Showing posts with label ELIMU YA BIASHARA. Show all posts
Showing posts with label ELIMU YA BIASHARA. Show all posts

Monday, July 15, 2019

NJIA PEKEE YA KUJIHAKIKISHA USALAMA KWENYE KAZI AU BIASHARA YAKO.

“In today’s competitive economy, it’s not enough to simply do your job well. Developing a reputation as an expert in your field attracts people who want to hire you, do business with you and your company, and spread your ideas. It’s the ultimate form of career insurance.” ― Dorie Clark
Wakati mapinduzi ya viwanda yanaanza, watu waliambiwa ili kuwa na usalama wa kazi basi soma kwa bidii, faulu sana na utapata kazi nzuri ambayo utaifanya mpaka kustaafu kwako na hapo utalipwa mafao ya kukuwezesha kuishi mpaka uzeeni.
Mapinduzi ya viwanda yamefika tamati na sasa tupo kwenye mapinduzi ya taarifa. Katika zama hizi uhakika pekee wa wewe kuwa na usalama kwenye kazi au biashara siyo tu elimu au taaluma uliyonayo, bali kutengeneza ubobezi kwenye kile unachofanya kiasi kwamba watu watapenda kufanya kazi na wewe.
Unapaswa kujijengea sifa ya ubobezi wa hali ya juu kwenye kile unachofanya kiasi kwamba kila mwenye uhitaji unaohusu unachofanya anakufikiria wewe au anaambiwa waje kwako.
Na hilo linawezekana kama utaweka juhudi katika kujua vizuri kile unachofanya, kukifanya vizuri na pia kutengeneza mtandao wa watu wanaojua kuhusu unachofanya na hivyo kusambaza sifa zako kwa wengine wengi.

Monday, July 1, 2019

VIPANDE VIKUU VINNE VYA BIASHARA YENYE MAFANIKIO.

(1). WATEJA.
Wateja ndiyo kipande cha kwanza muhimu sana cha biashara yako. Kama hakuna wateja basi hakuna biashara. Lazima uchague biashara yako inakwenda kuwahudumia watu gani, wanaopatikana wapi na unawafikiaje. Biashara lazima ijenge wateja ambao wanaotegemea kwa kile inachofanya.

Unapoingia kwenye biashara anza na kitu ambacho tayari watu wanajihitaji, hivyo wewe unakuja na suluhisho na kuhakikisha watu wanajua uwepo wako kwenye biashara hiyo. Hivi ndivyo unavyoweza kutengeneza wateja wa biashara yako.

(2).  MAHITAJI  YA  WATEJA.

Ukishachagua aina ya wateja ambao biashara yako inawahudumia, unapaswa kujua yale mahitaji yao ya msingi. Yale mahitaji yanayowasukuma kununua kile ambacho wewe unauza. Ukishayajua mahitaji hayo, jipange kuyatimiza kwa namna ambayo hakuna mfanyabiashara mwingine anayeweza kuyatimiza hivyo.

Kuna vitu viwili muhimu sana unapaswa kujua kuhusu mahitaji ya wateja wako, hofu na tamaa. Wateja wa biashara yako wanafanya maamuzi kwa kutumia hisia hizo mbili, labda wana tamaa ya kupata kitu fulani au wana hofu ya kupoteza kitu fulani. Jua hisia hizo mbili za wateja na zitumie katika mauzo.

(3). NAFASI  YAKO  KATIKA  SOKO.

Biashara yoyote unayofanya, kuna nafasi ambayo upo kwenye soko, unaweza kuwa ndiyo namba moja yaani wateja wanakufikiria wewe kwanza au ukawa haupo kwenye namba za juu, yaani wateja hawakufikirii kabisa. Ili kukuza biashara yako, unapaswa kuwa kwenye nafasi ya juu kwenye soko lako. Unapaswa kuwafanya wateja wako wakufikirie wewe kwanza inapokuja kwenye mahitaji yao.

Matangazo, alama za kibiashara, rangi za kibiashara, kauli mbiu na hata utamaduni wa tofauti wa biashara yako ni vitu vinavyowafanya wateja wakukumbuke na kukufikiria muda mrefu. Tengeneza picha ya tofauti ya biashara yako ambayo inawafanya wateja wakufikirie wewe mara zote.

(4). UBOBEZI  WA   BIASHARA   YAKO.

