Rafiki yangu mpendwa,
Kila
ninapopata nafasi ya kushauri au kutoa mafunzo kwa wafanyabiashara,
huwa nawauliza kama wanajua dhumuni na malengo ya biashara zao.
Majibu ambayo huwa napata yanaonesha wazi kwamba wengi hawajui tofauti ya dhumuni na lengo la biashara zao.
Wengi hujiona wapo kwenye biashara ili wapate faida.
Ni fikra na mtazamo huo ndiyo vimekuwa kikwazo kwa ukuaji wa biashara zao. Kama biashara inachoangalia ni kuingiza faida pekee, lazima itapoteza wateja kwa kiasi kikubwa sana.
Dhumuni
la biashara linapaswa kuwa ni kutengeneza na kutunza wateja. Lakini
lengo kubwa la biashara linapaswa kuwa kutengeneza faida. Ni kupitia
wateja ndiyo biashara inaweza kuingiza faida.
Hivyo kwa kuanza na wateja, biashara itakuwa kwenye nafasi nzuri ya kutengeneza faida nzuri.
Biashara nyingi huwa zinashindwa kwa sababu hazina wateja wa kutosha kuziwezesha kujiendesha kwa faida. Kwenye makala ya leo ya ushauri wa changamoto tunakwenda kujifunza jinsi ya kutengeneza na kutunza wateja kwenye biashara na iweze kufanikiwa.
Wasomaji wenzetu waliotuandikia kuomba ushauri kwenye hili walikuwa na haya ya kusema;
“Biashara yangu inapoteza wateja kila siku haikui zaidi ya kumaliza pesa zangu za kubrandy nimefungua Min Juice bar huduma na bidhaa tunazozalisha ni nzuri na bora sana lakini tatizo ni nini?” – Victor V. G.
“Sehemu nilipo weka biashara sio chumba cha njee ni ngum kufikiwa na wateja nifanye nini ili niweze kufikiwa na wateja na kujulikana pande zote” – Laban H.
Changamoto hizo mbili linamlenga mteja, moja kupata mteja na ya pili kumtunza asipotee. Tutayajadili haya mawili kwa kina.
Kupata wateja wa biashara.
Ili kupata wateja kwenye biashara yako, lazima kwanza uchague ni wateja wa aina gani unaowalenga, lazima ujue sifa zao kabisa.
Kwa bidhaa au huduma unayouza, jua ni watu gani unaowalenga na jua sifa zao muhimu.
Jua matatizo au mahitaji waliyonayo ambayo biashara yako inatatua.
Jua uwezo wao wa kuweza kumudu gharama ya unachouza.
Jua wanakopatikana na njia gani ya kuweza kuwafikia.
Ukishazijua sifa za wateja wa biashara yako, usiwasubiri waje kwenye biashara, bali wafuate kule walipo.
Uzuri wa zama hizi siyo lazima biashara yako iwe eneo linaloonekana ndiyo ipate wateja.
Kwa kuwa na mkakati mzuri wa masoko unaweza kuwafikia wateja kule waliko, iwe ni ana kwa ana au kwa mawasiliano.
Usifanye biashara kizamani kusubiri waje, bali toka na watafute wateja.
Tayari
umeshajua matatizo au mahitaji yao na tayari una suluhisho linalowafaa,
ni wewe kuwafikia na kuhakikisha wanajua uwepo wa biashara yako na
kushawishika kuja kwenye biashara yako.
Baada ya kuwashawishi wateja na wakaja kwenye biashara yako, unapaswa kuwashawishi wanunue.
Usiwakubalie kirahisi pale wateja wanapokuambua wameshaona na watakuja siku nyingine kununua, hapo wanakukimbia kirahisi.
Washawishi wanunue kwa kuwahakikishia kwamba hawatapoteza fedha zao wanapofanya maamuzi ya kununua.
Kumbuka
wateja wako wametafuta fedha zao kwa maumivu na hawapo tayari kutengana
nazo kirahisi. Lazima uwape uhakika kwamba wakitumia fedha zao kwenye
biashara yako yatakuwa ni matumizi bora kuliko mengine wanayoweza
kufanya kwa fedha hizo.
