BADILI FIKRA.FIKIRI TOFAUTI .BADILI MAISHA.JITAMBUE .JIFUNZE ELIMU YA SAIKOLOJIA,TEOLOJIA , FEDHA ,UTAMBUZI(SELF HELP EDUCATION),FALSAFA YA MAISHA,MAISHA NA MAFANIKIO,BIASHARA / UJASIRIAMALI.FURAHIA WASAA WAKO NA MAISHA NA MAFANIKIO BLOGU.THIS IS THE COMMUNITY CAPACITY BUILDING BLOG.ENJOY THE BLOG.STRETCH YOUR MIND. YOU CAN CHANGE YOUR LIFE FOR EVER. YOU CAN ACHIEVE EXCELLENCE.YOU CAN MAKE A DIFFERENCE.
Tuesday, January 3, 2023
Monday, November 1, 2021
Sunday, October 10, 2021
Friday, October 1, 2021
Friday, September 3, 2021
MITIHANI YA MAISHA HAINA MWISHO , UKISHINDA MTIHANI HUU UNAKUJA ULE.
Bila maandalizi maishani ni kukubali kushindwa au kufeli. Maandalizi hutusaidia kupunguza mawezekano ya kushindwa, kushangazwa au hata kuumia. Wanasema wakati wa vita sio wakati sahihi wa kufanya maandalizi isipokuwa kabla ya vita ndo ulikuwa wakati sahihi wa kujiandaa. Si hilo tu hata maisha ya kila siku bila maandalizi ya mapema ni mtu kujiandaa kushindwa au kuumia zaidi.
Imekuwa ni kawaida yetu sisi binadamu kutoweka uzito katika maandalizi ya mambo mengi maishani na hili linajitokeza kutokea kwa mambo yakitukuta hatukuwa na maandalizi yoyote yale. Inawezekana ni suala la kiuchumi, mahusiano au hata masuala ya kiafya huwa hatujiandai mpaka pale mambo yamejitokeza na kutuzindua kuwa tulipaswa kujiandaa mapema kabisa.
Maisha yamejaa mitihani na majaribu katika kila kona ya kuishi kwetu ikiwa ni kutufungua na kutukumbusha ilivyo haja kubwa ya kuwa na maandalizi mapema ya mambo hayo. Mambo mengi yanayojitokeza na tukayaona ni kama yametokea ghafla kama ajali ni kuwa hatukuwa na maandalizi nayo. Kila mtego ambao mtu anaweza kukutwa amenaswa ni kuwa hakugundua mapema kuwa ilibidi kujua ishara za awali na kujiandaa ili asijekushindwa katika mtihani huo. Wengi tumejikuta tunaanguka katika mambo mengi maishani sababu ya kuondoa nafasi ya maandalizi ambayo ilipaswa kuwepo kila siku.
Maisha hayaachi kutufundisha uhalisia wake kuwa kuna nyakati ngumu na nyepesi, furaha na huzuni, giza na nuru, kushuka na kupanda, kufaulu na kufeli na kuishi na kufa. Safari zote hizi hujitokeza na zinakuja wakati wowote ule ambao mtu anaweza asitegemee ingekuwa hivyo. Bila maandalizi ya kujua hilo ndo kunakozalisha kuyaona maisha yana sura moja tu ya kuwa ni magumu na yasoruhusu watu kuwa na furaha. Yote hujitokeza sababu ya mtu kukosa kujiandaa na kujua ukweli huu wa maisha kuwa wakati wowote ni safari ya maandalizi kwa kuwa mitihani haikosi kuwepo maishani.
Tunapaswa kujiandaa kukutana na kila aina ya watu ambao wanaweza kutufundisha vitu au kutuachia maumivu, wanaweza kutusaidia kukua au kutudumaza kabisa, watu wanaoweza kutuunga mkono au kutukatisha kabisa tamaa, watu ambao watafurahia hatua zetu au kutozifurahia. Aina ya watu hawa tunaweza kukutana nao katika safari ya maisha yetu ya kila siku. Tunapokosa kuwa tayari kujiandaa kwa hilo tunakubali kuumia na kushangazwa na mambo yatakapojitokeza.
Jiandae kwa kila hatua yako hasa pale ambapo upo karibu na watu wanaokuzunguka. Watu wanaotuzunguka wana uwezo mkubwa wa kutufanya tujikute tunaumizwa nao kwa vitu ambavyo wanaweza kuvifanya na tukabaki kushangaa kwa sababu huwa hatujiandai kuwa hata wanaotuzunguka ni watu wenye madhaifu na wanaweza kutuumiza pia. Mitihani ya maisha inaweza kuja kutoka eneo lolote na mtu anapokosa kujua hili tu ni kujiandaa kuumia na kushangazwa na mambo hayo.
Jiandae kwa kuyaweka mambo katika makundi mawili. Kundi la kwanza ni lile lile la kuangalia mambo yaliyo katika uwezo wako ushughulike nayo na kundi la pili ni yale mambo yaso katika uwezo wako uyaache kama yalivyo au kuwa tayari kuishi nayo. Ni falsafa ngumu kuifuatilia ila inampa nguvu mtu katika kujiandaa na kukabiliana na mitihani maishani na majaribu mengi ambayo hujitokeza kutupima na kufungua uhitaji wa kujiandaa zaidi kila siku.
JIUNGE DARASA--ONLINE " UJIFUNZE MENGI USIYOYAJUA TUWASILIANE SASA NIKUUNGE KWA DARASA. "
NA KOCHA MWL. JAPHET MASATU , DAR ES SALAAM , TANZANIA
WhatsApp + 255 716924136 / + 255 755 400128
Thursday, September 2, 2021
KUWA NA VIPAUMBELE KATIKA MAISHA NA VIFANYIE KAZI
Tunaingia katika taabu maishani sababu ya kukosa msingi wa kujipa msimamo dhidi ya mambo fulani fulani katika maisha. Mtu anaporuhusu kila kitu kiwe sehemu ya maisha yake ni kuruhusu kuyaweka maisha hatarini. Mtu anayekosa msimamo ni rahisi kuyumbishwa na hali zozote zile zitakazojitokeza katika safari ya maisha. Na watu wengi wapo katika hatari hii ya kutoyapa maisha msimamo au msingi fulani unaowaongoza kutoyumbishwa na mambo maishani.
Msimamo hauendi pekee katika maisha bali hata uendeshaji wa kazi unahitaji mtu ajiwekee msimamo fulani ili kutoyumba kwa kazi zake. Mfano kama kazi ya utabibu mtu akikosa msimamo fulani alojiwekea wa kazi ni rahisi kuyakubali mambo mengine ambayo ni nje na maadili ya kazi yake.
Msimamo huu wa maisha ni kuchagua mambo ambayo hutakuwa tayari kuyavunja iwe kwa namna yoyote ile mtu atashawishiwa. Msimamo huu ni katika kuweka ugumu wa kutovunja ahadi ambayo mtu amejiwekea mwenyewe dhidi ya misingi fulani maishani. Hili humsaidia mtu kuwa na maisha yasoyumbishwa.
Ni hatua ngumu ambayo si watu wote wanaweza kuiendea katika maisha. Kuwa maisha yao yataongozwa na misimamo fulani fulani ambayo itawafanya waonekane ni watu wenye misimamo mikali dhidi ya wengine, au watu wasojali hisia za watu wengine. Ila hakuna matokeo mazuri maishani yanaweza kujitokeza isipokuwa kwa mtu kuweka mambo yake katika msimamo asokubali kuvunja kwa namna iwayo yoyote ile.
Weka msimamo katika kazi unayofanya, weka msimamo katika namna unavyohusiana na watu na weka msimamo katika mambo yote unayojua bila kuwa na msimamo thabiti basi mambo mengi yanaweza kuharibika. Hili litakusaidia kuwa na maisha yenye uimara na utulivu wakati wote. Kuna faida kubwa katika kujenga msimamo maishani ili lolote linalokuja kwako linakukuta ukiwa imara na hutayumbishwa na kitu chochote kile.