Je biashara yako imebobea kwenye nini? Biashara yako inajulikana kwa kipi? Je ni kitu gani wateja wanapata kwako ambacho hawawezi kupata kwa wafanyabiashara wengine?

Hayo ni maswali muhimu ya kupima ubobezi wa biashara yako. Biashara iliyobobea kwenye kile inachofanya ndiyo biashara ambayo inapata mafanikio makubwa sana.

Jua ni aina gani ya biashara unayofanya, na kipi cha tofauti unachotoa kwa wateja wako kisha kazana kutoa kitu hicho kwa namna ambayo wateja hawawezi kupata sehemu nyingine na utaweza kufanikiwa sana kwenye biashara unayofanya. Bobea kwenye vitu vichache na hilo litakufanya kinara kuliko kung’ang’ana kufanya vitu vingi.

Sunday, June 30, 2019

ASILI YA BIASHARA NI KUKUA NA KUFA.

Biashara ni kiumbe hai. Inatungwa, inazaliwa, inakua, inafikia makamo na kisha kufa. Hivi ndivyo mifumo yote ya maisha inavyokwenda. Kuanzia kwetu sisi binadamu, kabla hujazaliwa mimba inatungwa, anazaliwa mtoto, anakua, anafikia makamo na kisha anakufa.
Katika mfumo huu wa ukuaji wa biashara, utungwaji wa mimba ya biashara ni yale mawazo ya kuanza biashara ambayo mtu anakuwa nayo. Kisha kuanza kwa biashara ni sawa na mtoto anayezaliwa, kukua na kisha kufa. Sasa kama ilivyo kwenye asili, siyo mimba zote zinazotungwa zinazaliwa, nyingine zinaharibika kabla ya kufikia kuzaliwa. Na hata watoto wadogo wanaozaliwa, wengi hawafiki utu uzima, wanakufa kabla. Na wachache wanafika utu uzima na kufa.
Kwenye biashara, biashara nyingi huwa zinashindwa kabla hata ya kuanza, nyingi zinaishia kwenye mawazo pekee. Kwa zile ambazo zinaanza, nyingi huwa zinakufa kwenye uchanga, hazikui kufikia ukomavu. Na zile ambazo zinakua, huwa zinafikia ukomavu na kufa.
Lakini zipo biashara chache sana ambazo zimeweza kuondoka kwenye mfumo huo wa ukuaji na kufa. Biashara hizi zimekuwa zinajua kinachopelekea biashara kufa baada ya kukomaa ni bidhaa au huduma kuzoelekea na kutokuwa na kitu kipya.
Ili kuondokana na hali hiyo ya biashara kufika ukingoni na kufa, wafanyabiashara hao ambao biashara zao hazifi, wamekuwa wanakuja na bidhaa mpya au huduma mpya kila mara ambapo bidhaa au huduma ya zamani imefikia kilele chake cha mauzo. Hawasubiri mpaka mauzo yaanze kupungua na biashara kufa. Badala yake wanakuja na bidhaa au huduma mpya inayowafanya waendelee kuwa sokoni.
Huu ndiyo mfumo unaotumiwa na makampuni makubwa ya teknolojia, chukulia mfano wa kampuni ya Apple ambayo inazalisha simu aina ya Iphone. Kila mwaka huwa wanakuja na toleo jipya la simu zao, ambalo halitofautiani sana na toleo lililopita. Yote hii ni kuhakikisha kwamba wanaendelea kuwa sokoni. Kwa sababu kampuni ikishatoa toleo jipya, na watu wote wakawa nalo, hakuna tena fursa ya ukuaji. Lakini wanapokuja na toleo jipya, wale waliokuwa na toleo la zamani wanatamani kuwa na toleo jipya na hapo mauzo yanaanza upya.
Kwa biashara unayofanya, angalia jinsi unavyoweza kutumia njia hiyo ya kuwa na toleo jipya la bidhaa au huduma kila wakati ili biashara yako isife.

