Sunday, June 30, 2019

ASILI YA BIASHARA NI KUKUA NA KUFA.

Biashara ni kiumbe hai. Inatungwa, inazaliwa, inakua, inafikia makamo na kisha kufa. Hivi ndivyo mifumo yote ya maisha inavyokwenda. Kuanzia kwetu sisi binadamu, kabla hujazaliwa mimba inatungwa, anazaliwa mtoto, anakua, anafikia makamo na kisha anakufa.
Katika mfumo huu wa ukuaji wa biashara, utungwaji wa mimba ya biashara ni yale mawazo ya kuanza biashara ambayo mtu anakuwa nayo. Kisha kuanza kwa biashara ni sawa na mtoto anayezaliwa, kukua na kisha kufa. Sasa kama ilivyo kwenye asili, siyo mimba zote zinazotungwa zinazaliwa, nyingine zinaharibika kabla ya kufikia kuzaliwa. Na hata watoto wadogo wanaozaliwa, wengi hawafiki utu uzima, wanakufa kabla. Na wachache wanafika utu uzima na kufa.
Kwenye biashara, biashara nyingi huwa zinashindwa kabla hata ya kuanza, nyingi zinaishia kwenye mawazo pekee. Kwa zile ambazo zinaanza, nyingi huwa zinakufa kwenye uchanga, hazikui kufikia ukomavu. Na zile ambazo zinakua, huwa zinafikia ukomavu na kufa.
Lakini zipo biashara chache sana ambazo zimeweza kuondoka kwenye mfumo huo wa ukuaji na kufa. Biashara hizi zimekuwa zinajua kinachopelekea biashara kufa baada ya kukomaa ni bidhaa au huduma kuzoelekea na kutokuwa na kitu kipya.
Ili kuondokana na hali hiyo ya biashara kufika ukingoni na kufa, wafanyabiashara hao ambao biashara zao hazifi, wamekuwa wanakuja na bidhaa mpya au huduma mpya kila mara ambapo bidhaa au huduma ya zamani imefikia kilele chake cha mauzo. Hawasubiri mpaka mauzo yaanze kupungua na biashara kufa. Badala yake wanakuja na bidhaa au huduma mpya inayowafanya waendelee kuwa sokoni.
Huu ndiyo mfumo unaotumiwa na makampuni makubwa ya teknolojia, chukulia mfano wa kampuni ya Apple ambayo inazalisha simu aina ya Iphone. Kila mwaka huwa wanakuja na toleo jipya la simu zao, ambalo halitofautiani sana na toleo lililopita. Yote hii ni kuhakikisha kwamba wanaendelea kuwa sokoni. Kwa sababu kampuni ikishatoa toleo jipya, na watu wote wakawa nalo, hakuna tena fursa ya ukuaji. Lakini wanapokuja na toleo jipya, wale waliokuwa na toleo la zamani wanatamani kuwa na toleo jipya na hapo mauzo yanaanza upya.
Kwa biashara unayofanya, angalia jinsi unavyoweza kutumia njia hiyo ya kuwa na toleo jipya la bidhaa au huduma kila wakati ili biashara yako isife.

No comments:

Post a Comment