NA KOCHA MWL. JAPHET MASATU , DAR ES SALAAM , TANZANIA.
WhatsApp + 255 716 924 136 / + 255 755 400128 / + 255 68 361 539
MAGUMU , MATATIZO NI SEHEMU UKUAJI KATIKA SAFARI YA MAISHA , USIJILAUMU NA KULALAMIKA
Kujilaumu ni kitendo cha kujiona mwenye hatia dhidi ya jambo fulani unaloona kwa namna moja umelisababisha litokee na linakuumiza sana ukilitafakari. Hali hii ni mbaya tena iso na usaidizi wowote ule mbali na kuongeza ugumu na taabu ya jambo apitialo mtu. Mtu anaweza kuendelea kuumia juu ya jambo alofanya iwe ni siku za karibuni au miaka mingi imepita. Haisaidii kujilaumu au kulaumu mtu juu ya matukio mbalimbali yanayotokea maishani.
Jamii zetu nyingi tumejengewa hali za kulaumu watu pale mambo yanapoenda tofauti na vile ambavyo tumepanga. Hivyo watu wengi kulaumu wengine inakuwa inaonekana ni kisingizio cha kujiondoa dhidi ya jukumu hilo na kuona wengine walipaswa kuadabishwa kwa hilo. Wakati wote kulaumu au kujilaumu hakujawahi kusaidia kutatua majukumu ya maisha mtu anapoishi. Ni kujisahaulisha tu kuwa tatizo halipo ingali tatizo lipo.
Eneo mojawapo ambalo watu wengi huanza kujilaumu ni pale ambapo vipindi vya hali ngumu maishani vinapobisha hodi, watu hujilaumu huenda wao si watu wenye bahati maishani, wao ni watu wanaonewa, wao hawastahili kupitia hayo na wengine ni kuona ni mikosi tu wao kutokoma kupitia hayo magumu. Magumu ni tafsiri yetu tunayoiweka katika yale yanapotokea maishani. Inaweza kuwa ni matukio yenye kuumiza yamekuja kwa mkupuo kama misiba, hali zisizoleta dalili za afueni iwe ni mahusiano au uchumi, hali za kiugonjwa na kadhalika.
Magumu hutukuza misuli ya akili, hutukuza kuwaza kiutu uzima. Hili ndilo linalowasaidia watu wengi katika umri mdogo kuwa na uwezo mkubwa wa kukabiliana na maisha ambapo kumetokana na wao kupitia magumu na magumu hayo hayakuwadumaza bali yaliwasaidia kukua zaidi. Si rahisi mtu aliyepitia magumu na yakamsaidia kukomaa kushangazwa na hali ngumu za maisha zikitokea maana tayari anajua na uzoefu wa kupitia magumu ya awali. Watu imara hawatengenezeki kwa njia rahisi isipokuwa kwa darasa la kushinda changamoto na kukabiliana na kila gumu njiani.
Mtoto ambaye anaepushwa asipitie magumu au kujua uhalisia wa maisha mapema ni kumwandaa kutokuwa imara siku za baadaye. Atakapokuja kuishi na kukutana na magumu kwa mara ya kwanza lazima itampa wakati mgumu sana kukabiliana na hilo. Huenda wazazi wengi wanaogopa kuwaambia watoto wao juu ya ugumu katika kuyakabili maisha kwa kuona watakuwa wakiwaonea ila si kweli bali wanawapa wakati mgumu baadaye watakapopita katika magumu hayo. Magumu humfanya mtu akutane na ukweli wa maisha kuwa maisha ili ukue kiuzoefu lazima upite magumu mbalimbali yanayomjenga mtu kuwa imara na kuyaendesha maisha.
Uhalisia wa maisha ni kuwa mtu atapitia magumu katika siku za kuishi kwetu. Magumu yapo na yataendelea kuja kwa namna tofauti tofauti. Si kuyalaumu pale yanapokuwa zamu yake kujitokeza. Magumu hutuimarisha na kutukuza kuyaona mambo
NA KOCHA MWL. JAPHET MASATU , DAR ES SALAAAM , TANZANIA
WhatsApp + 255 716 924136 / + 255 755 400128 / + 255 688 361 539
KUPOTEZA " TUMAINI " NI KITU KIBAYA SANA KATIKA MAISHA
Maisha yanaweza kukupitisha katika nyakati ngumu ambazo mbele yako huoni kama utatoka au kuna nafuu yoyote. Nyakati hizi ndizo zinazofanya wengine wasiamini kama lipo tumaini au njia ya kuvuka. Ni lugha ngumu mtu kukuelewa pale anapopitia magumu na unamwambia kuwa hayo magumu utashinda tu huku akiangalia hakuna dalili zozote za suluhisho. Kibinadamu si hali rahisi kushawishiwa kuwa mambo yatakaa sawa na yatapita. Hili ndilo ambalo watu wengine huamua kukatisha maisha yao kwa kuona hawaoni msaada unaoweza kuwatoa walipo.
Hali ya kukosa tumaini inaweza kumkuta mtu yeyote yule katika zama tuishizo. Mambo yanapobadilika ghafla na matarajio mbalimbali kupotea ni hali inayosababisha mtu ashuke hamasa ya kufanya vitu, changamoto zinapokuwa hazikomi, hali ngumu za kiuchumi, migogoro katika kazi au mahusiano, nyakati ngumu za masoko na biashara vinapokuja kwa pamoja kwa mtu mmoja si jambo jepesi la kuvumilika. Ni wengi utakuta wanapata hali ya kukosa hamasa, wanashuka ari ya kufanya kazi na mzigo unapowazidia basi tumaini la nafuu ya hali wapitiazo hufifia au hata kuzima kabisa. Inahitaji ustahimilivu, faraja na nguvu ya kutia moyo na watu wengine kipindi cha hali ngumu.
Mtu anapoanza kupoteza matumaini ni dalili za hatari ambapo asiposaidiwa ni rahisi kufanya maamuzi mabaya ya kimaisha. Hali ya kukosa tumaini huanza pale ambapo mtu huanza kukata tamaa kwa yale anayoyapitia. Huenda ni katika kila jaribio mtu anaona kushindwa na kuanguka. Kukata tamaa kunamsababisha mtu afadhaike na kupata hali ya kupata hatia, kuona hamasa haipo tena na kujawa na hali ya kukata tamaa kabisa ya kimaisha. Hali hizi huwatokea watu wengi wanaopitia hali za sonona katika maisha ambapo kutokana na hali mbalimbali walizoshindwa kuzikabili basi wakajikuta wanazidiwa na kupoteza tumaini.
Magumu katika maisha hayakosekani na si kuwa watu hawapitii magumu. Ikiwa kila mmoja atahadithia simulizi ya yale aloyapitia utakuja kuona unayoyapitia huenda ni madogo. Kinachotia moyo ni kuwa wapo ambao maisha yao ukiyatazama unaona la kwako unalopitia ni dogo na wakati mwingine maisha yao yanaweza kukutia moyo kuwa hupaswi kumbe kukata tamaa. Kila wasaa unapoona tumaini linafifia jipe wasaa wa kuona watu wengine wenye magumu zaidi wasivyokata tamaa wala mioyo yao kuinama.
Unaweza kupoteza kila kitu maishani na ukarejea tena katika kuyaishi maisha endapo hutapoteza “tumaini”. Watu wengi ambao wamepitia magumu, taabu na shida na wakainuka tena hawakupoteza tumaini. Waliweka tumaini kuwa licha magumu yote ambayo yamejitokeza bado wanaona ipo njia, hali zitabadilika na mbele kuna njia ya kutoka. Maisha huwa mapya pale ambapo kila unapopitia magumu hupotezi tumaini kwa kile unachokifanya, tumaini la kuishi na tumaini la kuona kila kitu kitakuwa sawa kadri muda unavyoenda.
