Showing posts with label SHERIA NA JAMII. Show all posts
Showing posts with label SHERIA NA JAMII. Show all posts

Wednesday, April 27, 2016

ZIJUE AINA 7 ZA ADHABU ZINAZOTOLEWA NA KORTI



1. ADHABU  YA  KIFO (DEATH PENALTY)
Adhabu hii hutolewa kwa wenye makosa makubwa kama kuua kwa kukusudia (murder). Kifungu  cha  26  Kanuni za Adhabu kinasema kuwa mtu atakapohukumiwa adhabu ya kifo basi adhabu hiyo itatekelezwa kwa kunyongwa kwa kitanzi mpaka mtu huyo atakapokufa.
Baadhi ya nchi adhabu ya kifo hutekelezwa kwa kupigwa risasi na nyingine kudungwa sindano ya sumu. Sisi kwetu ni kitanzi/kamba shingoni kwa kuning’inizwa mpaka roho itoke. Pamoja na hayo, adhabu hii inapingwa sana na mashirika ya haki za binadamu pamoja na wanaharakati wengine duniani kote.
 
2. ADHABU YA  KIFUNGO (IMPRISONMENT)
Adhabu ya kifungo hutolewa kwa muda tofauti kutegemea na aina ya kosa alilotenda mtu. Yapo makosa watu hufungwa miaka saba, mwaka mmoja, miezi, mpaka thelathini lakini pia kipo kifungo cha maisha. 
Kifungo kimegawanyika mara mbili. Kipo kifungo cha ndani na kipo cha nje. Kifungo cha ndani ni kifungo ambacho mtu anakuwa ndani ya uzio maalum ambao haruhusiwi kutoka huku ukihudumiwa na askari magereza. Hii huitwa jela (jail). Hataruhusiwa kutoka humo mpaka muda maalum utakapoisha. 
Aidha, kifungu cha nje wakati mwingine huitwa kifungo cha masharti. Ni kifungo ambacho mtuhumiwa hazuiliwi katika jela isipokuwa atapewa masharti kadhaa atakayotakiwa kutekeleza akiwa nje ya jela. Anaweza kuwa anaishi nyumbani kwake lakini kwa sharti la kuripoti sehemu fulani kila siku au vinginevyo, anaweza kuzuiwa kusafiri nje ya mkoa wilaya au vinginevyo, anaweza kupewa sharti la kutotenda kosa ndani ya mwaka, miaka au vinginevyo n.k. Kubwa hapa ni kuwa kifungo hiki mtu anakuwa nje lakini kwa masharti maalum.
 
3. ADHABU  YA  KUCHAPWA  VIBOKO (CORPORAL  PUNISHMENT)
Hakimu au jaji anaweza, kwa mamlaka aliyonayo, kuamuru mtuhumiwa kuchapwa bakora. Adhabu hii inaweza kutolewa ikiwa kama adhabu inayojitegemea au kama nyongeza baada ya adhabu nyingine.
Maana yake ni kuwa unaweza kuhukumiwa kifungo na viboko au viboko pekee na uachiwe huru.
 
4. ADHABU YA FAINI (FINE)
Hii nayo inaweza kuwa adhabu inayojitegemea au inayotumika kama adhabu ya nyongeza baada ya kuwa imetolewa adhabu nyingine. Faini huhusisha malipo ya fedha ambayo yatalipwa kwa utaratibu maalum utakaowekwa na Mahakama. 
 
5. ADHABU YA KUNYANG’ANYWA  MALI (FORFEITURE)
Mahakama inaweza kuamuru mali ya mtuhumiwa kunyang’anywa baada ya kupatikana na hatia. Mali kunyang’anywa ni sehemu ya adhabu. Mara nyingi mali zinazonyang’anywa ni zile zilizotumika katika uhalifu. Gari au pikipiki kutumika katika wizi ambao umethibitishwa inaweza kunyang’anywa. Hii ni pamoja na mali nyingine kama nyumba, meli, n.k.
 
6. ADHABU YA KULIPA FIDIA (COMPENSATION
Fidia ni tofauti na faini. Fidia ni kulipia kile ulichoharibu, kupoteza au hasara uliyosababisha.
Fidia ni mpaka kiwepo kitu kilichosababisha hasara, upotevu, au uharibifu. Pesa inayolipwa kufidia hasara, uharibifu ndiyo inayoitwa fidia. Aidha, faini hulipwa bila kuhitaji kuwepo kitu kilichoharibika au kusababishiwa hasara.
 
7. ADHABU  YA  KUTUNZA  AMANI  NA  KUWA NA  TABIA NJEMA (PEACE  KEEPING & BE OF GOOD  BEHAVIOUR)
Mara nyingi adhabu hii hutolewa kwa wenye makosa madogo madogo. Hatutarajii mtu aibe, aue au abake halafu adhabu yake iwe kuhakikisha anatunza amani na kuwa na tabia njema mtaani.
Ifahamike kuwa adhabu hii hutekelezwa mtu akiwa nje.  Ni sawa na kifungo cha nje kwa sharti la kutunza amani na kuwa mtu mwema mtaani. Endapo mtu huyu atatenda kosa jingine katika kipindi hiki cha uangalizi basi atapewa adhabu nyingine kubwa zaidi.

CHANZO   CHA   HABARI :  GAZETI  LA  JAMHURI ,  FEBRUARI , 10 , 2016.