5, 2018

PATA MUDA WA KUKAA MWENYEWE KWENYE CHUMBA KWA UTULIVU. USIJIOGOPE WEWE MWENYEWE.

Mwanasayansi na hisabati Blaise Pascal aliwahi kusema matatizo yote ya binadamu yanatokana na mtu kushindwa kukaa mwenyewe kwenye chumba kwa utulivu.
 
Na hili ni sahihi kabisa, kinachowafanya watu wengi kuingia kwenye matatizo mbalimbali, ni kushindwa kutulia na mawazo yao, kukosa ujasiri wa kukaa na kutafakari chochote walichonacho kwenye mawazo yao.
 
Mimi nakwenda mbali na kusema kwamba watu wengi tunajiogopa sisi wenyewe. Ndiyo maana tukikutana na upweke tu tunakimbia haraka sana.
 
Kama unabisha jiangalie tu tabia yako, huwa unafanya nini pale unapojikuta upo mwenyewe. Lazima utatafuta kitu cha kuchukua muda wako na kushika mawazo yako. Labda utaanza kuchezea simu, utaanza kusoma kitu au hata kuwatafuta watu ambao hukuwa umepanga kuwatafuta.
 
Yote hayo ni kuepuka tu kuwa peke yako, upweke umekuwa hofu kubwa kwetu, hatutaki kabisa kukaa wenyewe, tukiwa tumeachwa na fikra zetu.
 
Rafiki, hebu acha kujiogopa, hebu rudisha urafiki kwako binafsi. Unapopata nafasi ya kuwa na upweke, itumie hiyo kuyatafakari maisha yako, itumie hiyo kujijengea taswira ya kule unakoenda.
 
Usijiogope na kukimbia kila unapojikuta mpweke, badala yake tumia nafasi hiyo kujenga urafiki na wewe binafsi na hata kujijua zaidi na kujua kwa kina kule unakokwenda.

Friday, November 30, 2018

JIWEKEE MUDA WA UKOMO KWA CHOCHOTE UNACHOPANGA KUFANYA.

Mtu mmoja amewahi kusema kwamba jukumu huwa linachukua muda uliopangwa lifanyike. Akimaanisha kama kuna jukumu ambalo linapaswa kufanywa kwa masaa mawili, litakamilika ndani ya masaa mawili. Jukumu hilo hilo likipangwa kufanyika ndani ya masaa matano, litachukua masaa matano.
Huwa tunasukumwa kufanya zaidi pale ambapo muda unakuwa mdogo, na tunaahirisha mambo pale muda unapokuwa mwingi. Ndivyo maana wanafunzi ni vigumu sana kusoma siku za kawaida, lakini mtihani unapokaribia, hamasa ya kusoma inakuwa juu.
Jiwekee muda wa ukomo kwa chochote unachopanga kufanya, na muda huo uwe mfupi kuliko muda uliozoeleka. Kwa kuwa na muda huu na kuufuata, utaweza kujisukuma kufanya zaidi. Kadiri unavyokuwa na muda mfupi wa kutekeleza jambo, ndivyo mawazo ya kuahirisha yanavyopotea kwenye akili yako. Waahidi watu kwamba jukumu litakamilika mapema kuliko kawaida, na tekeleza hilo uliloahidi.

KUWA NA MAMBO YAKO MATANO KWA SIKU AMBAYO UTAYATEKELEZA.

Kila siku unayoianza, ainisha mambo matano muhimu ambayo ukiyafanya siku hiyo yatakusogeza karibu na mafanikio unayotaka kuyafikia. Mambo hayo matano unapaswa kuyafanyia kazi bila ya kujali mazingira yapoje. Inyeshe mvua au liwake jua, hayo matano ni muhimu kwa siku yako na unapaswa kuyafanyia kazi.
Kwa kuwa na tano za siku, unajiweka kwenye nafasi ya kutekeleza yale muhimu na kuepuka kupotezwa na kelele ambazo zimekuzunguka kila mahali.

TUMEZOEA KUSIMAMIWA : KUWA NA MTU WA KUKUSIMAMIA.