Thursday, June 27, 2019

MAHUSIANO NI MUHIMU KULIKO BIDHAA KATIKA BIASHARA

  1. Ipo njia moja ya kupata chochote unachotaka na njia hiyo ni kuomba. Ombeni na mtapewa ni siri muhimu ya mafanikio kwenye biashara. Kama kuna kitu unataka, omba, na wengine watakuwa tayari kukupa. Huwezi kupata kitu bila kuomba.
  2. Unapoomba kazi, badala ya kutuma maombi kama wengine wanavyofanya, tafuta mikutano na wahusika wa eneo unalotaka kufanya kazi. Kwa kutumia mtandao wa kijamii wa LinkedIn, unaweza kukutana na mtu yeyote na ukaongeza nafasi zako za kupata kazi unayotaka.
  3. Biashara ni watu, haijalishi unajua nini, bali unamjua nani na nani anakujua wewe. Hivyo kazana kukuza zaidi mtandao wako wa watu unaowajua na wanaokujua.
  4. Mchukulie kila mtu unayekutana naye kama mtu mashuhuri, jua ni mtu muhimu, muoneshe umuhimu na watu watapenda kukutana na wewe. Ili kufanikiwa kwenye biashara unahitaji kutengeneza marafiki wengi.
  5. Kutana na watu, furahia na jifunze. Weka kipaumbele chako katika kujenga mahusiano imara kwenye biashara yako na kazi yako, fanya kile ambacho unapenda ukiwa umezungukwa na watu unaowapenda. Pia jifunze kupitia wale ambao unafanya nao kazi na wanaokuzunguka.
  6. Kuwa mtu wa shukrani, kila unapokutana na mtu, au mtu anapokufanyia kazi, chukua muda wa kumwandikia ujumbe wa shukrani, inaimarisha zaidi mahusiano yako.
  7. Wale uliosoma nao shule moja au chuo kimoja ni watu muhimu sana kwenye mafanikio yako. Kuwa nao karibu na tengenezeni mahusiano bora, kila mtu anaweza kunufaika kupitia kazi za wengine. Kama hakuna umoja wa wale mliosoma pamoja, una fursa nzuri ya kuuanzisha.
  8. Wafuatilie watu baada ya kukutana nao. Unapokutana na kujuana na mtu mara ya kwanza, endelea kuwafuatilia kwa mawasiliano, hili linaimarisha mahusiano mnayokuwa mmeanzisha.

Tuesday, June 25, 2019

SABABU TANO ( 5 ) ZINAZOUA BIASHARA NYINGI KUKUA

(1). MMILIKI  WA  BIASHARA.
Mmiliki wa biashara ni kikwazo cha kwanza kabisa kwenye ukuaji wa biashara. Pale ambapo biashara inamtegemea mmiliki wa biashara hiyo kwenye kila kitu haiwezi kukua. Kama mwanzilishi wa biashara ndiye anayetegemewa kufanya kila kitu kwenye biashara, biashara haiwezi kukua.
Ili biashara kukua lazima mmiliki aweze kujitofautisha na kujitenganisha na biashara hiyo. Ajenge biashara ambayo inaweza kujiendesha yenyewe bila ya uwepo wake.

(2). KUKOSA  WATEJA  WAPYA.
Biashara inakua kwa kutengeneza wateja wapya kila wakati. Biashara nyingi zimekuwa hazina mfumo mzuri wa kutengeneza wateja wapya kila wakati. Hivyo wanaendelea kuwa na wateja wale wale na hilo linakuwa kikwazo kikubwa kwenye ukuaji.
Ili biashara ikue lazima iwe inatengeneza wateja wapya kila wakati. Wateja wapya ndiyo wanaoleta ukuaji wa biashara.

 ( 3 ). KUKOSA   WAFANYAKAZI  BORA.
Wafanyakazi wa biashara ndiyo wanaoweza kuikuza au kuiangusha. Biashara nyingi hazina wafanyakazi sahihi na hilo limekuwa linazizuia biashara hizo kukua.
Wafanyabiashara wengi hawana mfumo mzuri wa kuajiri watu sahihi kwenye biashara zao na hilo limekuwa linawagharimu kwenye ukuaji. Ili biashara ikue, inahitaji kuwa na wafanyakazi bora ambao wanaweza kutekeleza majukumu yao vizuri.

 ( 4 ). MZUNGUKO  HASI  WA   FEDHA.
Fedha ndiyo damu ya biashara, mzunguko wa fedha ukiwa vizuri biashara inakua, ukiwa vibaya biashara inakufa.
Biashara nyingi zinazokufa zina mzunguko hasi wa fedha, ikiwa na maana kwamba matumizi ya biashara ni makubwa kuliko mapato.
Ili biashara ikue, inahitaji kuwa na mfumo bora wa kudhibiti mzunguko wa fedha ili uwe chanya. Mapato yawe makubwa kuliko matumizi.

