Saturday, June 12, 2021

TUJIFUNZE KUVAA VIATU VYA WENGINE KILA TUNAPOFANYA AU KUSEMA JAMBO.

Sisi binadamu huwa tuna hulka ya kutowafikiria wengine bali kujijali wenyewe tu na wanabinafsi wa hisia zetu. Hili limechangia migogoro mingi katika maisha ya watu iwe ni katika kuishi na watu, kuwaongoza watu au mahusiano. Binadamu wote ni sawa katika mjengo wa mwili kuwa wote wanapata maumivu katika kuumia kama wengine. Hakuna binadamu ambaye mwili wake hauna damu au nyama. Wote ni sawa na hili linafanya hata kufa tutakufa binadamu wote mbali na tofauti zetu za kirika, kikabila, kitaifa au kirangi.

Chuki na unyama ambao huwa unajitokeza katika jamii zetu ni zao la watu kutojali hisia za watu wengine na hawajui namna wanavyoweza kuvaa hivyo viatu. Inawezekana ni tukio la maonevu katika jamii, mauaji au utesaji ila wasijue namna hata na wao wanaweza kupitia hali hizo au kufanyiwa hivyo na huenda wakaumia kama wanavyowasababishia wengine maumivu au uchungu. Kuwatendea wengine yaweza kuwa ni rahisi pale ambapo mtu hajali namna wengine watakavyoumizwa na hayo.

Binadamu pia tuna hisia za furaha na huzuni. Pale mambo mabaya yanapojitokeza huwa tunaumia kihisia, tunapata majonzi, tunapata taabu katika kukabiliana nayo. Mabaya haya si kuwa yanafanywa na wanyama isipokuwa ni binadamu wenzetu ambao kwa namna moja wana watu wanaowazunguka, wenye hisia kama wengine na wenye miili kama wengine. Kutenda ubaya tu na kisha kuacha kama mtu hajaona ubaya alotenda ni kuzalisha machungu kwa wengine ambao nao huwezi jua ni kwa namna gani hujipanga kuachilia au ulipizaji wa kisasi.

Ni rahisi kutusi wengine, rahisi kutotenda haki kwa wengine na ni rahisi kutojali wengine katika makubaliano fulani. Utakuta ni hali ya kawaida katika jamii zetu huwa tunapanga muda fulani wa jambo kufanyika ila watu hatuendi hivyo na wakati mwingine hata bila kutoa sababu za msingi. Watu wanaozingatia huwahi kufika na kukaa sana wakisubiri wengine. Hatujui ni kwa namna gani hukwazika na hilo jambo, lakini utakuta huwa hatujali hilo kuwa namna wengine watajisikia kwa kuchelewa kwetu. Huenda tunafanya hivyo sababu hatujawahi kuvaa viatu vyao kuwa vipi ukiwahi sehemu ukaachwa ukingoja masaa mengi au pengine hata mtu anakuja kukuambia haji licha umesubiri masaa mengi.

Tunaumizwa na mambo mengi katika kuishi kwetu kwa kuwa na watu ambao hawajajifunza au hatujajifunza kuvaa viatu vya watu wengine. Kwa kukosa kujua kuvaa viatu vya wengine tumekuwa ni watu wepesi kuhukumu, kuwasema wengine na kuchukulia wengine wana mioyo migumu na si laini kama wengine. Hili linaumiza jamii nyingi na kuendelea kuzalisha watu wenye mioyo ya kikatili, visasi, chuki na wasio na upendo kwa wanaowazunguka. Ila falsafa inatualika sote kuanza kujifunza kuvaa viatu vya wengine kila tunapofanya jambo au kusema jambo. Tuangalie je ingekuwa ni upande watu tungelipokeaje au kulichukulia.  

KARIBU  UJIUNGE " DARASA   ONLINE "

KOCHA  MWL.  JAPHET  MASATU , DAR  ES  SALAAM

WhatsApps  + 255  716924136 /    + 255 755 400128 /  + 255 688 361539

EMAIL : japhetmasatu@gmail.com

No comments:

Post a Comment