14 Oktoba 2018, BBC SWAHILI
Hivi karibuni
imekuwa kawaida sana kumkuta mtoto anatumia simu ya mkononi ya mzazi
wake na mara nyingine wanatumia bila hata kupata ridhaa ya mzazi
mwenyewe.
Baadhi ya watoto huonyesha utaalamu wa hali ya juu katika kufungua kurasa mbalimbali za simu hizo.Na inadaiwa kuwa kuna watoto ambao huwa wanajifunza mambo mengi kupitia simu za mkononi.
Hata hivyo si wazazi wote ambao hukubali simu zao zitumiwe na watoto, baadhi huwa wakali na kuweka kila aina ya nywila ingawa wengine huwa hawaoni shida kuwapatia watoto wao simu punde tu wanaporejea kutoka kwenye majukumu yao ya kila siku.
Baadhi ya wazazi huwa wanaona kuwa simu ndio njia pekee inayoweza kuwafanya watoto wao watulie na wao wapate muda wa kupumzika ama hata kufanya shughuli zao za nyumbani.
Je,kuna faida yeyote endapo mtoto atatumia simu?
BBC imezungumza na baadhi ya wazazi ili kufahamu ni kwa kiasi gani watoto wao hutumia simu zao na wanawadhibiti vipi vitu anavyoangalia mtoto?
"Kwa kweli simu yangu hata sina uhuru nayo huwa nikifika tu nyumbani wanangu huwa wananipokea kwa mbwembwe zote na cha kwanza kubeba ni simu na nikihitaji lazima niwaombe wao.
Simu ikiita utakuta wao ndio wanapokea,mara nyingi wanaangalia video za kartoon au za watoto wenzao zilizopo you tube," Mama Brian anaeleza
Alex Kayetta ambaye ni baba wa mtoto mmoja, anasema simu yake huwa haimiliki punde tu anapofika nyumbani ,
"Mwanangu akishashika simu yangu yani kuipata lazima nimbembeleze, na akichukua mara nyingine huwa lazima nimtafute alipo ,kuna siku nilimkuta amejificha ndani ya beseni akicheza michezo ya kwenye simu'game' nikampiga picha".
Freddie Kyara ni mwanasaikolojia kutoka nchini Tanzania ambaye anaeleza kuwa hali hii huwa inafanana na jinsi mzazi anapokua kwenye simu muda mrefu na hupoteza fursa ya kuwa karibu jamii na ndivyo hivyo inavyotokea kwa mtoto.
Na kwa upande wa mtoto kutumia simu huwa kuna madhara pia "Kukua kwa mtoto kunahitaji awe na mbinu za kijamii, kama vile kucheza na watoto wenzake na kujifunza mambo mbalimbali kutoka kwa wenzake, lakini siku hizi unaweza kukuta mtoto anashindwa kucheza na watoto wengine kwa sababu amezoea yeye rafiki yake ni simu tu.
Ubunifu wa mtoto unaweza kupungua. Sisi wakati tunakuwa hatukuwa tunajua habari za simu, ilikuwa ni kucheza mpira na kujishughulisha na shughuli mbalimbali za nyumbani na hali hiyo ilitufanya tuweze kujenga urafiki na watu na kujua tabia za watu tofautitofauti.
Mtoto anaweza kujifunza pia kwenye simu lakini lazima uthibiti uwepo kwa sababu sio kila kilichopo kwenye simu kina maudhui mazuri kwa watoto na wanapaswa kutengewa muda" Kyara ,mtaalamu wa saikolojia alieleza.
Hata hivyo jumbe mbalimbali zimekuwa zikisambaa kuonya madhara ya mionzi ya simu kwa watoto wadogo na kudai kuwa umri sahihi wa kupewa simu ni kuanzia miaka kumi na sita.
Jambo ambalo Daktari Fredrick Mashili anasema madhara ya namna hiyo huwa inategemeana zaidi na umri wa mtoto japo kwa upande mwingine macho yanaweza kupata shida ingawa hakuna ushahidi wa kutosha kuthibitisha madhara hayo ya mionzi.
"Kuna wasiwasi kwamba mtu akianza kutumia simu mapema anaongeza muda wa kuyashughulisha macho yake katika mionzi kwa muda mrefu zaidi kitu ambacho si kizuri kwa afya ya macho," Dkt.Mashili alieleza.
No comments:
Post a Comment