 ( 5 ). MAUZO  YASIYOTOSHELEZA.
Mauzo ndiyo injini au moyo wa biashara. Mauzo ndiyo yanayosukuma mzunguko wa fedha kwenye biashara. Bila ya mauzo hakuna biashara.
Biashara nyingi zimekuwa hazina mauzo ya kutosheleza kuzalisha mapato yanayoiwezesha biashara hiyo kujiendesha kwa faida.
Biashara hizo hazina mfumo bora wa masoko ambao unawezesha mauzo kuwa mazuri na yanayoiwezesha biashara kujiendesha yenyewe.
Rafiki, hizi ndizo sababu tano kubwa zinazozuia biashara nyingi kukua, ukizikabili sababu hizi tano, biashara yako itaweza kukua sana.

Saturday, June 22, 2019

KWANINI BIASHARA NYINGI HAZIFAI KUUZA ?

Biashara nyingi hazifai kuuza kwa sababu zinaendeshwa kwa vurugu. Kwa nje biashara inaweza kuonekana inakwenda vizuri, lakini kwa ndani mambo ni vurugu. Hakuna mpangilio wowote wala mfumo ambao unafuatwa. Kila kitu kinafanywa kwa namna ambavyo mtu anajisikia kufanya. Hakuna viwango vyovyote vinavyofanyiwa kazi.
Wateja wanaokuja kupata huduma kwenye biashara, hawaji kwa sababu ya biashara, bali wanakuja kwa sababu ya mtu. Na wengine wanasema wazi kwamba wanataka kuhudumiwa na fulani tu.
Wafanyabiashara wengi hufurahia pale wateja wanapotaka wahudumiwe na wao tu, wakiona ni wateja wanawaamini na kuwakubali sana. Lakini wasijue kama hicho ndiyo kifungo chao.
Huwezi kuuza biashara ambayo haiendeshwi kwa mfumo na kila kitu kinamtegemea mmiliki wa biashara hiyo.
Na biashara ya aina hii inakuwa mzigo kwa mmiliki na kumnyima uhuru.
Karibu tujifunze jinsi ya kutengeneza biashara inayokupa uhuru na unayoweza kuiuza muda wowote na hili litakuwezesha kuwa na biashara bora na isiyokutegemea kwa kila kitu. Na hata kama hutaki kuuza biashara yako, kitendo cha biashara kuweza kujiendesha yenyewe bila ya wewe kuwepo, utakuwa ushindi mkubwa sana kwako.

