Tuesday, June 1, 2021

KILA TATIZO HATA LIWE KUBWA KIASI GANI LITAPITA TU NA KUSAHAU VUTA TU SUBIRA.

Maisha hupokezana kwa mambo nayo huja na kupita. Yote haya yanakuja ili kutupima na kutufungua akili ilivyo wazi kuwa hakuna jambo zito kubwa kuliko lingine. Mambo mazito tunayapa majina pale ambapo hatuoni njia namna gani tuweze kutoka au kupata suluhisho.

Suluhisho ni njia ambayo jambo lilokuwa likionekana ni zito na gumu kuwa jepesi. Ugumu wa maisha ni pale ambapo tunakutana na nyakati ambazo mbele yetu hatuoni njia, hatuoni nafasi ya kushinda au hatuoni upenyo wa kupita. Magumu huja kutufundisha kuna njia nyingi unazoweza kuzitumia kupita gumu lolote linapojitokeza.

Nyakati ngumu zinazojitokeza mara kwa mara katika maisha yetu haziji kutudumaza bali kutuchangamsha akili tufikiri zaidi, tujichunguze na kutafakari namna ya kuvuka. Changamoto zinapojitokeza hazituachi namna tulivyo awali bali zinatuimarisha na kujigundua kuwa tuna uwezo mkubwa zaidi wa kuvuka vikwazo na kilichokuwa kinatukwamisha ni kihunzi kidogo cha kuruka tu.

Mtu ambaye mara kwa mara anakutana na changamoto na kuzishinda anajitengenezea uimara na uzoefu unaompa nafasi ya kukabiliana na jambo lolote linaloweza kujitokeza katika safari ya maisha. Wale ambao huwa tunawaona wamefanikiwa kwa kitu fulani iwe ni biashara, uongozi, elimu na mahusiano basi moja kwa moja utakuta wamekuwa ni washindi wa changamoto nyingi ambazo zimewakuta.

Changamoto zinazompata mtu zinaweza kuzaliwa katika ugeni wa mambo kunakoweza kuchangiwa na uhafifu wa maarifa, uzoefu na utambuzi. Changamoto zinaumiza pale ambapo mtu anakutana na uhalisia unaovunja kuona kwake kitu katika hali alofikiria ingekuwa hivyo. Hili limepelekea changamoto ziwaangushe wengine, waanguke katika walichokianzisha na kufeli kabisa katika hatua ambazo walikusudia wangeweza kuvuka.

Muda hutusaidia kupisha changamoto ambazo huwa tunapitia. Ukitulia na kufikiria maisha yako utaona kuna nyakati ambazo uliwahi pitia changamoto nyingi na ukafikiria huenda zingekumaliza au zisingeisha na kupita. Ila muda ukazipitisha na kuzigeuza leo yawe mafunzo na kukufanya uwe imara zaidi. Hili ndivyo linavyotokea katika maisha kuwa kila kitu ambacho unakiona ni kizito si kizito kiuhalisia kitakuwa chepesi kadri muda unavyopita na kukivunja vunja kiwe hakina nguvu tena kama ya awali.

Ndimi  Rafiki   yako 

KOCHA   MWL.  JAPHET   MASATU , DAR  ES  SALAAM , TANZANIA

WhatsApp + 255 716924136  /  + 255 755 400128

 

No comments:

Post a Comment