Sisi binadamu ni wabaya sana kwenye kujisimamia wenyewe, huwa tunajionea sana huruma na ni rahisi sana kujidanganya. Unaweza kuwa na orodha yako ya siku, umepanga mambo yako matano muhimu na hata kujiwekea ukomo. Lakini katikati ya siku yako ukawa hujisikii kuendelea na yale uliyopanga, ni rahisi kujihalalishia kwamba labda umechoka au ni kitu hakiwezekani.
Lakini unapokuwa na mtu wa pembeni, mtu ambaye jukumu lake ni kuhakikisha umekamilisha uliyopanga na hapokei sababu bali matokeo, utalazimika kufanya kile ulichopanga kufanya.
Tafuta mtu wa karibu kwako, ambaye hakuonei huruma kisha mtake akusimamie kwa karibu ili utimize unachotaka. Kama huwezi kupata mtu wa karibu basi kuwa na kocha au menta ambaye atakusimamia kwa karibu.

JIAMBIE HIVI " NAFANYA SASA , MUDA HUU ".

Kuna wakati unakuwa umeshapanga kabisa nini utafanya na kwa wakati gani. Lakini inapofika muda wa kufanya, mawazo ya kuahirisha yanaanza kukuingia. Unaanza kuona labda hujawa tayari au ni bora kusubiri.
Ni katika wakati kama  huu ndiyo unapaswa kujiambia kauli hii, NAFANYA SASA HIVI, rudia kauli hiyo mara nyingi uwezavyo na utajikuta umeanza kufanya. Kila unapofikiria kuahirisha kufanya kitu, jiambie kauli hiyo kwamba unafanya. Kila unapoanza kujiambia kwambe umechoka, anza kujiambia kauli hiyo.
Kwa kurudia rudia kujiambia kauli hiyo, unaanza kuiamini na kujiamini wewe mwenyewe na kuanza kufanya.

Tuesday, October 16, 2018

WAZAZI HUKWAMISHA AU KUENDELEZA VIPAJI VYA WATOTO WAO.

9 Oktoba 2018
Mzazi ana nafasi kubwa sana katika kuendeleza kipaji cha mtoto

Kipaji ni uwezo wa kuzaliwa nao wa kufanya jambo fulani kwa ngazi ya juu bila kufundishwa au baada ya kufundishwa kidogo tu. Kipaji kinaweza kuwa cha kimwili au cha kiakili lakini pia kinaweza kuendelezwa au kudumazwa.
Mzazi ni mtu wa kwanza anayeweza kutambua uwezo ama kipaji cha mtoto wake. Hata hivyo ana fursa ya kuendeleza au kutokukiendeleza kipaji cha mtoto.

Baadhi ya wazazi hutambua vipaji vya watoto mapema na kuanza kuviendeleza kwa kuwapatia nyenzo mbali mbali ambazo huwasaidia katika kuboresha uwezo walio nao.

Lakini pia wapo wazazi ambao wanamalengo yao juu ya ni kitu gani wanapenda watoto wao wafanye. Ama yamkini hawana ufahamu wa nini cha kufanya ili kumwendeleza mtoto mwenye kipaji .Hata hivyo vipo baadhi ya vipaji ambavyo wazazi huona ni upotevu tu wa maadili mfano kuimba na kucheza mziki.

BBC imezungumza na mama Ritha, mama mwenye watoto wanne. Anasema kwa kiasi kikubwa baadhi ya wazazi na hata yeye mwenyewe kipindi cha nyuma walikwamisha sana watoto sababu walikuwa hawatambui kama kipaji pia ni njia salama ya kumwezesha mtoto kimaisha.
"Wazazi wengi huwa hawajuagi tena zamani tulikuwa tunaona watoto wanapotea kabisa. Mi binti yangu wa kike alikua anapenda kuandika nyimbo za wasanii wa marekani na hata za kwake mwenyewe kwenye daftari lake afu kukiwa na sherehe yeye ndo mwimbaji. Nikaona anapotea nlikua na mchapa na nlimwambia akifika chuo kikuu ndo afanye uo mziki lakini si nyumbani kwangu maana hata baba yake alikuwa hapendi kabisa," Mama Ritha anaiambia BBC
Hata hivyo ameongeza kuwa wazazi pia huwanyima fursa za kujifunza watoto kwani kila akishika kitu mzazi hupiga kelele mtoto aache kwa madai kwamba ataumia.
Hata hivyo wapo baadhi ya watoto ambao wamepewa msaada mkubwa na wazazi wao katika kuboresha na kuendeleza vipaji vyao.

