WATANZANIA wamepokea kwa huzuni
kubwa habari kuhusu ajali iliyoua wenzao 36 kule Butiama, Mara, na wengine
wapatao 76 wakijeruhiwa, wengine vibaya sana.
Ni huzuni ya Taifa. Nachukua fursa
hii kuwapa pole wafiwa na kuwatakia waliojeruhiwa kila la heri wapone haraka.
Hata hivyo, ajali ya Butiama ni
kengele nyingine ya hatari tunayopigiwa. Zipigwe kengele ngapi za hatari ili
tuamke na kuanza kuchukua hatua madhubuti?
Hatupaswi kuishia kwenye kuomboleza
tu na kumwachia Mungu. Tuna wajibu wa kuchukua hatua.
Tunajua, kuwa nyingi ya ajali za
barabarani zinatokana na uzembe wa madereva ikiwamo ulevi; kwamba madereva
wanaendesha wakiwa wamelewa. Kuna wanaokunywa viroba, wenye kuvuta bangi na
hata kumung'unya kubeli. Ni hawa tuliowaachia dhamana ya kuendesha malori na
mabasi yenye abiria 65 na zaidi.
Na tuwe na maswali ya msingi ya
kujiuliza; Hivi madereva wetu wa malori na mabasi wanapatikana vipi? Kwamba
mafunzo yao wanayapata wapi? Kwanini hatuna idara ya Serikali yenye
kuthibitisha leseni zao ikiwamo mafunzo waliyoyapata?
Hakika kuna maswali mengi yenye
kuhitaji majibu kutoka kwetu wenyewe. Kwamba tunahitaji kongamano la kitaifa
kujadili ajali za barabarani na njia ya kuzipunguza. Maana, kubaki kuomboleza
na kutochukua hatua madhubuti kupambana na hali hii kunatuacha kila mmoja wetu
kuwa kwenye hatari ya kuathirika na ajali za barabarani kwa njia moja au
nyingine. Na tuchukue hatua, SASA.
Nimepata kuandika haya huko nyuma,
lakini nayarudia hapa kutokana na umuhimu wake kwa kuzingatia kilichotokea
Butiama.
Ajali, na hususan, ajali za
barabarani imekuwa ni janga kwa nchi yetu. Kwa mujibu wa ripoti iliyotoka miaka
michache iliyopita, Mtafiti wa usalama barabarani (public transport and safety)
katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam T. Rwebangira , asilimia 76 ya ajali nyingi
zinazohusisha mabasi ya abiria zinatokana na mambo ya kibinadamu, asilimia 17
zinatokana na magari yenyewe na asilimia 7 ni sababu nyingine zisizoweza
kuzuilika.
Hizo asilimia 17 zinabainisha kuwa
vyombo vingi vya usafiri ikiwamo mabasi mengi tunayotumia hapa Tanzania ni
mabovu na usalama wake si thabiti kwa lengo la kusafirisha abiria.
Tuangalie basi hizi asilimia 76 ya
sababu za kibinadamu zinazosababisha ajali nyingi hapa Tanzania.
Mtafiti Rwebangira alibaini
kwamba kila mwaka Tanzania inapoteza zaidi ya shilingi bilioni 20 kutokana na
ajali mbalimbali za barabarani.
Vyanzo na tafiti mbalimbali
vinaainisha kwamba asilimia zaidi ya 78 ya waathirika wa ajali za barabarani ni
abiria na watembea kwa miguu.
Kiundani takwimu za kuanzia miaka ya
2000 zinaonyesha asilimia zaidi ya 40 ya wanaokufa kwenye ajali za barabarani
ni abiria na zaidi ya asilimia 38 ni watembea kwa miguu.
Takwimu hizo hizo kutoka vyanzo
mbalimbali zinaonyesha viini vya ajali za barabarani ambavyo ni uendeshaji wa
hatari/uzembe zaidi ya asilimia 54, ubovu wa magari zaidi ya asilimia 16,
uzembe wa watembea kwa miguu zaidi ya asilimia 6.8, mwendo kasi zaidi ya
asilimia 3, uzembe wa wapanda pikipiki zaidi ya asilimia 3, uzembe wa wapanda
baisikeli, zaidi ya asilimia 6, ulevi, zaidi ya asilimia 1.2 na mengineyo kama
vile utelezi na ukungu husababisha zaidi ya asilimia 6 za ajali barabarani.
Hivyo basi, zaidi ya asilimia 94 ya
ajali za barabrani zinaweza kuzuilika na jamii yenyewe.
