Watu
wengi wamekuwa wanakutana na hali hii, akiwa hana fedha anakuwa na
mawazo na mipango mizuri sana ya kutekeleza anapopata fedha. Anakuwa
mpole na mwenye akili nzuri juu ya matumizi ya fedha. Akiona wengine
wanatumia fedha vibaya anajiambia kama mimi ningepata fedha hizo, basi
ningefanya mambo mazuri sana.
Lakini
mtu huyo huyo anapopata fedha, anajikuta anafanya vitu ambavyo hata
hakupanga kufanya. Mtu akishapata fedha zile akili nzuri na mipango
aliyokuwa nayo anasahau kabisa. Anajikuta ananunua vitu ambavyo
hakupanga kununua, mahitaji muhimu ambayo hayakuwepo awali yanaanza
kujitokeza. Ni mpaka fedha hiyo inapoisha ndiyo mtu anarudi kwenye akili
zake na kujiuliza zile fedha zimeishaje bila kufanya mambo mazuri.
Kama
umewahi kukutana na hali kama hii usijione kama una bahati mbaya, au ni
mjinga sana inapokuja kwenye fedha. Jua hiyo ni hali inayowakumba watu
wengi kwenye fedha, na inatokana na wengi kutokuielewa vizuri saikolojia
ya fedha. Fedha ni nguvu, na nguvu yoyote isipodhibitiwa na kutumiwa
vizuri inaleta uharibifu.
Leo
nakwenda kukushirikisha dhana itakayokuwezesha kuwa na udhibiti mzuri
kwenye fedha zako, dhana itakayokuzuia usitumie hovyo fedha pale
unapokuwa nazo.
Dhana
hii ni kuhesabu fedha kwa kulinganisha na maisha ambayo umepoteza
kupata fedha hizi. Wote tunajua kwamba muda ni fedha, na pia tunajua
kwamba muda ni maisha, hivyo basi maisha pia ni fedha.
Sasa
chukua kipato chako unachopata kwa mwezi, kisha gawa kwa masaa
unayofanya kazi. Mfano kama kipato chako ni milioni moja, halafu
unafanya kazi masaa 8 kwa siku, siku 5 au 6 za wiki, kwa mwezi unafanya
kazi kwa masaa 160 mpaka 200. Ukigawa milioni moja kwa masaa 200 utapata
shilingi elfu 5. Hii ina maana kila saa unayofanya kazi unalipwa
shilingi elfu 5.
Sasa
kwa sababu muda ni fedha na maisha ni muda hivyo maisha ni fedha, kila
elfu 5 unayoipata, unapoteza saa moja ya maisha yako. ukipata elfu 10
umepoteza masaa mawili.
Sasa
kila unapotaka kununua kitu, kabla hujafanya maamuzi ya kukinunua
jiulize kwanza swali hili, je kitu hiki ninachokwenda kununua, kina
thamani sawasawa na maisha niliyopoteza?
Kwa
mfano umekutana na nguo ambayo inauzwa shilingi elfu 20, umeipenda
kweli na unataka kuinunua. Jiulize kwanza je nguo hii ina thamani sawa
na masaa manne ya maisha yangu? Je kama nikiambiwa nichague kupata nguo
hii na kupata masaa manne zaidi kwenye maisha yangu nitachagua nini?
Kwa
kuchukulia fedha zako kama maisha ambayo unapoteza, utajijengea nidhamu
kubwa sana ya fedha na kuacha matumizi ya hovyo, yasiyo na manufaa
kwako. Pia utapata muda zaidi wa kufanya yale muhimu kwako, pamoja na
kuwekeza fedha zako maeneo ambayo yanazalisha na hivyo kukusaidia
usifanye kazi muda mrefu kupata fedha za kupoteza.
Linganisha
kila fedha unayotaka kutumia na maisha unayopoteza, na utaona jinsi
gani vitu vingi unavyopenda kununua havina thamani unayovipa.
No comments:
Post a Comment