BBC imezungumza na mwanadada mpambaji Plaxeder Jumanne au baby precious kama anavyojulikana katika kazi zake za upambaji, anasema mama yake ndio mtu wa kwanza kumshauri ageuze kipaji chake kuwa biashara huku akimnunulia vifaa orijino vya urembo.

"Mie nlikuwa nawachukua watoto wenzangu nawapamba nlikua napenda sana urembo kama mama yangu. Hata nilipo kuwa nikaanza kuwapamba watu. Nilikuwa natumia vifaa feki hivi vya bei rahisi lakini mama yangu alianza kwa kuninunulia vifaa orijino kabisa. Na huwezi amini nilikua nampamba yeye na kumfuta kabla sijapata wateja tena nimejifunza kufunga maremba ya kinaijeria kichwani kwa mama na alikuwa ananisaidia sana, sasa hivi nasafiri hadi mikoani na kupamba watu mbali mbali hadi watu maarufu na nimepata pesa nikanunua vifaa vingi sana Orijino," Plaxeda anaiambia BBC.

Hata hivyo manadada huyo anasema kwa sasa mama yake ametangulia mbele za haki tangu mwaka jana ila bado anamshukuru kwa sababu hivi sasa kazi ya upambaji inampa pesa kuliko ajira yake na imemwezesha kufungua biashara zingine.

"Mimi sijajitangaza sana ila kupitia vifaa alivyonianzishia navyo mama yangu nikawa napamba hadi maharusi na wasimamizi wao. Na kipaji hiki kimenipa pesa ninafanya biashara ya kutengeneza nywele hasa mawigi na pia kufungua biashara ya nguo. Mama yangu angekuwepo angefurahi sana ila naamini anaona. Nimewaremba baadhi ya wasanii wa Tanzania. Safari ndo inaanza," Plaxeder anaiambia BBC.


Mwanaharakati wa masuala mbali mbali ya kibinadamu Shahista Alidina maarufu kama Shaykaa, anasema baadhi ya wazazi hupenda kutimiza ndoto zao kupitia watoto na mwishowe huwakwamisha.

"Unakuta mzazi kama alishindwa kuwa mwanasheria au daktari kama alivyotaka huko nyuma atataka mtoto wake afuate ndoto hiyo. Hawataki kuwapa uhuru watoto wafuate wanavyopenda. Unakuta kipaji cha mtoto kinaweza mletea kipato cha kutosha tu ila mzazi anampa mtoto shinikizo la kufaulu tu shule awe namba moja, mbili au tatu na ndiomaana unaona watoto wengine hadi wanajiua. Wanawanyima fursa watoto kufanya vitu wanavyovipenda," Shaykaa anaiambia BBC.

Hata hivyo anaongeza kuwa kunachangamoto nyingine kwa wazazi kupangia kazi watoto kuwa hii ni ya wanawake au hii ni ya wanaumena kujenga uoga kwa watoto na kuwanyima fursa ya kujituma zaidi.

"Kusoma kwa mtoto ni muhimu ila kuna muda wa ziada na kuna maisha nje ya darasa. Unakuta mtoto wa kike anapenda kucheza mpira, lakini mzazi atapinga kuwa huu ni mchezo wa wanaume mwanamke hatakiwi, sasa hapo moja kwa moja mzazi atakuwa ameua kabisa kipaji cha mtoto kama mtoto atakosa fursa ya kujiendeleza huko mbele," anasema Shaykaa
Mwanaharakati huyo pia amewaasa wazazi kuhakikisha wanawasaidia watoto kujiendeleza kijamii.

"Mtoto ni muhimu awe na maisha yake pia, na tutambue kuwa na wao ni binadamu wala si wafungwa. Ni muhimu ndio kufuata dini na misingi bora ya maisha pamoja na mila na desturi lakini tusisahau kuwa mtoto anapofikia umri wa kujielewa anahaki ya kufanya maamuzi kuwa anapenda nini ilimradi ni jambo jema kisheria, kidini, kiafya na kijamii. Tuwe marafiki kwao lakini tusiwapotoshe watoto wetu, Shaykaa anaiambia BBC.

JE, TUWAPE WATOTO WETU SIMU ZETU ZA MKONONI WACHEZEE ??