HATUA NANE (8 ) ZA KUTENGENEZA BIASHARA INAYOJIENDESHA YENYEWE NA UNAYOWEZA KUIUZA MUDA WOWOTE

Kutoka kwenye kitabu "BUILT TO SELL", mwandishi " John Warrillow " anatushirikisha hatua nane za kufuata katika kutengeneza biashara ambayo inaweza kujiendesha yenyewe bila ya kuwepo kwa mwanzilishi wa biashara hiyo na pia inaweza kuuzwa muda wowote.
(1). Chagua bidhaa au huduma yenye uwezo wa kukua.
Hatua ya kwanza kabisa kwenye kutengeneza biashara inayojiendesha yenyewe na unayoweza kuiuza ni kuchagua bidhaa au huduma ambayo ina uwezo wa kukua.
Bidhaa au huduma yenye uwezo wa kukua ina vigezo vitatu;
Moja, inafundishika. Ni rahisi kumfundisha mtu mwingine jinsi ya kufanya kitu hicho na akaelewa.
Mbili; ina thamani kwa mteja. Hivyo mteja anakuwa tayari kulipa bei ambayo umeiweka. Kama kitu kinapatikana kwa wengine, mteja ataenda kwenye bei rahisi. Lakini kama kinapatikana kwako tu na mteja anakihitaji kweli, atakuwa tayari kulipa bei uliyopanga.
Tatu; manunuzi ni ya kujirudia. Mteja anahitaji kuwa anarudia tena na tena kununua. Isiwe ni kitu ambacho mteja ananunua mara moja kwenye maisha yake.
Baada ya kuchagua bidhaa au huduma ambayo inafundishika, ina thamani na manunuzi yake ni ya kujirudia, unahitaji kukaa chini na kuandika mchakato mzima wa jinsi unavyofanya biashara yako. Kila kitu kinachohusika kwenye biashara kinapaswa kuandikwa kwa namna ambayo mtu mwingine anaweza kufundishwa na akaelewa na kufuata. Huu unakuwa ndiyo mwongozo mkuu wa ufanyaji wa biashara yako.
Baada ya kuwa na mwongozo, unapaswa kuipa jina bidhaa au huduma yako. Unaipa jina kuitofautisha na bidhaa au huduma nyingine, hivyo inakuwa ya kipekee kwa wateja wako. Kadiri bidhaa au huduma inavyokuwa ya tofauti na zinazopatikana sokoni, ndivyo inakuwa na thamani kubwa kwa wateja wako.
Baada ya kuwa na jina linaloitofautisha bidhaa au huduma yako, andika maelezo mafupi kuhusu bidhaa au huduma hiyo ambayo yanajumuisha faida zake na jinsi inavyotatua changamoto za wateja wako, na tumia maelezo hayo kwenye masoko.
Katika hatua hii ya kwanza unachagua bidhaa au huduma moja au chache ambao unaweza kuweka nguvu zako zote na ukawafikia wateja wengi na biashara kukua pia. Ukifanya hatua hii kwa bidhaa au huduma nyingi utashindwa.
(2). Tengeneza mzunguko chanya wa fedha kwenye biashara.
Mzunguko wa fedha ndiyo uhai wa biashara yako. Yeyote anayetaka kununua biashara yako, akishaangalia kama inajiendesha yenyewe, anakwenda kuangalia mzunguko wa fedha wa biashara hiyo.
Mzunguko wa fedha kwenye biashara unaweza kuwa chanya au hasi. Mzunguko unakuwa chanya pale mapato ni makubwa kuliko matumizi na hasi pale matumizi ni makubwa kuliko mapato.
Ili kutengeneza mzunguko chanya wa fedha kwenye biashara yako, bidhaa au huduma unayouza inapaswa kuwafanya wateja walipe kwanza kabla ya kuipata. Epuka kuendesha biashara ambayo mteja anapata bidhaa au huduma kwanza halafu analipa baadaye. Hii inaifanya biashara ikae muda mrefu bila ya fedha na hivyo kuwa na mzunguko hasi wa fedha.
Biashara inapokuwa na mzunguko chanya, yule anayetaka kuinunua atakulipa zaidi kwa sababu tayari biashara inazalisha, tofauti na biashara yenye mzunguko hasi ambayo inahitaji kupokea fedha nyingi ili kujiendesha.
(3 ). Ajiri timu ya mauzo.
Baada ya kutengeneza bidhaa au huduma ambayo utaiuza kwa wateja kulipa kabla ya kuipata, unahitaji kujiondoa kwenye kuiuza bidhaa au huduma hiyo. Na hapa ndipo unapohitaji timu ya mauzo, watu ambao wanaenda kuuza bidhaa au huduma kwa niaba yako.
Hii ni hatua muhimu sana ambayo wengi hukwama, unapouza bidhaa au huduma yako mwenyewe, unawafanya wateja wakutegemee wewe. Lakini unapokuwa na mfumo wa mauzo, ambao unaendeshwa na watu wa mauzo, wateja hawakutegemei wewe bali wanategemea mfumo wa biashara.