Kuna nyakati ambazo nilipitia ngumu sana, niliona siwezi kuinuka tena, niliona ndo mwisho wa kile nilichokuwa nakitegemea ila ninashukuru kuwa nilibakiwa na hali ya kuwa na tumaini kuwa hali nayoipitia itapita. Hili limekuwa likinisaidia hata sasa kuwa kwa kila hali ambayo itatokea iwe ngumu, yenye misusuko mingi nachotakiwa kukitunza ni kuwa na tumaini kuwa mambo yataenda tu. Tumaini ni ukombozi mkubwa katika maisha tuishiyo duniani.
NA KOCHA MWL. JAPHET MASATU , DAR ES SALAAM
WhatsApp + 255 716924136 / + 255 755 400128
Saturday, July 10, 2021
KILA MTU ANA KIU YA KUTENDEWA UKARIMU / MEMA---" UKARIMU NI MGUSO WA PEKEE KWA KILA BINADAMU.
Maisha yetu sisi binadamu yanahitaji mguso. Mguso wa kutendewa mambo mazuri hata kama sisi tunawatendea wengine mabaya au tu wabinafsi. Ile kiu ya kutendewa mambo kwa ukarimu huwa kunatugusa sana. Kiu hii au njaa hii imo kwa kila mtu katika moyo wake kutamani kuona anapata kutendewa mema na mazuri. Licha tunaweza kuishi katika nyakati ambazo zimejaa watu wenye chuki, wasio na upendo bado mioyo yetu inatafuta wapi itapata ukarimu, wapi upendo ulipo, wapi furaha ilipo na wapi pa kupata matumaini.
Jamii zetu zina upungufu mkubwa wa watu ambao wana mioyo ya majitoleo. Kila mtu anapambana kuona ni kwa vipi atafaidika kuliko namna atakavyosaidia wengine wafaidike kwanza. Hili linajenga watu wakose ukarimu, wakose kusaidia wengine na wengine hata kuzuia wengine kupata vitu vizuri. Ukarimu imekuwa bidhaa adimu katika maisha tunayoishi maana kila mtu anajifikiria yeye mwenyewe tu na kusahau kuangalia wengine.
Usijekushangaa pale mtu mkarimu anapoonekana ni bidhaa adimu sokoni anapokuwa ni mtu anayewajali wengine, anayewatanguliza wengine, anayejitoa kwa faida ya watu wengine, anayejitosa kuingia gharama kwa ajili ya watu wengine. Si jambo rahisi kupatikana kwa kila mtu kuwa tayari kuingia gharama katika kujisahau yeye kwanza na kuwafikiria wengine kuwa kwa kuwafanyia wengine ukarimu ni yeye mwenyewe kujifanyia ukarimu. Ni vile mtu anavyojitoa kusaidia wengine ni yeye anajisaidia, ni kama vile mtu anavyoona kuwanyima nafasi wengine kufanikiwa ndivyo na yeye anavyojinyima kufanikiwa. Lolote lile tunalowafanyia wengine si kuwa wanaathirika wao tu bali hata sisi tunaathirika iwe moja kwa moja au njia nyingine.
Watu waliojeruhika ni wengi katika mioyo yao, watu walipitia mateso na taabu ni wengi, watu walopita manyanyaso ni wengi. Tendo la ukarimu kwa makundi haya ya watu ni jambo kubwa lisiloweza kupimika. Watu hawa wana kiu na njaa ya kuona hata kidogo wapate kuona matendo mema na ya ukarimu yakifurika katika maisha yao. Tendo jema lina mguso na huacha alama kubwa kwa maisha ya watu.
Tunaishi sasa na ipo siku ambayo tutayaacha maisha haya ya mwili na kufa. Kumbukumbu la maisha yetu itaanzia kwanza katika wema tulotenda kwa wengine au ubaya kwa wengine. Matendo mema huliliwa sana na watu ambao walitenda katika siku za uhai wao. Matendo ya ukarimu hugusa mioyo ya watu na huacha alama njema ya jina la mtu duniani. Tafuta nafasi hata ndogo ya kuonesha matendo ya ukarimu kwa watu wanaokuzunguka. Utaacha mguso usiofutika katika maisha yao na hii ni maana njema ya kuishi kikamilifu na kuishi kwa umoja kwa kuhesabu watu wanaokuzunguka ni sehemu ya viungo vya mwili wako.
UJUMBE : TAFUTA NAFASI YA KUTENDA TENDO LA UKARIMU. MUNGU AKUBARIKI SANA.
Ndimi KOCHA MWL. JAPHET MASATU , DAR ES SALAAM , TANZANIA.
( WhatsApp + 255 716 924136 ) / + 255 755 400 128
Tuesday, June 15, 2021
MIHEMKO : MOTO UNAOTUTEKETEZA.
Tunaishi katika wakati ambao vyombo vya habari vimepata nafasi kubwa ya kutoa taarifa, matangazo au habari ambazo zinasababisha watu wengi kuhemka au kujengewa hofu dhidi ya mambo yanavyoendelea katika jamii. Utaona au kusikia matangazo iwe katika vyombo vya habari au mtandaoni yote yameshajua namna yanavyoweza kufanya watu washindwe kujidhibiti kuamua mambo au kufuatilia vitu. Hili limechangia sana watu wengi waendeshe maisha yanayokosa utulivu kabisa.
Utaona naona ambavyo matukio mengi yakitokea iwe ni jambo linalovuma mtandaoni basi kila mtu hatataka kutulia limpite bali afuatilie. Kufuatilia huko hakujasaidia zaidi kumeleta usumbufu mkubwa kwa maisha ya watu wengi pale ambapo hata wameweza kuwa wamejiunga kupewa taarifa ya mambo ikitokea basi waarifiwe almaarufu “notifications”. Hili limesababisha watu muda wote wakae mitandaoni au kushika simu kuhakikisha hapitwi na matukio yoyote yale. Hili limesababisha watu wengi wakose muda binafsi wa kukaa wenyewe kutafakari maisha.
Si ajabu kuona leo hii watu wakishindwa kudhibiti hisia zao za furaha au huzuni kwa kushirikisha kila kitu katika mitandao ya kijamii. Mfano mtu kagombana na mpenzi wake basi hilo tukio atataka watu wote wajue kuwa mahusiano yao yapo katika migogoro. Wengine hata wameweza kuthubutu hata kuanika mambo yao ya siri mtandaoni na baadaye wanajutia juu ya maamuzi hayo waloyatenda sababu tu ya mihemko au hasira.
Bado kuna kundi la watu wachache ambao wana uwezo wa kudhibiti mihemko yao licha wanaweza kuonesha kwa wengine namna walivyoguswa na matukio au hali wazipitiazo. Mtu anajenga udhibiti wa mihemko akijua katika mihemko kuna maamuzi ya ovyo hufanyika na mwisho wake ni fedheha. Mtu ambaye pia anashindwa kujidhibiti kifalsafa ni kudhihirisha uchanga wa kuielewa falsafa. Udhibiti wa mihemko au hisia ni ukomavu ambao katika shule ya falsafa unahimizwa sana maana kuna manufaa makubwa katika udhibiti wa mihemko kuliko hasara zake.
Njia ni ile ile katika udhibiti wa mihemko kwa kujiuliza je nitakalo kulifanya ni lazima kulifanya ?. Kadri unavyojiuliza na kujihoji juu ya ulazima wa kushirikisha kitu, kusema kitu, kufanya kitu ndivyo unavyoweza kuamua kitu kwa hekima na bila majuto siku za usoni.
Karibu Ujiunge na " DARASA ONLINE " kujifunza zaidi
Tuwasiliane
Sunday, June 13, 2021
WAEPUKE KAMA UKOMA WATU WENYE TABIA HIZI 15 , NI SUMU KWA MAFANIKIO YAKO.
Rafiki yangu mpendwa,
Kuna watu wanaitwa ‘watu sumu’ watu ambao kwa kujihusisha nao unajikuta ukirudi nyuma badala ya kusonga mbele.
Kwa kuwa wale unaojihusisha nao huwa wana ushawishi mkubwa kwako, unapaswa kuwa makini sana na kila mtu unayemruhusu awe karibu yako.
Leo tunakwenda kuziangalia tabia 15 za watu hao sumu, kama unazo unapaswa kuziacha na ukiwaona watu wanazo kaa nao mbali.