14 Oktoba 2018, BBC  SWAHILI

  Simu yaweza kumsaidia mtoto kujifunza lakini bado nimuhimu kwa mzazi kuwa makini
Hivi karibuni imekuwa kawaida sana kumkuta mtoto anatumia simu ya mkononi ya mzazi wake na mara nyingine wanatumia bila hata kupata ridhaa ya mzazi mwenyewe.
Baadhi ya watoto huonyesha utaalamu wa hali ya juu katika kufungua kurasa mbalimbali za simu hizo.

Na inadaiwa kuwa kuna watoto ambao huwa wanajifunza mambo mengi kupitia simu za mkononi.
Hata hivyo si wazazi wote ambao hukubali simu zao zitumiwe na watoto, baadhi huwa wakali na kuweka kila aina ya nywila ingawa wengine huwa hawaoni shida kuwapatia watoto wao simu punde tu wanaporejea kutoka kwenye majukumu yao ya kila siku.

Baadhi ya wazazi huwa wanaona kuwa simu ndio njia pekee inayoweza kuwafanya watoto wao watulie na wao wapate muda wa kupumzika ama hata kufanya shughuli zao za nyumbani. 

Je,kuna faida yeyote endapo mtoto atatumia simu?
BBC imezungumza na baadhi ya wazazi ili kufahamu ni kwa kiasi gani watoto wao hutumia simu zao na wanawadhibiti vipi vitu anavyoangalia mtoto?

"Kwa kweli simu yangu hata sina uhuru nayo huwa nikifika tu nyumbani wanangu huwa wananipokea kwa mbwembwe zote na cha kwanza kubeba ni simu na nikihitaji lazima niwaombe wao.
Simu ikiita utakuta wao ndio wanapokea,mara nyingi wanaangalia video za kartoon au za watoto wenzao zilizopo you tube," Mama Brian anaeleza

Baadhi ya watoto hutambua hadi nywila za simu za wazazi wao
Alex Kayetta ambaye ni baba wa mtoto mmoja, anasema simu yake huwa haimiliki punde tu anapofika nyumbani ,
"Mwanangu akishashika simu yangu yani kuipata lazima nimbembeleze, na akichukua mara nyingine huwa lazima nimtafute alipo ,kuna siku nilimkuta amejificha ndani ya beseni akicheza michezo ya kwenye simu'game' nikampiga picha".

Freddie Kyara ni mwanasaikolojia kutoka nchini Tanzania ambaye anaeleza kuwa hali hii huwa inafanana na jinsi mzazi anapokua kwenye simu muda mrefu na hupoteza fursa ya kuwa karibu jamii na ndivyo hivyo inavyotokea kwa mtoto.

Na kwa upande wa mtoto kutumia simu huwa kuna madhara pia "Kukua kwa mtoto kunahitaji awe na mbinu za kijamii, kama vile kucheza na watoto wenzake na kujifunza mambo mbalimbali kutoka kwa wenzake, lakini siku hizi unaweza kukuta mtoto anashindwa kucheza na watoto wengine kwa sababu amezoea yeye rafiki yake ni simu tu.

Ubunifu wa mtoto unaweza kupungua. Sisi wakati tunakuwa hatukuwa tunajua habari za simu, ilikuwa ni kucheza mpira na kujishughulisha na shughuli mbalimbali za nyumbani na hali hiyo ilitufanya tuweze kujenga urafiki na watu na kujua tabia za watu tofautitofauti. 

Mtoto anaweza kujifunza pia kwenye simu lakini lazima uthibiti uwepo kwa sababu sio kila kilichopo kwenye simu kina maudhui mazuri kwa watoto na wanapaswa kutengewa muda" Kyara ,mtaalamu wa saikolojia alieleza.

Hata hivyo jumbe mbalimbali zimekuwa zikisambaa kuonya madhara ya mionzi ya simu kwa watoto wadogo na kudai kuwa umri sahihi wa kupewa simu ni kuanzia miaka kumi na sita.
Jambo ambalo Daktari Fredrick Mashili anasema madhara ya namna hiyo huwa inategemeana zaidi na umri wa mtoto japo kwa upande mwingine macho yanaweza kupata shida ingawa hakuna ushahidi wa kutosha kuthibitisha madhara hayo ya mionzi.

"Kuna wasiwasi kwamba mtu akianza kutumia simu mapema anaongeza muda wa kuyashughulisha macho yake katika mionzi kwa muda mrefu zaidi kitu ambacho si kizuri kwa afya ya macho," Dkt.Mashili alieleza.


