Saturday, June 22, 2019

ACHA MAIGIZO KATIKA MAISHA YAKO, ISHI UHALISIA WAKO

Watu wanalalamika kwamba hawapati watu sahihi kwenye maisha yao, hawapati wenza sahihi, hawapati watu sahihi wa kushirikiana nao. Na hilo ni rahisi kupata sababu, ambayo ni kila mtu kuwa kwenye maigizo wakati wa kuanza. Na kwa kuwa tunajua maigizo huwa hayadumu muda mrefu, basi muda unapokwenda, rangi halisi za watu zinaonekana na watu kufikiri wenzao wamebadilika. Watu huwa hawabadiliki, ila wanajionesha, wanachoka kuigiza na mambo yanabaki wazi.


Acha kuigiza, acha kuishi maisha ya wengine, ishi maisha yako, ishi uhalisia wako, fanya kile chenye maana kwako, kile ambacho unakiamini kweli, kile ambacho upo tayari kukifanya hata kama hakuna anayekuangalia, hakuna anayekusifia, na kwa njia hii utakuwa na maisha yenye furaha, na pia utawavutia watu sahihi kwa kuwa kile unachoonesha ndicho kilicho ndani yako.

Na kwa kumalizia, waigizaji huwa wanavutia waigizaji, ukianza kuwa halisi, waigizaji wote wanakukimbia, kwa sababu hawataweza kuvumilia ule uhalisi wako.

1 comment:

  1. Maisha ni magumu, lakini sisi wenyewe tumekuwa tunayafanya yawe magumu zaidi. Hasa pale tunapokazana kuishi maisha ya kuwafurahisha wengine, na hivyo kulazimika kuishi maisha ya kuigiza, maisha ambayo siyo halisi kwetu. Tunafanya vitu ambavyo hatupendi kufanya, na wala havina maana kwetu, kwa sababu tu tunataka tuonekane na watu fulani kwamba na sisi tupo aina fulani.

    Hili linafanya maisha kuwa magumu kwa sababu, wale tunaokazana watuone, wala hawana muda na sisi. Wanahangaika na maisha yao, ambayo nayo ni changamoto kwao, au wanahangaika na kuwaridhisha wengine na hivyo hawakuoni wewe unavyohangaika kuwaridhisha.

    ReplyDelete