Tabia 15 za watu sumu wa kuwaepuka kwenye maisha yako.
( 1), KUISHI JUU YA KIPATO.
Mtu yeyote anayetumia zaidi ya kipato chake ni mtu sumu, hataweza kupiga hatua kubwa kwenye maisha yake.
Hawa ni watu ambao hukopa fedha kwa matumizi ya kawaida ambayo hata siyo muhimu.
Kama una tabia hii acha mara moja. Na ukishaona mtu ana tabia hii achana naye, maana atakushawishi na wewe uwe kama yeye.
( 2 ). WANAJUA KILA KITU KWENYE MICHEZO NA BURUDANI.
Watu
sumu huwa wana muda mwingi wa kufuatilia mambo ya michezo na burudani
kuliko wanavyotumia kufanya mambo ya kuwapa mafanikio.
Badala ya
kuyageuza maisha yao kuwa burudani kwao kwa kuziishi ndoto zao,
wanatafuta burudani kutoka nje, kitu ambacho huwa hakiwasaidii.
Chagua kupata burudani kwenye kuishi ndoto zako na siyo kuhangaika na ndoto za nje.
( 3 ). KUFUATILIA WATU MAARUFU.
Watu sumu huwa wanafuatilia na kujua maisha ya wengine kuliko wanavyoyajua maisha yao wenyewe.
Wanayajua mahusiano ya watu maarufu, wanajua kiasi cha fedha walichonacho na hata wanajua jinsi ya kuwashauri.
Cha
kushangaza, hawajui kuhusu fedha zao wenyewe na hawawezi kujishauri
licha ya maisha yao kuhitaji sana ushauri kuliko hata wanaoutoa kwa
wengine.
Acha mara moja kufuatilia maisha ya wengine na pambana na maisha yako, na wale wanaopenda kufanya hivyo, achana nao.
( 4 ). HAWAPENDI HATARI.
Kufanya vitu vipya kuna hatari ya kushindwa, watu sumu hawapendi kushindwa, hivyo hufanya yale tu waliyozoea.
Wakikuona wewe unajaribu vitu vipya na vikubwa hawatakuacha kirahisi, watakukosoa na kukukatisha tamaa ili usichukue hatua hizo.
Tambua
bila kuchukua hatua hatari huwezi kufanikiwa, hivyo achana na yeyote
anayekukatisha tamaa kwenye hatua kubwa unazopanga kuchukua.
( 5 ). HAWANA MSUKUMO MKUBWA.
Watu
sumu wameridhika sana na maisha ya chini waliyonayo, hawana msukumo wa
kufanya makubwa zaidi. Wakipata kazi wanaona wamemaliza kila kitu.
Wakiwa na biashara ndogo wanaona wameshayawezea maisha. Ni mpaka
wakutane na changamoto ndiyo wanajua mazoea siyo mazuri.
Wewe kuwa na
msukumo wa kufanya makubwa, jiwekee malengo makubwa na pambana
kuyafikia, ukishayafikia usiridhike, weka malengo mengine makubwa zaidi.
Achana kabisa na wale walioridhika na maisha yao ya chini.
( 6 ). WANAWALAUMU WANASIASA.
Watu
sumu huwa wanatupa lawama zao kwa wanasiasa na wengine wenye mamlaka.
Kama hawajapata wanachotaka, wanaona sababu ni wanasiasa.
Wanawasikilia na kuwaamini wanasiasa wanapowaahidi mambo mbalimbali.
Wasichojua ni kwamba wanasiasa wanaishi kwa kuwategemea wao, hivyo hawawezi kuwasaidia kwa namna yoyote ile.
Jua haya maisha ni vita yako mwenyewe, kama utashinda au kushindwa ni kwa sababu zako mwenyewe hivyo usimlaumu yeyote.
Usimwamini mwanasiasa yeyote anapokuahidi chochote, pambana kwa juhudi zako kupata kile unachotaka.
( 7 ). WANACHUKIA MATAJIRI.
Watu
sumu huwa wanawachukia sana matajiri, wanawaona ndiyo chanzo cha wao
kubaki kwenye umasikini. Au wanapotaka kitu kutoka kwa matajiri na
wasiwape, wanawaona wana roho mbaya. Wasijue kwamba matajiri hao wana
nidhamu kubwa kwenye yale waliyopanga.
Wapende matajiri, waone ni watu wazuri, jifunze kutoka kwao ili na wewe uweze kufikia utajiri pia.
Na ukimuona mtu yeyote anawasema vibaya matajiri, kaa naye mbali.
( 8 ). WANAKANDIA ELIMU YA MAENDELEO BINAFSI.
Watu
sumu huwa wanajiona tayari wanajua kila kitu kwenye maisha yao. Waambie
wasome vitabu vya maendeleo binafsi na watakuambia hawana muda.
Waoneshe muda wanaopoteza na watakuambia hakuna kipya kwenye vitabu
hivyo, ni yale yale tu.
Wewe usiwe kwenye kundi hilo, penda kujiendeleza binafsi, soma vitabu, jifunze na chukua hatua.
Na unapokutana na mtu akakuambia hakuna kipya kwenye vitabu au tayari anajua yote hayo, kaa naye mbali, ni mtu sumu huyo.
( 9 ). WANAKUPA USHAURI MBAYA.
Watu
sumu hukimbilia kukupa ushauri kabla hata hujawaomba na ushauri
wanaokupa huwa ni mbaya. Kwa sababu hawataki upige hatua kuliko wao,
watahakikisha wanakushauri mambo yatakayokukwamisha.
Usipende kutoa ushauri kwa wale ambao hawajakuomba na epuka sana kupokea ushauri kwa watu ambao hujawaomba.
Gharama ya ushauri wa bure ni pale unapoanza kuufanyia kazi, kwa kuwa utakugharimu sana.
Jua watu ambao ushauri wao huwa una walakini na waepuke sana, maana pia huwa wanalazimisha upokee ushauri wao.
(10 ). KUULIZA MASWALI YA KIJINGA.
Watu sumu huwa wanapenda sana kuuliza maswali ya kijinga. Waambie kitu kizuri na wao watatafuta njia ya kuonesha hakiwafai wao.
Waambie wasome vitabu watakuambia hawajui wapate wapi vitabu.
Waambie wapambane kutoka kwenye umasikini na watakuambia wote hatuwezi kuwa matajiri.
Waambie wajiajiri watakuambia wote tukijiajiri nani atamfanyia kazi mwenzake.
Yote hayo ni maswali ya kijinga na usijisumbue kuyajibu, waache wajiridhishe nayo.
Waepuke sana watu wenye maswali ya kijinga, maswali yanayotengeneza vikwazo kwenye kila jambo zuri.
( 11 ). HAWANA NIDHAMU.
Wanapanga kufanya kitu, ila inapofika wakati wa kukifanya wanaahirisha na kuona hawajawa tayari.
Tatizo siyo kutokuwa tayari, tatizo ni kukosa nidhamu ya kujisimamia na hilo linakuwa kikwazo kwa mafanikio yako.
Jijengee nidhamu ya hali ya juu sana, panga mambo na fanya kama ulivyopanga bila kuruhusu chochote kukuzuia.
Na ukiwaona watu ambao hawana nidhamu, kaa nao mbali.
( 12 ). WANA CHUKI NA WIVU.
Watu
sumu hawapendi kuona wengine wakipiga hatua kuliko wao, hivyo huwa na
chuki na wivu kwa wale wanaopata matokeo mazuri kuliko wao.
Usiwe mtu wa chuki au wivu, kuwa mtu wa kupenda na kujifunza kutoka kwa wengine.
Na unapojikuta umezungukwa na watu wenye chuki na wivu, kimbia haraka.
( 13 ). HAWAWEZI KUDHIBITI HISIA ZAO.
Watu
sumu ni watu ambao hisia zao hulipuka haraka hata kwa vitu vidogo tu.
Huwa ni rahisi sana kukasirishwa na mambo madogo madogo na yasiyo na
tija. Kwa watu kujua udhaifu wao, wanautumia kujinufaisha.