Friday, October 12, 2018

KILA MTU ANA NAMBA NA VIWANGO VYAKE KIFEDHA. HATUWEZI KULINGANA.

Linapokuja swala la fedha, kila mtu ana namba na viwango vyake. Kwa sababu tunatofautiana ndoto, kazi/biashara, kipato, mitindo ya maisha na hata mazingira, matokeo yetu ya kifedha hayawezi kulingana.

Hivyo kujipima hatua ulizopiga kifedha kwa kuwatumia wengine ni kujiumiza na hata kujirudisha nyuma, kwa sababu kuna namba nyingi ambazo utakuwa huzijui kuhusu wengine. Kwa mfano unaweza kumwona mtu kwa nje anaonekana kuwa na vitu vinavyoashiria ana fedha nyingi, lakini kumbe vitu vyote hivyo amepata kwa mkopo ambao ataulipa maisha yake yote.
Pia unaweza kumwona mtu ukafikiri hayupo vizuri kifedha kwa mwonekano wake wa nje, kumbe anafanya uwekezaji ambao baadaye utamwezesha kufikia uhuru wa kifedha.

Kwa kuwa ni vigumu kupima hatua ulizopiga kifedha kwa kuwatumia watu wengine, unahitaji kujitumia wewe mwenyewe.

UTOAJI WA FEDHA KWA WENGINE BILA KUTEGEMEA KUPATA CHOCHOTE NI MUHIMU SANA.

Kiasi cha fedha unachotoa kwa wengine bila ya kutegemea kupata chochote ni kiwango kingine muhimu sana cha kupima afya yako kifedha na kujua hatua ulizopiga. Kwa kadiri unavyotoa zaidi ndivyo unavyoonesha kwamba unaitumia fedha na siyo fedha inakutumia wewe.

Unahitaji kuwa na utaratibu wa kutoa fedha kuwasaidia wengine bila ya kutegemea kulipwa fedha hizo. Kwa sababu tunatoshelezwa zaidi na utoaji kuliko upokeaji.

Pia unapotoa fedha kwa wengine, unatengeneza pengo ambalo itabidi lizibwe, hivyo unakuwa umejiweka kwenye nafasi ya kuongeza kipato chako zaidi.

WEKA AKIBA ILI USIINGIE KWENYE MADENI MABAYA NA CHANGAMOTO ZA MAISHA.


Hichi ni kiwango kinachoonesha maandalizi yako uliyonayo sasa kwa upande wa fedha. Kadiri unavyokuwa na akiba kubwa kifedha, ndivyo unavyoweza kujilinda na dharura mbalimbali zinazoweza kukutokea. Akiba unayokuwa nayo ndiyo itakukinga usiingie kwenye madeni mabaya pale unapokutana na changamoto ambazo hukuzitegemea.

Kiwango sahihi cha akiba unayopaswa kuwa nayo ni ile inayoweza kutosheleza kuendesha maisha yako kwa miezi 6 mpaka mwaka mmoja hata kama utakuwa huna kipato kabisa katika kipindi hicho.

Kuza kiwango chako cha akiba na hili litakupa pumziko na kukuondolea wasiwasi kuhusu fedha kitu ambacho kitakuwezesha kufanya mambo yako kwa utulivu na ufanisi mkubwa.

EPUKA MADENI ILI KUEPUKA KUJIWEKA KWENYE WAKATI MGUMU KIFEDHA.

Kiasi cha fedha unachodaiwa na wengine kutokana na vitu ulivyonunua bila ya kuwa na fedha ni kipimo cha maamuzi yako ya kifedha kwa siku za nyuma. Kadiri madeni yako yanavyokuwa makubwa, ndivyo sehemu kubwa ya kipato chako inavyoelekea kwenye kulipa madeni hayo na wewe kubaki na kiasi kidogo ambacho hakiwezi kukutosheleza.

Unahitaji kutokuwa na deni binafsi kabisa, na madeni mazuri unayopaswa kuwa nayo ni yale yanayojilipa yenyewe. Madeni yanayojilipa yenyewe ni yale ambayo yanazalisha faida na faida hiyo unatumia kulipa deni. Haya ni madeni ambayo hayakuumizi.