Tukiangalia sababu za ajali nyingi
za barabarani utakuta nyingi zinahusiana sana na uzembe na kutokuwa makini.
Sababu kubwa ya kwanza ni ulevi wa
aina zote wa madereva na abiria.
Wakati fulani nikiwa nasafiri, moja
ya sifa alizokuwa anapewa dereva wa basi nililopanda na lililokuwa likienda kwa
kasi ni kuendesha akiwa na mzinga wa konyagi nyuma ya kiti chake. Akifika
mwisho wa safari chupa hiyo ya konyagi huwa haina kilichobaki. Eti hii pia ni
sifa! Jamii nzima inapaswa kupiga vita tabia za kilevi za madereva wetu.
Sababu nyingine ni mwendo kasi
unaoendana na kutojali sheria na alama za barabarani. Tunajua, kwamba madereva
wetu wengine wanaendesha wamelewa. Tunawaacha wakimbize basi wanavyotaka.
Tujiulize, je, dereva huyu
aliyekunywa pombe kabla ya kuanza kuendesha gari anaweza kuwa na maarifa yake
ya kawaida na uwezo wake wa kawaida kumudu kasi ya mwendo wa gari? Je, atakuwa
makini na kutumia akili yake yote kwenye chombo anachokiendesha?
Siku hizi utakuta dereva anakwenda
spidi ya kilomita 150 kwa saa halafu anazungumza kwenye simu. Kuzungumza kwenye
simu za mikononi hakufai kabisa kwa dereva wa gari la abiria aendeshapo gari.
Hii ni hatari kwa abiria na watu wengine watembeao kwa miguu. Tunalitia hasara
kubwa taifa na familia zetu kwa mambo tunayonaweza kuyazuia bila gharama
yoyote.
Mabasi mengine utakuta yamepakia
abiria na mizigo kupita kiasi. Hatari iliyopo ni basi kushindwa kupita kwenye
baadhi ya madaraja na kusababisha ajali mbaya.
Tuangalie sheria Namba 30 ya Mwaka
1973 na marekebisho yake ya mwaka 1996 inayohusu ni jinsi gani magari
yanatakiwa yawe yakiwa barabarani.
Tatizo letu si dereva wala abiria
kama wanasoma sheria za barabarani.
Suala la ubovu wa magari nao ni
sababu mojawapo ya ajali nyingi za barabarani. Kuna rafiki yangu aliyenusurika
kufa katika milima ya Kitonga kwa sababu basi alilopanda lenye abiria zaidi ya
65 lilikuwa halina breki. Tujiulize, je, inawezakanaje gari bovu liruhusiwe
kuwa barabarani? Kwa kutumia gari bovu hatulidanganyi jeshi la polisi bali
tunajidanganya sisi wenyewe.
Kumekuwa na sababu nyingine nyingi
kama vile watu wanaondesha magari kwa sababu wana magari lakini si madereva,
kuacha nafasi ndogo kati ya gari na gari, uzoefu mdogo wa barabara na zaidi ya
yote ni dereva na hasa dereva wa mabasi anapaswa kupumzika vya kutosha.
Tafiti zinaonyesha, kwamba dereva
anapaswa kupumzika kila baada ya saa mbili za kuendesha kwa mfululizo. Na
tafiti nyingine zinaonyesha dereva anapaswa kuendesha gari kati ya saa tatu
hadi nne.
Lakini kwa vyovyote vile, dereva
hapaswi kuendesha gari zaidi ya saa nne bila kupumzika. Dereva hapaswi
kulazimishwa safari, dereva anapaswa kula chakula kizuri kinachofaa, anapaswa
kulala sehemu nzuri na yenye ubora, na apewe maslahi bora.
Haiwezekani hujui dereva amelala
wapi ukaruhusu aendeshe gari la abiria. Unajuaje kama alikwenda kulala saa 9
usiku au hakulala kabisa.
Tukumbuke, kwamba ajali hizi
zinachukua nguvu kazi kubwa ya nchi yetu. Na mbaya zaidi baadhi ya watu
wanachukuliwa na ajali za barabarani ni viongozi bora kabisa.
Kwa pamoja, twapaswa kuchukua hatua
katika hili na kupunguza gharama na mzigo kwa Serikali na familia zetu. Mzigo
usiokuwa wa lazima kutokana na ajali za barabarani zinazoweza kuzuilika.
Nahitimisha.
NA MAGGID MJENGWA, 10 SEPT 2014 , GAZETI LA RAIA MWEMA ,