Jifunze kudhibiti hisia zako na usimpe yeyote ruhusa ya kukukasirisha kwa jambo lolote lile.
Pia waepuke sana wale ambao hisia zao zinaweza kuibuliwa na mambo madogo madogo.
( 14 ). WANACHAFUA MIILI NA AKILI ZAO.
Watu
sumu huchafua miili yao kwa kuilisha vyakula visivyo vya afya na vilevi
mbalimbali, hilo hupelekea miili yao kuwa dhaifu na kushindwa kupambana
na mafanikio.
Pia huchafua akili zao kwa kujaza habari hasi na umbea.
Epuka kuchafua mwili na akili yako, lisha vitu ambavyo ni safi na bora. Epuka vyakula vya haraka, vilevi na habari hasi.
Pia waepuke wote ambao hawathamini miili na akili zao.
( 15 ). WANA SABABU NYINGI.
Watu sumu huwa wana sababu za kujitetea kwenye kila jambo. Huwa siyo watu wa kuchukua uwajibikaji kwenye jambo lolote lile.
Wewe achana na sababu, kama kuna kitu kimetokea, kubali kuwajibika. Kwa njia hiyo wengi watakuamini na kukupa majukumu zaidi.
Waepuke sana wale wenye sababu na visingizio kwenye kila jambo.
Saturday, June 12, 2021
WEKA NGUVU ZAKO KWENYE KUFANYA KILICHO BORA LEO , WAKATI BADO UNA NAFASI YA KUFANYA HIVYO.
Wewe Sio Mtabiri Mzuri, Hivyo Acha Kujiogopesha.
Mara baada ya sultani wa dubai kuamua kusafiri baharini na baadhi ya wapambe wake.
Siku iliyofuata walijumuika kwa pamoja kwa ajili ya kuanza safari.
Hata hivyo , wakati meli ilipoondoka kutoka nchi kavu, mmoja wa wapambe wake, ambaye hakuwahi kuona bahari hapo kabla alianza kupata hofu ya kukaa ndani ya meli , alilia na kupiga kelele.
Sultani alijaribu kumtuliza lakini hakumsikiliza.
Watu wengi kwenye meli walijaribu kumtuliza lakini hawakufanikiwa.
Safari ya kila mtu ambayo ilipaswa kuwa ya kufurahia na utulivu , iligeuka kuwa moja ya mateso.
Sultan hakujua cha kufanya.
Siku mbili zilipita kama hivo.
Mpambe huyo alikataa kula hata kulala.
Kila mtu kwenye meli alichukizwa na tabia yake.
Sultan alifikiria inaweza kuwa bora zaidi kurudi bandarini.
Hapo ndipo mtu mmoja alipomjia na kusema, mkuu kwa idhini yako, nitaweza kumtuliza.
Ikiwa tu utaniruhusu kutumia njia zangu bila kuhoji.
Bila kusita, sultan alisema, “ dhahiri “. Una ruhusa yangu.
Si hivyo tu kama utafanikiwa nitakulipa kwa ajili ya kutatua tatizo hili.
Mtu mwenye hekima alitoka nje na kumwambia mmoja wa wafanyakazi “ Mtupie ndani ya bahari, mara moja”.
Mfanyakazi alisita kwanza lakini mtu huyo alikuwa na ruhusa ya sultani, kwa hivyo alimshika mtu huyo na kumtupa baharini.
Mpambe aliripuka na kuzama , akameza maji mengi ya bahari.
Kisha akarudi juu na akapiga kelele zaidi kuliko hapo awali na akazama tena.
Hii ilitokea mara 2-3 na kisha waziri akaamuru arudishwe tena ndani ya meli.
Mpambe alirudishwa ndani ya meli, mara hii hakulalamika wala kulia na safari ikawa na amani.
Kila mmoja alifurahia safari na wote walikuwa na amani.
Baada ya kumaliza safari, meli ilirudi bandarini.
Aliporudi, kabla ya kuondoka kwenye meli , sultan akaenda kumwona, Yule mwanahekima na kumuuliza, ulijuaje kwamba kwa kumtupa mtu huyo baharini, atatulia?
Yule mwanahekima alimjibu , “kwa sababu ya uzoefu wangu wa kwenye ndoa”, baada ya ndoa yangu, siku zote nilikuwa na hofu ya kumpoteza mke wangu na siku zote nilikuwa nikimlalamikia na kama vile mtu huyo alivyofanya kwenye meli.
Siku moja mke wangu hakuweza kunivumilia tena aliniacha.
Kuishi bila yeye ilikuwa uzoefu wa kutisha kutoka kwangu.
Alirudi pale nilipomuahidi kwamba sitamlalamikia tena.
Kwa njia hiyo hiyo, mtu huyo alikuwa hajawahi kupima maji ya chumvi na hakuwahi kujua uchungu wa kuzama.
Lakini alipotupwa baharini na kurudishwa kwenye meli, hapo ndipo alipoelewa.
Umekuwa unatabiri mambo mengi sana kuhusu maisha yako, lakini je ni mambo mangapi uliyotabiri yametokea?
Ni mambo mangapi ambayo ulikuwa unayahofia, yanakunyima usingizi yametokea kweli?
Nafikiri ni machache sana, kama hata yapo.
Ukweli ni kwamba wewe sio mtabiri mzuri, na wala hutakuwa mtabiri mzuri kadiri siku zinavyokwenda.
Umekuwa ukijitabiria kwamba maisha yatakuwa magumu zaidi, kwamba utapata hasara kwenye biashara, kwamba utafukuzwa kazi, kwamba mambo hayataenda vizuri!!
Lakini haya yote huwa yanatokea?
Hayatokei na hata kama yakitokea sio kwa sababu umetabiri ila kwa sababu umeamua kukubaliana na kile unachotabiri.
Unatabiri kwamba utapata hasara kwenye biashara halafu unaendelea kuendesha biashara yako kwa mazoea, unaishia kupata kweli hasara.
Ninachotaka kukuambia leo ni kwamba chochote unachotabiri leo hakina maana, chochote unachohofia leo ni kupoteza muda wako.
Hata ungetabiri kiasi gani na kujijaza hofu kiasi gani hakuna mmoja wetu anayejua nini kitatokea kesho.
Na hii ni vizuri sana kwa sababu lengo lako kubwa ni kuishi vizuri leo, kufanya kile ulichopanga kukifanya leo, kwa ubora wa hali ya juu sana kama vile ndio unakifanya kwa mara ya mwisho na hutakuwa na haja ya kuhofu kuhusu kesho tena.
Kwa sababu ukiishi vizuri leo, unaandaa mazingira mazuri ya kuishi vizuri kesho. Ukifanya kazi yako kwa ubora leo unaandaa mazingira mazuri ya kufanya kazi yako vizuri kesho.
Ukimhudumia mteja wako vizuri leo, kwa huduma nzuri ambayo hajawahi kuipata sehemu nyingine yeyote, unafikiri kesho ataenda wapi?
Unaona mambo yalivyo mazuri sasa?
Huna haja ya kutabiri, huna haja ya kuhofia, weka nguvu zako kwenye kufanya kilicho bora leo, sasa hivi wakati bado una nafasi hiyo ya kufanya hivyo.
NA KOCHA MWL JAPHET MASATU, DAR ES SALAAM
JIUNGE SASA NA DARASA ONLINE UJIFUNZE KWA VITENDO
TUWASILIANE KWA WhatsApp + 255 716 924 136
TUJIFUNZE KUVAA VIATU VYA WENGINE KILA TUNAPOFANYA AU KUSEMA JAMBO.
Sisi binadamu huwa tuna hulka ya kutowafikiria wengine bali kujijali wenyewe tu na wanabinafsi wa hisia zetu. Hili limechangia migogoro mingi katika maisha ya watu iwe ni katika kuishi na watu, kuwaongoza watu au mahusiano. Binadamu wote ni sawa katika mjengo wa mwili kuwa wote wanapata maumivu katika kuumia kama wengine. Hakuna binadamu ambaye mwili wake hauna damu au nyama. Wote ni sawa na hili linafanya hata kufa tutakufa binadamu wote mbali na tofauti zetu za kirika, kikabila, kitaifa au kirangi.
