Wednesday, October 10, 2018

TATIZO NI TAFSIRI YA MATUKIO YANAYOTUTOKEA.

Watu wawili wanaweza kushindwa kwenye kitu kimoja, mmoja akachukulia kushindwa huko kama kichocheo cha kufanya zaidi na akafanikiwa. Mwingine anaweza kuchukulia kushindwa huko kama sababu ya kukata tamaa na kushindwa kabisa.

Tukio ni moja, tafsiri tofauti na matokeo tofauti kabisa.
Siyo kinachotokea, bali namna unavyotafsiri kinachotokea ndiyo inaleta madhara kwako.
Kwenye Falsafa ya Ustoa pia kuna dhana inayoitwa upili wa udhibiti. Dhana hii inaeleza kwamba vitu vyote vinavyotokea kwenye maisha yako, vinagawanyika katika makundi mawili, kundi la kwanza ni vitu unavyoweza kuviathiri, hivi vipo ndani ya uwezo wako. Kundi la pili ni vitu usivyoweza kuviathiri, hivi vipo nje ya uwezo wako.

Hivyo unapokutana na chochote na ukajiambia ni kigumu au kinakushinda, huna haja ya kusumbuka, badala yake jiulize je kipo ndani ya uwezo wako au nje ya uwezo wako. Kama kipo ndani ya uwezo wako chukua hatua sahihi, kama kipo nje ya uwezo wako kikubali kama kilivyo au kipuuze. Hakuna namna bora ya kuendesha maisha yako kama hii, kwa sababu hakuna chochote kitakachotokea, ambacho kitakuvuruga kabisa.

Ndugu  yangu , nikukumbushe tena ya kwamba kama unataka kuitawala dunia, kuna mtu mmoja unayepaswa kumtawala, na mtu huyo ni wewe mwenyewe. Hutaweza kujitawala wewe mwenyewe kwa mabavu au nguvu, badala yake utajitawala kwa kudhibiti mawazo yako na hisia zako.

1 comment:

  1. Kama unataka kuitawala dunia nzima, kama unataka dunia isikupe shida kwa chochote kile kinachotokea, basi unahitaji kumtawala mtu mmoja pekee hapa duniani.

    Mtu huyo ni wewe mwenyewe, nafsi yako ambayo ndiyo inatengeneza dunia unayoiona wewe.

    ReplyDelete