Mjue mteja, mfikie mteja na kumshawishi kuja kwenye biashara na anapofika mshawishi anunue, hizo ni hatua tatu kubwa za kupata wateja kwenye biashara yako.
Kutunza wateja wa biashara wasipotee.
Kama
mteja hajanunua kwenye biashara yako, huyo siyo mteja wako. Hata kama
amekuahudi atanunua, kama bado hajanunua, usimhesabie ni mteja.
Mteja akishanunua kwako mara moja, ni rahisi kununua tena kwa mara nyingibe kulimo kwa mteja ambaye hajanunua kabisa.
Mteja ambaye ameshanunua, kuna imani ambayo tayari ameshaijenga kwenye biashara.
Wanapokosea
wafanyabiashara wengi ni kuhangaika kukimbizana na wateja wapya huku
wakiwasahau kabisa wateja ambao tayari walishanunua.
Hii ni sawa na kuacha dhahabu ya uhakika uliyonayo ndani na kwenda kuhangaika kutafuta dhahabu sehemu ambayo huna uhakika nayo.
Sisemi
uache kutafuta wateja wapya, ila ninachosema ni juhudi unazoweka
kutafuta wateja wapya, weka juhudi za kiwango hicho hicho kuwatunza
wateja ambao tayari wameshanunua.
Kuwatunza wateja ambao wameshanunua kwako, zingatia haya muhimu.
Moja
ni kuwapatia huduma bora kabisa kwenye biashara yako. Wape wateja wako
huduma bora ambazo hawawezi kuzipata sehemu nyingine yoyote. Hilo
litawasukuma kurudi tena kwako kwa sababu wanajua watapata ambacho
hawawezi kupata pengine.
Kama hakuna tofauti ya wanachopata kwako na wanachopata kwa wengine, hawatajisumbua kurudi tena kwako.
Mbili
ni kuendelea kuwasiliana nao mara kwa mara. Kila mteja ambaye
ameshanunua kwako, hakikisha unakuwa na mawasiliano yake. Uzuri kila mtu
ana njia mbalimbali za mawasiliano, kuanzia namba za simu, barua pepe
na mitandao ya kijamii.
Mteja akishanunua kwako hawezi kuwa mgumu
kutoa mawasiliano yake, hivyo muombe akupe mawasiliano hayo na yatumie
kuwasiliana naye.
Siyo tu unatumia kumtangazia biashara yako, bali
kumjulia hali, kumtumia salamu mbalimbali kulingana na sikukuu au
matukio mbalimbali.
Kadiri unavyowasiliana na wateja wako, ndivyo wanavyokufikiria wewe na biashara yako na kuja kwako pale wanapokuwa na uhitaji.
Tatu
ni waombe wakuletee wateja zaidi. Kama mteja ameridhika na huduma
unazompa, na hilo utalijua kwa shuhuda atakazokupa yeye mwenyewe, muombe
awaalike watu wake wa karibu nao waje kupata huduma hizo.
Mteja anapochukua hatua ya kuwaalika wengine, yeye mwenyewe ataendelea kuja maana hawezi kuwaleta watu halafu yeye asije.
Kwa kumshawishi na akakubali kuleta wateja zaidi, anakuwa amechagua kuendelea kuwa mteja wako kwa muda mrefu zaidi.
Na
mteja anapokuletea wateja zaidi, hakikisha unawapa huduma bora kabisa
ili asipoteze imani yake kwa wale aliowashawishi kuja kwenye biashara
yako.
Utoaji wa huduma bora na za kipekee, mawasiliano ya mara kwa mara na wateja kukuletea wateja zaidi ni njia bora za kuwafanya wateja kuendelea kuwa kwenye biashara yako.
Kama
mfanyabiashara jua dhumuni na lengo la biashara na weka juhudi kubwa
kwenye kutafuta wateja wapya wa biashara yako, na juhudi za aina hiyo
pia kwenye kuwatunza wateja ambao tayari wameshanunua.
Kwa namna hiyo biashara itakuwa na wateja wengi na kuweza kuingiza faida nzuri.
Let me welcome to my website
ReplyDeleteaomlasthope