Sunday, June 13, 2021

WAEPUKE KAMA UKOMA WATU WENYE TABIA HIZI 15 , NI SUMU KWA MAFANIKIO YAKO.


 Rafiki yangu mpendwa,
Kuna watu wanaitwa ‘watu sumu’ watu ambao kwa kujihusisha nao unajikuta ukirudi nyuma badala ya kusonga mbele.

Kwa kuwa wale unaojihusisha nao huwa wana ushawishi mkubwa kwako, unapaswa kuwa makini sana na kila mtu unayemruhusu awe karibu yako.

Leo tunakwenda kuziangalia tabia 15 za watu hao sumu, kama unazo unapaswa kuziacha na ukiwaona watu wanazo kaa nao mbali.




Tabia 15 za watu sumu wa kuwaepuka kwenye maisha yako.

( 1), KUISHI  JUU  YA  KIPATO.
Mtu yeyote anayetumia zaidi ya kipato chake ni mtu sumu, hataweza kupiga hatua kubwa kwenye maisha yake.
Hawa ni watu ambao hukopa fedha kwa matumizi ya kawaida ambayo hata siyo muhimu.
Kama una tabia hii acha mara moja. Na ukishaona mtu ana tabia hii achana naye, maana atakushawishi na wewe uwe kama yeye.

( 2 ). WANAJUA  KILA  KITU  KWENYE   MICHEZO  NA  BURUDANI.
Watu sumu huwa wana muda mwingi wa kufuatilia mambo ya michezo na burudani kuliko wanavyotumia kufanya mambo ya kuwapa mafanikio.
Badala ya kuyageuza maisha yao kuwa burudani kwao kwa kuziishi ndoto zao, wanatafuta burudani kutoka nje, kitu ambacho huwa hakiwasaidii.
Chagua kupata burudani kwenye kuishi ndoto zako na siyo kuhangaika na ndoto za nje.

( 3 ). KUFUATILIA  WATU  MAARUFU.
Watu sumu huwa wanafuatilia na kujua maisha ya wengine kuliko wanavyoyajua maisha yao wenyewe.
Wanayajua mahusiano ya watu maarufu, wanajua kiasi cha fedha walichonacho na hata wanajua jinsi ya kuwashauri.
Cha kushangaza, hawajui kuhusu fedha zao wenyewe na hawawezi kujishauri licha ya maisha yao kuhitaji sana ushauri kuliko hata wanaoutoa kwa wengine.
Acha mara moja kufuatilia maisha ya wengine na pambana na maisha yako, na wale wanaopenda kufanya hivyo, achana nao.

( 4 ). HAWAPENDI  HATARI.
Kufanya vitu vipya kuna hatari ya kushindwa, watu sumu hawapendi kushindwa, hivyo hufanya yale tu waliyozoea.
Wakikuona wewe unajaribu vitu vipya na vikubwa hawatakuacha kirahisi, watakukosoa na kukukatisha tamaa ili usichukue hatua hizo.
Tambua bila kuchukua hatua hatari huwezi kufanikiwa, hivyo achana na yeyote anayekukatisha tamaa kwenye hatua kubwa unazopanga kuchukua.

( 5 ). HAWANA  MSUKUMO  MKUBWA.
Watu sumu wameridhika sana na maisha ya chini waliyonayo, hawana msukumo wa kufanya makubwa zaidi. Wakipata kazi wanaona wamemaliza kila kitu. Wakiwa na biashara ndogo wanaona wameshayawezea maisha. Ni mpaka wakutane na changamoto ndiyo wanajua mazoea siyo mazuri.
Wewe kuwa na msukumo wa kufanya makubwa, jiwekee malengo makubwa na pambana kuyafikia, ukishayafikia usiridhike, weka malengo mengine makubwa zaidi.
Achana kabisa na wale walioridhika na maisha yao ya chini.

( 6 ). WANAWALAUMU  WANASIASA.
Watu sumu huwa wanatupa lawama zao kwa wanasiasa na wengine wenye mamlaka. Kama hawajapata wanachotaka, wanaona sababu ni wanasiasa.
Wanawasikilia na kuwaamini wanasiasa wanapowaahidi mambo mbalimbali.
Wasichojua ni kwamba wanasiasa wanaishi kwa kuwategemea wao, hivyo hawawezi kuwasaidia kwa namna yoyote ile.
Jua haya maisha ni vita yako mwenyewe, kama utashinda au kushindwa ni kwa sababu zako mwenyewe hivyo usimlaumu yeyote.
Usimwamini mwanasiasa yeyote anapokuahidi chochote, pambana kwa juhudi zako kupata kile unachotaka.

( 7 ). WANACHUKIA  MATAJIRI.
Watu sumu huwa wanawachukia sana matajiri, wanawaona ndiyo chanzo cha wao kubaki kwenye umasikini. Au wanapotaka kitu kutoka kwa matajiri na wasiwape, wanawaona wana roho mbaya. Wasijue kwamba matajiri hao wana nidhamu kubwa kwenye yale waliyopanga.
Wapende matajiri, waone ni watu wazuri, jifunze kutoka kwao ili na wewe uweze kufikia utajiri pia.
Na ukimuona mtu yeyote anawasema vibaya matajiri, kaa naye mbali.