Chuki na unyama ambao huwa unajitokeza katika jamii zetu ni zao la watu kutojali hisia za watu wengine na hawajui namna wanavyoweza kuvaa hivyo viatu. Inawezekana ni tukio la maonevu katika jamii, mauaji au utesaji ila wasijue namna hata na wao wanaweza kupitia hali hizo au kufanyiwa hivyo na huenda wakaumia kama wanavyowasababishia wengine maumivu au uchungu. Kuwatendea wengine yaweza kuwa ni rahisi pale ambapo mtu hajali namna wengine watakavyoumizwa na hayo.
Binadamu pia tuna hisia za furaha na huzuni. Pale mambo mabaya yanapojitokeza huwa tunaumia kihisia, tunapata majonzi, tunapata taabu katika kukabiliana nayo. Mabaya haya si kuwa yanafanywa na wanyama isipokuwa ni binadamu wenzetu ambao kwa namna moja wana watu wanaowazunguka, wenye hisia kama wengine na wenye miili kama wengine. Kutenda ubaya tu na kisha kuacha kama mtu hajaona ubaya alotenda ni kuzalisha machungu kwa wengine ambao nao huwezi jua ni kwa namna gani hujipanga kuachilia au ulipizaji wa kisasi.
Ni rahisi kutusi wengine, rahisi kutotenda haki kwa wengine na ni rahisi kutojali wengine katika makubaliano fulani. Utakuta ni hali ya kawaida katika jamii zetu huwa tunapanga muda fulani wa jambo kufanyika ila watu hatuendi hivyo na wakati mwingine hata bila kutoa sababu za msingi. Watu wanaozingatia huwahi kufika na kukaa sana wakisubiri wengine. Hatujui ni kwa namna gani hukwazika na hilo jambo, lakini utakuta huwa hatujali hilo kuwa namna wengine watajisikia kwa kuchelewa kwetu. Huenda tunafanya hivyo sababu hatujawahi kuvaa viatu vyao kuwa vipi ukiwahi sehemu ukaachwa ukingoja masaa mengi au pengine hata mtu anakuja kukuambia haji licha umesubiri masaa mengi.
Tunaumizwa na mambo mengi katika kuishi kwetu kwa kuwa na watu ambao hawajajifunza au hatujajifunza kuvaa viatu vya watu wengine. Kwa kukosa kujua kuvaa viatu vya wengine tumekuwa ni watu wepesi kuhukumu, kuwasema wengine na kuchukulia wengine wana mioyo migumu na si laini kama wengine. Hili linaumiza jamii nyingi na kuendelea kuzalisha watu wenye mioyo ya kikatili, visasi, chuki na wasio na upendo kwa wanaowazunguka. Ila falsafa inatualika sote kuanza kujifunza kuvaa viatu vya wengine kila tunapofanya jambo au kusema jambo. Tuangalie je ingekuwa ni upande watu tungelipokeaje au kulichukulia.
KARIBU UJIUNGE " DARASA ONLINE "
KOCHA MWL. JAPHET MASATU , DAR ES SALAAM
WhatsApps + 255 716924136 / + 255 755 400128 / + 255 688 361539
EMAIL : japhetmasatu@gmail.com
Tuesday, June 1, 2021
KUJUA KUSUDI LAKO SEMA NDIYO , KUISHI KUISHI KUSUDI LAKO SEMA HAPANA.
VITU VIWILI VYA KUFANYIA KAZI KWENYE MAISHA YAKO.
Ili uweze kufikia mafanikio makubwa na kuacha alama hapa duniani, kuna vitu viwili vikubwa unavyopaswa kuvifanyia kazi. Nimeweza kuja na vitu hivi viwili baada ya kujifunza na kutafakari kwa kina na kuona jinsi watu wanahangaika na mambo mengi lakini hawapati matokeo yoyote makubwa.
Ukiamua kuachana na mengine yote unayohangaika nayo na kufanyia kazi haya mawili tu, utaacha alama kubwa hapa duniani.
Mambo hayo mawili ni KUJUA NA KUISHI KUSUDI LAKO na KUWA NA NDOTO KUBWA unazofanyia kazi kwenye maisha yako. Haya mawili tu ndiyo yanahitaji muda, umakini na nguvu zako zote ili uweze kufanya makubwa.
KUSUDI LA MAISHA YAKO.
Mark Twain amewahi kusema kuna siku mbili muhimu kwenye maisha ya mwanadamu, siku ya kuzaliwa kwake na siku anayojua kwa nini amezaliwa.
Kila mtu huwa anazaliwa, ndiyo njia pekee ya kuja hapa duniani. Lakini ni wachache sana wanaojua kwa nini walizaliwa na hao ndiyo wanaoleta matokeo makubwa na kuacha alama hapa duniani.
Ubaya ni kwamba kujua kwa nini umezaliwa ni wajibu wako mwenyewe, hakuna anayeweza kukufundisha wala kukuambia. Hata wazazi waliokuzaa hawajui kwa nini ulizaliwa. Walimu wanaokufundisha ndiyo kabisa wanaharibu, maana wanakulazimisha uwe kitu kingine na siyo wewe.
Unahitaji mabadiliko makubwa kwenye maisha yako ili uweze kujua kwa nini ulizaliwa, unahitaji kuvunja mazoea mengi uliyojenga kwenye maisha yako ili uweze kuisikiliza sauti ya ndani yako na kujua kwa nini uko hapa duniani.
Wengi hawajui kusudi la maisha yao kwa sababu wameamini kile ambacho jamii na mfumo wa elimu umewalisha kwa miaka mingi. Kama shule ilikuambia umefeli kwa sababu huna akili, unaamini hivyo kwamba huna akili. Wakati shule haiwezi kupima uwezo mkubwa ulio ndani yako, kitu ambacho shule inapima ni kukariri.
KUJUA KUSUDI, SEMA NDIYO KWA KILA KITU.
Ili uweze kujua kusudi la maisha yako unahitaji kurudi kwenye maisha ya utoto wako, na kusema ndiyo kwa kila kinachokuja mbele yako. Jaribu mambo mengi uwezavyo, fanya kila kinachokuvutia kufanya na kadiri unavyofanya hivyo utaona kuna vitu unapenda kuvifanya vizuri zaidi na watu wanavifurahia unapovifanya. Hapo ndipo utajua kusudi lako lilipo na kuweza kulifanyia kazi.
KUISHI KUSUDI, SEMA HAPANA.
Baada ya kujua kusudi la maisha yako, sasa unahitaji kuweka umakini wako wote kwenye kuishi hilo. Hupaswi tena kuhangaika na mambo mengine nje ya kusudi hilo.
Muda na nguvu zako vina ukomo, usipoteze kuhangaika na mambo mengine. Kuna mazuri yatakayokuja kwako na yenye fursa ya kunufaika zaidi, lazima uweze kusema hapana kwa hayo mazuri ili uweze kupata yaliyo bora kupitia kuishi kusudi lako.
Ili kuishi kusudi lako, SEMA HAPANA kwa mambo mengine yote na baki kwenye kuishi kusudi lako tu.
Baada ya mimi kujua kusudi langu lipo kwenye kufundisha wengine kupitia uandishi na ukocha, nimekuwa nasema hapana kwa mengine yote isipokuwa kusudi hili.
Ukishajua kusudi lako, yapangilie maisha yako kwa namna ambayo kuishi kusudi hilo ndiyo kipaumbele kikubwa kwako na sema hapana kwa mengine yote ambayo hayahusiani na kusudi hilo.
Ni kwa njia hiyo ndiyo unaweza kuweka umakini, muda na nguvu za kutosha kwenye kusudi lako na liweze kuleta matunda mazuri kwako.
NDOTO KUBWA YA MAISHA YAKO.
Maisha yasiyokuwa na ndoto ni maisha ambayo hayana msukumo wa kuyaishi.