Kazi yako kama mjasiriamali ni kuuza kampuni yako, siyo kuuza bidhaa au huduma za kampuni hiyo. Ajiri na tengeneza timu bora ya mauzo na ipe mwongozo wa kuuza bidhaa au huduma yako na wewe utapata muda mwingi wa kuikuza zaidi kampuni yako.
Unapoajiri watu wa mauzo, ajiri ambao wana uzoefu wa kuuza bidhaa na epuka sana watu ambao wana uzoefu wa kuuza huduma. Hii ni kwa sababu wauzaji wa bidhaa huwa wanamuuzia mteja kile kilichopo, wakati wauzaji wa huduma wanabadilika kulingana na mahitaji ya mteja. Kwa sasa biashara yako inauza bidhaa, hata kama ni huduma, unapaswa kuiuza kama bidhaa, hivyo watu waliozoea kuuza bidhaa watakusaidia kuuza vizuri bila ya kutaka kubadili chochote.
Pia unapoajiri watu wa mauzo, ajiri angalau wawili. Hii inaleta hali fulani ya ushindani baina yao na inawasukuma kujituma zaidi. Mfano kama mmoja ameuza kwa wateja 10 kwa wiki, na mwingine akauza kwa wateja 7, yule wa wateja saba atakazana naye afike wateja 10. Kadhalika wa wateja kumi atakazana zaidi ili asipitwe. Watu wa mauzo huwa wanapenda kujipima kwa namba, unapokuwa na wawili na kuendelea, wanakuwa na ushindani ambao unawasukuma zaidi.
(4 ). Acha kuuza vitu vingine vyote.
Tumeona chanzo cha biashara nyingi kutokuuzika ni zinaendeshwa kwa vurugu, kila kitu kinauzwa na mteja akisema anataka kitu cha tofauti anapatiwa. Sasa hutaweza kuikuza wala kuiuza biashara kama inaendeshwa kwa vurugu kiasi hicho.
Hivyo baada ya kuchagua bidhaa au huduma moja kuu unayouza kwenye biashara yako, acha kuuza vitu vingine vyote. Inawezekana kuna vitu vingine ulikuwa unauza ambavyo vinakuingizia faida. Lakini kama vipo nje ya ile bidhaa au huduma uliyoiainisha kama msingi mkuu wa biashara yako, basi unapaswa kuacha kuuza vitu hivyo vingine.
Unahitaji kuweka nguvu zako zote kwenye kuikuza biashara yako kupitia bidhaa au huduma yenye fursa ya ukuaji zaidi. Unapojihusisha na kuuza vitu vingine, unawapa wateja wako wakati mgumu kukuelewa na kukutegemea.
Wateja wana tabia ya kujaribu wafanyabiashara, watakujaribu kwenye kutaka bei ya chini zaidi, watakujaribu kwenye kutaka kitu cha tofauti na unachotoa na watakujaribu kwa kutaka uboreshe zaidi kile unachotoa kiendane na wao. Epuka sana mitego na majaribu haya ya wateja, simamia kile ulichopanga na wateja wanapojifunza kwamba unasimamia nini, wanakuheshimu kwa hilo na kuwa tayari kununua kile unachouza.
Muhimu ni uzingatie hatua ya kwanza ya kuwa na bidhaa au huduma yenye thamani kwa wateja na ambayo hawawezi kuipata sehemu nyingine yoyote.
(5). Kuwa na mpango bora wa motisha kwa mameneja wako.
Kadiri biashara yako inavyokwenda, inazidi kukua. Timu ya mauzo inaleta wateja na biashara inakuwa kwenye mzunguko chanya wa fedha. Kwa kuwa wewe huhusiki moja kwa moja kwenye mauzo na wala kuandaa bidhaa au huduma, unahitaji kutengeneza viongozi kwenye biashara yako.
Hata mtu anayetaka kununua biashara yako, anaanza kuangalia uongozi uliopo kwenye biashara hiyo. Hivyo utahitaji kuwapandisha cheo wafanyakazi wako na kuwafanya kuwa mameneja, kisha kuajiri wafanyakazi wengine watakaofanya kazi chini ya usimamizi wao.
Ili mameneja hawa wajitume kweli unahitaji kuwa na mpango bora wa motisha kwao.
Zipo njia mbalimbali za kutoa motisha kwa mameneja wako, ipo njia ya kuwalipa bonasi mwisho wa mwaka kutokana na ongezeko la faida, hii inawasukuma kujituma zaidi ili kutengeneza faida kubwa.
Lakini pia baadhi ya wafanyabiashara wamekuwa wanawapa mameneja wao sehemu ya umiliki wa biashara hiyo, kwa kuwapa hisa. Kama lengo lako ni kuuza biashara yako, usitumie njia hii, kwa sababu ukishawapa umiliki, mchakato wa kuiuza biashara hiyo unakuwa mgumu zaidi.
Tumia mfumo wa kulipa bonasi kutokana na ongezeko la faida. Na pale biashara inapouzwa, basi wape zawadi ya bonasi kutokana na mauzo hayo.