Lakini madeni ambayo unalipa kwa fedha zako unazopata kwenye shughuli zako binafsi, ni utumwa ambao utakutesa kwa muda mrefu. Kama upo kwenye madeni ya aina hii kazana kuondoka na usiingie tena ili kuepuka kujiweka kwenye wakati mgumu kifedha.

WEKEZA SASA KWA AJILI YA BAADAYE , WAKATI UNA NGUVU ZA KUFANYA KAZI.

Kiwango ambacho umekiwekeza kwenye maeneo ambayo yanazalisha riba au faida ni kipimo muhimu kwa maandalizi yako ya kifedha ya baadaye. Kama hapo ulipo hujafanya uwekezaji wote kwa ajili ya baadaye, kama hujawa na maandalizi ya kukuwezesha kuingiza kipato bila ya wewe kufanya kazi moja kwa moja, huna maandalizi ya kifedha ya baadaye, na haupo eneo zuri kifedha.

Unahitaji kufanya uwekezaji kwa ajili ya baadaye, kwa sababu utakuja wakati ambapo huna uwezo wa kufanya kazi kama unavyofanya sasa, lakini una mahitaji muhimu kwa maisha yako. Unapokuwa umewekeza na uwekezaji unazalisha, maisha yako yanakwenda vizuri.

Kiwango sahihi cha uwekezaji unachopaswa kuwa nacho ni kile ambacho kinazalisha faida au riba ambayo inakuwezesha wewe kuendesha maisha yako kwa kadiri ya mahitaji yako.

Wednesday, October 10, 2018

TATIZO NI TAFSIRI YA MATUKIO YANAYOTUTOKEA.

Watu wawili wanaweza kushindwa kwenye kitu kimoja, mmoja akachukulia kushindwa huko kama kichocheo cha kufanya zaidi na akafanikiwa. Mwingine anaweza kuchukulia kushindwa huko kama sababu ya kukata tamaa na kushindwa kabisa.

Tukio ni moja, tafsiri tofauti na matokeo tofauti kabisa.
Siyo kinachotokea, bali namna unavyotafsiri kinachotokea ndiyo inaleta madhara kwako.
Kwenye Falsafa ya Ustoa pia kuna dhana inayoitwa upili wa udhibiti. Dhana hii inaeleza kwamba vitu vyote vinavyotokea kwenye maisha yako, vinagawanyika katika makundi mawili, kundi la kwanza ni vitu unavyoweza kuviathiri, hivi vipo ndani ya uwezo wako. Kundi la pili ni vitu usivyoweza kuviathiri, hivi vipo nje ya uwezo wako.

Hivyo unapokutana na chochote na ukajiambia ni kigumu au kinakushinda, huna haja ya kusumbuka, badala yake jiulize je kipo ndani ya uwezo wako au nje ya uwezo wako. Kama kipo ndani ya uwezo wako chukua hatua sahihi, kama kipo nje ya uwezo wako kikubali kama kilivyo au kipuuze. Hakuna namna bora ya kuendesha maisha yako kama hii, kwa sababu hakuna chochote kitakachotokea, ambacho kitakuvuruga kabisa.

Ndugu  yangu , nikukumbushe tena ya kwamba kama unataka kuitawala dunia, kuna mtu mmoja unayepaswa kumtawala, na mtu huyo ni wewe mwenyewe. Hutaweza kujitawala wewe mwenyewe kwa mabavu au nguvu, badala yake utajitawala kwa kudhibiti mawazo yako na hisia zako.

Monday, October 8, 2018

TENGENEZA NJIA , USIFUATE NJIA

”Do not go where the path may lead, go instead where there is no path and leave a trail.” – Ralph Waldo Emerson

Watu wengi wamekuwa wanashindwa kwenye maisha kwa sababu hawathubutu kufanya vitu vipya, badala yake wanaangalia kile ambacho tayari kimeshafanya na wao wanafanya. Hii ni kufuata njia, sasa unapochagua kufuata njia fulani, jua utafika kule ambapo njia hiyo imeelekea. Kama utafanya kile ambacho wengine wanafanya, utapata matokeo ambayo wanayapata.