Kama unataka kuacha alama hapa duniani, lazima uwe na ndoto kubwa, lazima uwe na picha ambayo hakuna anayeiona na hata ukiwaambia wengine hawaamini kama inawezekana.
Ukishakuwa na picha hiyo kubwa, unapaswa kuifanyia kazi kila siku mpaka utakapoifikia. Unapaswa kuwa tayari kutoa kafara ya kila aina kwenye maisha yako ili kufika kwenye ndoto yako kubwa.
JISUKUME UANZE LEO , UJITOSE LEO , UMALIZE LEO UTAREKEBISHA MBELE YA SAFARI
Imekuwa ni jambo rahisi kwa watu wengi kughairisha vitu nami nikiwa mmojawapo ya watu ambao nimewahi kupitia hali za kughairisha vitu na baadaye ikawa ni ngumu kufanya tena. Kughairisha kunafariji pale ambapo kitu ulichopaswa kufanya wakati huo unakisogeza mbele au kusema nitafanya baadaye na hilo kushindwa kulifanya. Kughairisha kumeiba ndoto zetu na zimefanya tusiishi kitoshelevu wakati ambao tulikuwa na nafasi ya kufanya.
Unapoghairisha mambo unavuta hali ya kuzembea kuanza kitu ambacho kilikuwa kinawezekana kuanza. Unapofika wakati ujao kile ulichofikiria ungekianza kinaanza kuwa kigumu kukifanya na kadri muda uendavyo unapata ukinzani mkubwa zaidi na hilo linafanya usifanye chochote kile. Wakati unaofaa kuanza kufanya kitu ni wakati huo huo unaosema siwezi sasa nifanye baadaye.
Mara nyingi tunapotaka kuanza kitu basi ndani yetu tunapata sauti ambazo zinatufanya tujishauri kuwa ngoja nitafanya wakati mwingine si sasa. Ile nafasi ya kuamua sasa inapopotea ndivyo wakati unaokuja baadaye inakuwa ngumu kweli kweli kuanzisha kitu. Au wakati mwingine gharama ya jambo ambalo ungelifanya sasa inaweza kuwa mara mbili kwa baadaye. Kumbe kuanzisha kitu sasa kunasaidia kupata matokeo ya haraka zaidi kuliko kujichelewesha.
Kila kitu katika maisha kinahitaji safari na kadri unavyojishauri usianze kufanya kitu ndivyo unavyochelewa katika safari ya kitu hicho. Utakuwa umekutana na watu ambao walikuwa na nafasi ya kuanzisha biashara mapema wakiwa na nguvu ila wanangoja hadi wanapostaafu ndo wanataka kuanzisha biashara ambapo kupata mafanikio kunakuwa kugumu kuliko wale ambao walianza mapema wakaujua mchezo wa biashara na kujua namna ya kuendesha biashara. Unapochelewa kuanza kitu ndivyo unavyochelewa kujifunza mengi zaidi juu ya hicho kitu.
Kuna faida tele za kuanza sasa, wakati ambao wengine wanasema wataanza baadaye wewe jisukume uanze leo, umalize leo na ujitose leo maana muda utakapopita utakuwa upo mbali sana kuliko wengine. Unapojifunza kuchukua hatua leo ndivyo unavyoweza kufanikiwa mapema katika maisha.
Ndimi Rafiki Yako
KOCHA MWL. JAPHET MASATU , DAR ES SALAAM, TANZANIA
WhatsApp + 255 716 924 136 / + 255 755 400 128 / 0688 361 539 / +255 629 748 937
EMAIL : japhetmasatu@gmail.com
KILA TATIZO HATA LIWE KUBWA KIASI GANI LITAPITA TU NA KUSAHAU VUTA TU SUBIRA.
Maisha hupokezana kwa mambo nayo huja na kupita. Yote haya yanakuja ili kutupima na kutufungua akili ilivyo wazi kuwa hakuna jambo zito kubwa kuliko lingine. Mambo mazito tunayapa majina pale ambapo hatuoni njia namna gani tuweze kutoka au kupata suluhisho.
Suluhisho ni njia ambayo jambo lilokuwa likionekana ni zito na gumu kuwa jepesi. Ugumu wa maisha ni pale ambapo tunakutana na nyakati ambazo mbele yetu hatuoni njia, hatuoni nafasi ya kushinda au hatuoni upenyo wa kupita. Magumu huja kutufundisha kuna njia nyingi unazoweza kuzitumia kupita gumu lolote linapojitokeza.
Nyakati ngumu zinazojitokeza mara kwa mara katika maisha yetu haziji kutudumaza bali kutuchangamsha akili tufikiri zaidi, tujichunguze na kutafakari namna ya kuvuka. Changamoto zinapojitokeza hazituachi namna tulivyo awali bali zinatuimarisha na kujigundua kuwa tuna uwezo mkubwa zaidi wa kuvuka vikwazo na kilichokuwa kinatukwamisha ni kihunzi kidogo cha kuruka tu.
Mtu ambaye mara kwa mara anakutana na changamoto na kuzishinda anajitengenezea uimara na uzoefu unaompa nafasi ya kukabiliana na jambo lolote linaloweza kujitokeza katika safari ya maisha. Wale ambao huwa tunawaona wamefanikiwa kwa kitu fulani iwe ni biashara, uongozi, elimu na mahusiano basi moja kwa moja utakuta wamekuwa ni washindi wa changamoto nyingi ambazo zimewakuta.
Changamoto zinazompata mtu zinaweza kuzaliwa katika ugeni wa mambo kunakoweza kuchangiwa na uhafifu wa maarifa, uzoefu na utambuzi. Changamoto zinaumiza pale ambapo mtu anakutana na uhalisia unaovunja kuona kwake kitu katika hali alofikiria ingekuwa hivyo. Hili limepelekea changamoto ziwaangushe wengine, waanguke katika walichokianzisha na kufeli kabisa katika hatua ambazo walikusudia wangeweza kuvuka.
Muda hutusaidia kupisha changamoto ambazo huwa tunapitia. Ukitulia na kufikiria maisha yako utaona kuna nyakati ambazo uliwahi pitia changamoto nyingi na ukafikiria huenda zingekumaliza au zisingeisha na kupita. Ila muda ukazipitisha na kuzigeuza leo yawe mafunzo na kukufanya uwe imara zaidi. Hili ndivyo linavyotokea katika maisha kuwa kila kitu ambacho unakiona ni kizito si kizito kiuhalisia kitakuwa chepesi kadri muda unavyopita na kukivunja vunja kiwe hakina nguvu tena kama ya awali.
Ndimi Rafiki yako
KOCHA MWL. JAPHET MASATU , DAR ES SALAAM , TANZANIA
WhatsApp + 255 716924136 / + 255 755 400128
Saturday, May 15, 2021
JIFUNZE IMANI SAHIHI ITAKAYOKUSAIDIA ULIPWE ZAIDI. USITEGEMEE MSHAHARA PEKEE UTAKUFA MASKINI.
Sio siri tena kwenye hii karne ya 21,
Mambo yamebadilika sana.
Sahau kila kitu ulichowahi kusikia kuhusu kulipwa.
Sasa kuna njia bora ya kulipwa zaidi kuliko ilivyokuwa imezoeleka karne ya 20.
Ni njia ambayo haizungumzwi sana lakini inafanya kazi kwenye hii karne ya 21.
Haijalishi umeajiriwa au umejiajiri,
Inafanya kazi kwenye hali zote mbili.
Ukweli ni kwamba,
Kwa sasa haulipwi kutokana na masaa unayofanya kazi,
Bali unalipwa kulingana na matokeo unayozalisha.
Unapozalisha matokeo makubwa zaidi unalipwa kiasi kikubwa cha fedha.
Unapozalisha matokeo madogo zaidi unalipwa kiasi kidogo cha fedha.
Angalia huu u tofauti hapa chini,
Kuhusu imani walizonazo matajiri na masikini kuhusu kulipwa.
Matajiri huwa wanachagua kulipwa kwa matokeo wanayozalisha na hapo wanazalisha matokeo makubwa zaidi na kulipwa kiasi kikubwa cha fedha.
