Watu
ambao wana uelewa mkubwa sana wa fedha, yaani wahasibu, wanahisabati,
wachumi na hata washauri wa mambo ya fedha, huwa siyo wafanyabiashara
wazuri. Yaani huwa wakiingia kwenye biashara hawafanikiwi ukilinganisha
na wasiokuwa na uelewa mkubwa wa fedha.
Huku
watu wasiokuwa na uelewa mkubwa wa fedha, ambao hawajui hata kuandika
cheki vizuri, wakiingia kwenye biashara wanafanikiwa sana.
Katika
maeneo mengi ya maisha, kadiri mtu anavyokuwa na uelewa mkubwa, ndivyo
anavyochelewa kufanya maamuzi. Wale wenye uelewa mdogo, wanafanya
maamuzi haraka, lakini wenye uelewa mkubwa wanahusisha mambo mengi
kwenye maamuzi na hilo linawachelewesha kufikia maamuzi.
Inapokuja
kwenye fedha, wasiokuwa na uelewa mkubwa kwenye fedha wanatumia hesabu
za aina tano tu kwenye mambo ya kifedha, kujumlisha, kutoa, kugawanya,
kuzidisha na asilimia. Ni hesabu hizo tu zinazotosha kuendesha biashara
yenye mafanikio.
Wakati
wale wenye uelewa mkubwa wa fedha wanakuwa na hesabu nyingi zaidi
wanazotumia kwenye maamuzi, mfano, makadirio (projections), uwezekano
(probaility), hatari (risk) na nyingine nyingi katika kufanya maamuzi,
kitu ambacho kinawachelewesha na hata maamuzi wanayofanya yanakosa
uhalisia.
Kama
wewe una uelewa mkubwa wa kifedha na unataka kufanikiwa kwenye
biashara, kubali kuweka sehemu ya uelewa wako pembeni na uendeshe
biashara kwa vitendo na siyo nadharia.
Unaposoma
taarifa za kifedha, angalia zile hatua unazoweza kuchuka ili kukuza
biashara yako sasa badala ya kuhangaika na vitu vya kufikirika.
Ukishajua
MAGAZIJUTO basi una maarifa ya kifedha ya kukutosha kufanikiwa kwenye
biashara yako. Muhimu ni kuzijua namba zako muhimu kwenye biashara kama
masoko, mauzo, gharama za kuendesha biashara, faida na mtaji ili uweze
kuendesha biashara yenye mafanikio makubwa.