Njia pekee ya kufanikiwa zaidi, ni kufanya mambo mapya, kufanya yale ambayo hakuna mwingine anayefanya, kutengeneza njia mpya, pale ambapo hakuna njia. Hili linatisha, kwa sababu unakuwa huna uhakika, nafasi ya kushindwa ni kubwa, lakini pia nafasi ya kufanikiwa ni kubwa zaidi.
Kwenye chochote unachochagua kufanya, acha kuangalia wengine wanafanya nini ili uige, badala yake angalia kipi muhimu kinachopaswa kufanya kisha kifanye kwa njia ambayo ni sahihi kwako kufanya na kwa wale unaowahudumia. Kwa namna hii utatengeneza njia mpya na wewe kama kiongozi wa njia hiyo utanufaika zaidi.
Rafiki, sindano za leo zimekuwa ndefu na kali, lakini kama utazifanyia kazi, hutabaki hapo ulipo. Sina kingine cha kuongeza zaidi ya kukukumbusha kanuni yetu muhimu ambayo ni MAARIFA SAHIHI + KUCHUKUA HATUA KUBWA = MAFANIKIO MAKUBWA. Maarifa ni hayo, kazi kwako kuchukua hatua ili ufanikiwe.

Friday, September 21, 2018

JE, WAIJUA AKAUNTI YA FEDHA YA SAIKOLOJIA ?

Unahitaji kujizoesha kifikra na kisaikolojia kuwa na fedha nyingi, hata kama bado hujazishika kwenye mikono yako au kuwa nazo kwenye akaunti yako ya benki. Na unaweza kuanza kwa kufikiria mara kumi ya kipato unachopata sasa, kisha kufikiria kipato hicho mara kwa mara, kukiwekea mipango na kuweka lengo lako la kipato liwe ni kukua kufikia mara kumi ya kipato chako cha sasa. Kwa njia hii utaongeza kiwango chako cha fedha kisaikolojia.

 Watu wengi wanajua aina moja ya akaunti ya kifedha, ambayo ni akaunti ya benki, au akiba na uwekezaji ambao wamekuwa wamefanya. Hivyo ukitaka kuangalia utajiri wa mtu, unaangalia ni kiasi gani cha fedha anacho kwenye akaunti zake za benki na uwekezaji kiasi gani amefanya.

 Aina ya pili ya akaunti ya kifedha, ukiacha akaunti ya benki, ni akaunti ya fedha ya kisaikolojia. Kila mmoja wetu, ana kiwango chake cha kifedha kwenye fikra zake, ambacho ndiyo ameshajiambia anapaswa kupata kiwango hicho. Yaani kila mmoja wetu, kuna kiwango chake cha fedha, ambacho ameshakiweka kwenye fikra na mawazo yake, na akishapata kiwango hicho basi akili yake inatulia na hakazani tena kupata fedha zaidi.

Waangalie watu wote ambao wamepata fedha nyingi kwa mkupuo, kiasi kikubwa cha fedha ambacho hawajawahi kukishika kwenye maisha yao. Waangalie watu ambao wameshinda bahati nasibu, waangalie watu ambao wamerithi mali, waangalie watu ambao wamepokea mafao. Wengi haiwachukui muda wanakuwa wameshapoteza fedha nyingi walizopata na kurudi kwenye maisha yao ya kawaida.
Wanakuwa wamepata fedha nyingi kwenye akaunti ya benki, lakini akaunti yao ya kisaikolojia inasoma kiwango cha chini. Hivyo wanaacha kufikiria kabisa kuhusu fedha, wanaanza kupoteza fedha, mpaka zinapofika kwenye kile kiwango chao cha kisaikolojia ndiyo wanastuka na kuanza kufikiria kuhusu fedha.

 Pia unaweza kufikiria mara 100, mara 1000 na hata zaidi ya kipato unachopata sasa. Fikra zote hizo zitaiandaa akili yako kupokea fedha zaidi na kuweza kutulia na fedha zaidi unazopata. Unapofikiria mara elfu moja ya kipato unachopata sasa, ongezeko kidogo halitakusumbua kama linavyokusumbua sasa.


Na  Mwl  Japhet  Masatu , Dar  es  salaam , Tanzania,  Afrika Ya  Mashariki ---Mwl  wa  Maisha Na  Mafanikio, Mshauri, Public Speaker(MC), Mwandishi, Mjasiriamali /
Tuwasiliane kwa :+ 255 755 400 128 / + 255 716 924136(WhatsApp ).  EMAIL: japhetmasatu@gmail.com