Masikini wanachagua kulipwa kwa muda wanaotumia kufanya kitu na kwa kuwa muda una ukomo,
Wanajiwekea ukomo kwenye kipato chao.
Matajiri wote wamepata utajiri wao kupitia njia ambazo hazitegemei muda wao.
Kwa mfano kumiliki biashara inayojiendesha yenyewe ,
Kufanya uwekezaji maeneo yanayozalisha na kadhalika.
Kulipwa kwa muda ni kupitia mshahara au huduma binafsi ambazo mtu anatoza gharama kwa muda.
Hakuna mtu amewahi kufikia utajiri mkubwa kwenye maisha yake kwa kutegemea mshahara pekee.
Hata mshahara uwe mkubwa kiasi gani, bado unakuwa na ukomo.
Na mbaya zaidi, kadiri mshahara unavyokuwa mkubwa, ndivyo makato yanavyokuwa makubwa pia.
Kulipwa kwa muda ni kujiwekea ukomo na kanuni ya kwanza na muhimu kwenye fedha ni kuhakikisha huweki ukomo kwenye kipato chako.
Chagua kulipwa kwa matokeo na thamani unayozalisha ambayo haina ukomo,
Badala ya kutaka ulipwe kwa muda ambao una ukomo.
Je, ungependa ulipwe zaidi kwa kile unachofanya?
Kama ni ndio, KARIBU UJIUNGE , " DARASA ONLINE "
Ujifunze njia na hatua za kuchukua ili ulipwe zaidi.
Utajiri ni mchezo,
Mchezo ambao una kanuni zake na sheria zake,
Na ili uweze kushinda mchezo huu,
Lazima uzijue kanuni na uzishike sheria.
Haiwezekani kabisa kwa mtu ambaye hajui kanuni za mpira wa miguu,
Hana mazoezi akaenda uwanjani na kushinda.
Wengi wamekuwa wanaingia kwenye mchezo wa utajiri kama vile ni kitu cha kubahatisha,
Hawajui kanuni wala sheria,
Hawana maandalizi na kinachotokea ni kushindwa vibaya sana.
Karibu sana UJIUNGE " DARASA ONLINE " UJIFUNZE TABIA ZA KITAJIRI ILI KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA.
Ujifunze kwa kina na kuyaelewa maarifa haya muhimu sana kwako,
Kisha uchukue hatua ili maisha yako yaweze kubadilika, ufike kwenye utajiri, mafanikio na furaha.
TUWASILANE SASA,
Ndimi Rafiki yako
Kocha Mwl Japhet Masatu , Dar es salaam , Tanzania.
(WhatsApp + 255 716 924136 ) / + 255 755 400128 / + 255 688 361 539 / + 255 629748 937
EMAIL : japhetmasatu@gmail.com
Saturday, May 8, 2021
ACHA KUMLAUMU MTU YEYOTE BALI KUMBUKA WAJIBU WAKO NI UPI ??
Ni kawaida ya watu kulaumu pale mambo yanapoenda vibaya. Kulaumu kunampa mtu kuona jambo lilotokea hahusiki au kujiondoa katika wajibu fulani. Kulaumu ni kwa watu wasiojua ukweli wa maisha kuwa katika mambo wanayolaumu nao ni sehemu ya matokeo hayo. Kukosa kujua hili kunafanya kundi kubwa la watu mambo yanapotokea vibaya basi kutafuta wa kuwatwika lawama na wao wawe salama kuwa hawahusiki kwa chochote.
Jamii yetu ina watu wachache ambao mambo yakitokea yameenda vibaya basi wanajua kwa namna moja wamesababisha yawe hivyo na wana wajibu wa kufanya kitu kurekebisha, kukubali na kuandaa mpango wa kuchukua hatua ili kuepusha matatizo kama hayo wakati mwingine. Kufanya hivi ni kipimo cha ukomavu na ukuaji ndani ya mtu anapoachana na lawama bali kuwajibika na kuchukua hatua fulani dhidi ya jambo liliotokea.
Mara ngapi umekuwa mtu wa lawama na kulaumu watu ?, umejikuta katika kulaumu hujaongeza chochote zaidi ya kuharibu zaidi au pengine kutochukua hatua zozote zile maana anayelaumu hutaka kuonewa huruma na wengine. Ni mara ngapi tumekua hatuchukui hatua fulani katika maisha kwa kubaki kulaumu asingekuwa mtu fulani ningekuwa sehemu fulani, asingekuwa mtu fulani ningekuwa nimefanikiwa. Kulaumu kunafanya mtu awe mzembe na mvivu kufanya kazi akifikiria kwa kulaumu mambo yatabadilika yenyewe.
Lolote linalotokea jifunze kuangalia ni kwa namna gani na wewe umechangia utokeaji wake. Usibaki upande mmoja kulaumiwa bila kujua na wewe unachangia vipi hali hiyo hadi imejitokeza. Kuna sehemu ukitulia na kufikiria utaona na wewe unahusika katika utokeaji wa mambo mengi. Usiishie tu kulaumu haraka haraka bali angalia upande wako na kuwa tayari kuchukua hatua stahiki. Hili litakusaidia kuvuka vikwazo vya watu wengi wanalaumu tu bila kujua wajibu wao ni upi.
NA KOCHA MWL. JAPHET MASATU
WhatsApp + 255 716 924136 / + 255 755 400128
EMAIL : japhetmasatu@gmail.com
Saturday, April 3, 2021
JIANDAE KILA SIKU KUKABILIANA NA CHANGAMOTO ILI UKOMAE KIAKILI NA KIHISIA.
Kitu kimoja ambacho watu wengi hatuandaliwi mapema kufahamu basi ni kuambiwa ukweli wa maisha. Ukweli wa maisha ni kuwa maisha yatakuwa na changamoto siku zote. Changamoto hizi hazitaondoka hata tukifanikiwa kwa baadhi ya mambo tutakayo. Tutakapofanikiwa basi tutakutana na muundo mwingine wa changamoto.
Unaweza kutamani maisha yasingekuwa na changamoto ili yawe mazuri, imara au maana. Ila ukiangalia kwa kina uwepo wa changamoto ndio uletao ladha nzuri ya maisha, ndio unaofanya uzalishe wabunifu, wagunduzi na wanafalsafa. Changamoto zimefanya turejee ndani yetu na tugundue tuna uwezo mkubwa ambao tunapotumia tunavuka na kutatua hali mbalimbali ambazo zinajitokeza tunapoendelea kuishi.
Usipokuwa imara kihisia katika zama tunazoishi basi matukio yanayoendelea kutokea maishani yatakudhoofisha, yatakunyima furaha na yakufanya uishi na wasiwasi wakati wote. Ukomavu wa kihisia ni uwezo wa namna usivyoweza kutetereka na chochote kinachotokea maana unakuwa umejiandaa kuwa hata mabaya ni sehemu ya maisha, magumu ni njia ya maisha na changamoto ni fursa ya kukua na kukomaa. Watu wengi wasojiandaa kwa lolote kutokea ni rahisi hisia zao kuumizwa.
Kadri unavyoweza kukabiliana na changamoto na kuzivuka ndani yako unajenga utulivu, nguvu, uimara na ukomavu. Mtu ambaye anapitia changamoto nyingi ni mtu aliye imara kuliko mtu ambaye hapitii magumu au changamoto zozote. Uzuri wa changamoto ni kuwa unamsaidia mtu kutumia akili, kustahimili na kujituma ili avuke hapo. Kupitia mchakato wote wa kukabiliana na changamoto basi mtu anajenga uzoefu, hekima, ujuzi na uimara wa kukabiliana na changamoto nyingine mpya.
Simama imara katika wakati ambao maisha yatakutana na changamoto. Huu ni wakati ambao unapaswa kuwa tayari kukabiliana na changamoto ili zikusaidie ukomae, ukue na uwe imara zaidi kwa ajili ya changamoto nyingine mpya zitakazojitokeza maishani.
NA KOCHA MWL. JAPHET MASATU , DAR ES SALAAM
WhatsApp + 255 716 924136 / + 255 755 400128