( 8 ). WANAKANDIA  ELIMU   YA  MAENDELEO  BINAFSI.
Watu sumu huwa wanajiona tayari wanajua kila kitu kwenye maisha yao. Waambie wasome vitabu vya maendeleo binafsi na watakuambia hawana muda. Waoneshe muda wanaopoteza na watakuambia hakuna kipya kwenye vitabu hivyo, ni yale yale tu.
Wewe usiwe kwenye kundi hilo, penda kujiendeleza binafsi, soma vitabu, jifunze na chukua hatua.
Na unapokutana na mtu akakuambia hakuna kipya kwenye vitabu au tayari anajua yote hayo, kaa naye mbali, ni mtu sumu huyo.

 ( 9 ). WANAKUPA  USHAURI  MBAYA.
Watu sumu hukimbilia kukupa ushauri kabla hata hujawaomba na ushauri wanaokupa huwa ni mbaya. Kwa sababu hawataki upige hatua kuliko wao, watahakikisha wanakushauri mambo yatakayokukwamisha.
Usipende kutoa ushauri kwa wale ambao hawajakuomba na epuka sana kupokea ushauri kwa watu ambao hujawaomba.
Gharama ya ushauri wa bure ni pale unapoanza kuufanyia kazi, kwa kuwa utakugharimu sana.
Jua watu ambao ushauri wao huwa una walakini na waepuke sana, maana pia huwa wanalazimisha upokee ushauri wao.

(10 ). KUULIZA  MASWALI  YA  KIJINGA.
Watu sumu huwa wanapenda sana kuuliza maswali ya kijinga. Waambie kitu kizuri na wao watatafuta njia ya kuonesha hakiwafai wao.
Waambie wasome vitabu watakuambia hawajui wapate wapi vitabu.
Waambie wapambane kutoka kwenye umasikini na watakuambia wote hatuwezi kuwa matajiri.
Waambie wajiajiri watakuambia wote tukijiajiri nani atamfanyia kazi mwenzake.
Yote hayo ni maswali ya kijinga na usijisumbue kuyajibu, waache wajiridhishe nayo.
Waepuke sana watu wenye maswali ya kijinga, maswali yanayotengeneza vikwazo kwenye kila jambo zuri.

( 11 ). HAWANA  NIDHAMU.
Wanapanga kufanya kitu, ila inapofika wakati wa kukifanya wanaahirisha na kuona hawajawa tayari.
Tatizo siyo kutokuwa tayari, tatizo ni kukosa nidhamu ya kujisimamia na hilo linakuwa kikwazo kwa mafanikio yako.
Jijengee nidhamu ya hali ya juu sana, panga mambo na fanya kama ulivyopanga bila kuruhusu chochote kukuzuia.
Na ukiwaona watu ambao hawana nidhamu, kaa nao mbali.

( 12 ). WANA CHUKI  NA  WIVU.
Watu sumu hawapendi kuona wengine wakipiga hatua kuliko wao, hivyo huwa na chuki na wivu kwa wale wanaopata matokeo mazuri kuliko wao.
Usiwe mtu wa chuki au wivu, kuwa mtu wa kupenda na kujifunza kutoka kwa wengine.
Na unapojikuta umezungukwa na watu wenye chuki na wivu, kimbia haraka.

( 13 ). HAWAWEZI  KUDHIBITI  HISIA  ZAO.
Watu sumu ni watu ambao hisia zao hulipuka haraka hata kwa vitu vidogo tu. Huwa ni rahisi sana kukasirishwa na mambo madogo madogo na yasiyo na tija. Kwa watu kujua udhaifu wao, wanautumia kujinufaisha.
Jifunze kudhibiti hisia zako na usimpe yeyote ruhusa ya kukukasirisha kwa jambo lolote lile.
Pia waepuke sana wale ambao hisia zao zinaweza kuibuliwa na mambo madogo madogo.

( 14 ). WANACHAFUA  MIILI  NA  AKILI  ZAO.
Watu sumu huchafua miili yao kwa kuilisha vyakula visivyo vya afya na vilevi mbalimbali, hilo hupelekea miili yao kuwa dhaifu na kushindwa kupambana na mafanikio.
Pia huchafua akili zao kwa kujaza habari hasi na umbea.
Epuka kuchafua mwili na akili yako, lisha vitu ambavyo ni safi na bora. Epuka vyakula vya haraka, vilevi na habari hasi.
Pia waepuke wote ambao hawathamini miili na akili zao.

( 15 ). WANA  SABABU  NYINGI.
Watu sumu huwa wana sababu za kujitetea kwenye kila jambo. Huwa siyo watu wa kuchukua uwajibikaji kwenye jambo lolote lile.
Wewe achana na sababu, kama kuna kitu kimetokea, kubali kuwajibika. Kwa njia hiyo wengi watakuamini na kukupa majukumu zaidi.
Waepuke sana wale wenye sababu na visingizio kwenye kila jambo.

Kwa kuangalia tabia hizi 15, kuna watu wengi itabidi uachane nao kwenye maisha yako, lakini hakuna namna, lazima ufanye hivyo kama unayataka mafanikio makubwa katika  sayari  hii  DUNIA.

No comments:

Post a Comment