(6).Tafuta dalali sahihi kwako.
Baada ya biashara yako kuwa inajiendesha yenyewe, kwa kuwa na timu bora ya uongozi na mzunguko chanya wa fedha, sasa unaanza kuangalia uwezekano wa kuiuza.
Hapa ndipo unapohitaji kutafuta dalali au wakala ambaye atakuunganisha na wanunuaji wa biashara. Zipo kampuni ambazo hizi ndiyo kazi zake, kuwakutanisha wafanyabiashara na wawekezaji au wanunuaji wa biashara.
Unahitaji kuchagua kampuni ambayo utafanya nayo kazi, ambayo itakuwa upande wako. Hivyo ongea na watu mbalimbali mpaka upate ambaye unaona anaweza kukuwakilisha vizuri kwa wanunuzi wa biashara hiyo.
Kampuni hizi za udalali huwa zinalipwa kwa asilimia ya mauzo bada ya mauzo kufanyika, lakini zinakusaidia sana kukutana na wanunuzi na kuweza kuuza biashara yako.
(7). Iambie timu yako ya uongozi kuhusu mpango wa kuuza biashara.
Timu ya uongozi wa biashara yako ni watu ambao wana imani kubwa sana na wewe. Ni watu ambao wanajitoa sana ili biashara yako ikue zaidi. Hivyo unahitaji kuwa makini sana pale unapotaka kuuza biashara yako.
Kwanza unahitaji kufanya mchakato huo kwa siri mwanzoni wakati unatafuta mteja. Ukishapata mteja sasa, unahitaji kuiambia timu yako kuhusu mpango wako wa kuuza.
Inaweza kuwa wakati mgumu sana kwako kuiambia timu ambayo inakuamini kwamba unapanga kuuza biashara hiyo, wapo ambao watakuchukulia wewe ni msaliti na huwajali wao bali unajali fedha tu.
Hivyo unapopanga kuwaambia, waoneshe kwamba biashara inapouzwa, hata wao pia wananufaika. Mfano biashara ikinunuliwa na kampuni ambayo ni kubwa zaidi, wao wanapata nafasi ya kukua zaidi. Wanakuwa kwenye mazingira bora zaidi ya kufanya kazi na pia wanaweza kupata nafasi za juu zaidi.
Pia waahidi kupata bonasi pale ambapo biashara itauzwa. Kwa njia hii watakubaliana na wewe na watakuwa tayari kusaidia ili mchakato wa mauzo ukamilike vizuri.
Ni muhimu uiambie timu yako kwa sababu anayenunua atahitaji kukutana na timu yako ya uongozi na pia kuna ukaguzi wa kina utakaofanyika kwenye biashara yako, ambao utahusisha kila aliyepo kwenye timu ya uongozi.
Hatua ya nane; geuza ofa kuwa makubaliano ya kisheria.
Wale wanaoonesha nia ya kununua biashara yako huwa wanatoa ofa ya kiasi wanachopanga kulipa ili kununua biashara hiyo. Lakini ofa siyo makubaliano, wakati wowote wanaweza kubadilika.
Na katika makubaliano ya kibiashara, watu huwa wanakuwa na mbinu mbalimbali za kupata kitu kwa bei ya chini. Mfano kwenye kuuza biashara, mtu atatoa ofa yake, kisha atafanya uchunguzi kwenye biashara na baadaye atakuja na matokeo ya uchunguzi na kukuambia kuna mambo ambayo ameyaona na hataweza kulipa ofa ya kwanza na hivyo kupunguza.
Ili kuepuka kujikuta kwenye hali hiyo, kwanza chagua ni kiasi gani upo tayari kupokea kwa kuuza biashara yako. Hivyo wanapokuja na ofa ya juu ya kiasi hicho kubali. Lakini pia wape muda wa ukomo, la sivyo zoezi litachukua muda mrefu zaidi.
Wanapofanya uchunguzi na kuja na majibu yao, ambapo watapunguza ofa yao, angalia kama bado inaendana na mpango wako wa awali. Kama ndiyo basi kubaliana nao na kamilisheni dili. Kama ofa yao iko chini ya mpango wako wa awali kataa na tafuta mnunuzi mwingine.
Zoezi la kutengeneza biashara ambayo inaweza kujiendesha yenyewe linategemea zaidi mfumo unaoweka kwenye biashara hiyo, unapokuwa na mfumo bora ndivyo kazi inakuwa rahisi kwako.
Zoezi la kuuza biashara yako huwa ni gumu na linalokuweka kwenye wakati mgumu mno. Hivyo kama unachagua kuuza biashara, lazima ujue una kipindi kigumu mbele yako, kuanzia kupata mnunuzi mpaka kufikia makubaliano.
Iwe unapanga kuuza biashara yako au la, bado utanufaika sana kama biashara yako inaweza kujiendesha yenyewe bila ya kukutegemea wewe moja kwa moja. Hivyo fuata hatua hizi nane na utaweza kutengeneza bishara bora sana kwako.