Kwa kufanyia kazi maeneo haya 10 ninayoshirikisha hapa, kuna nafasi nzuri ya kujenga vijana imara na wenye mchango mkubwa kwenye taifa letu.
( 1 ): BIASHARA NA UJASIRIAMALI.
Serikali
haina uwezo wa kuwaajiri vijana wote waliohitimu elimu katika ngazi
mbalimbali. Hata sekta binafsi pia haiwezi kuwaajiri wote wanaotaka
kazi.
Lakini jamii zetu zina mahitaji na changamoto mbalimbali ambazo zikipata utatuzi wapo tayari kulipia.
Hii
inatoa fursa kubwa ya vijana kuweza kufanya biashara na ujasiriamali wa
aina mbalimbali kulingana na mahitaji yaliyo kwenye jamii.
Vijana wanaziona sana fursa hizo na wapo tayari kuzifanyia kazi, lakini mazingira yamekuwa siyo rafiki kwao kuchukua hatua.
Kuanzisha na kurasimisha biashara kwenye nchi yetu kimekuwa kikwazo kwa wenye nia ya kufanya hivyo.
Tunashukuru usajili wa biashara umerahisishwa sana kupitia BRELA, ila eneo la kodi bado lina changamoto kubwa.
Kijana anayeanzisha biashara mpya anatakiwa kuanza kulipa kodi kabla hata biashara haijaweza kuzalisha faida.
Biashara yoyote ile ina hatari ya kufa hasa kipindi cha mwanzo.
Kama
ukiwekwa utaratibu wa vijana kupata neema ya kodi katika miaka miwili
ya mwanzo ya biashara, huku wakiwa wanazifanya biashara zao kwa mfumo
rasmi, itasaidia sana.
Taifa litapata mapato zaidi kupitia mzunguko
unaotengenezwa na biashara mpya zinazoanzishwa na vijana kuliko
linavyopoteza kwenye kodi.
( 2 ): FEDHA NA UCHUMI.
Hali ya uchumi wa kijana wa Tanzania bado iko chini sana kutokana na ushiriki wake mdogo kwenye shughuli mbalimbali za kiuchumi.
Na kikwazo cha kwanza ni fedha, vijana wengi hawana vipato kabisa na wale walio navyo haviwatoshelezi kwenye mahitaji yao.
Hilo linakuwa kikwazo kwao kushiriki shughuli za uchumi kama kuanzisha biashara na hata kuwekeza pia.
Huduma
za kifedha zimekuwa zinawatenga vijana kwa sababu hawakidhi vigezo
muhimu vilivyowekwa, kama kuwa na dhamana ili kupata mikopo.
Kwa
kuwa serikali imeweza kuwakopesha vijana wengi wakapata elimu ya juu,
inaweza pia kuwakopesha fedha za kuwawezesha kushiriki shughuli za
uchumi.
Vijana wajengewe uwezo wa kuwa kwenye vikundi ambavyo
vitapewa mikopo ya kutumia kwa shughuli za uchumi na kuilipa kwa njia
nafuu kuliko mikopo ya taasisi za kifedha.
Pia elimu ya kijana iweze kutumika kama dhamana ya kupata fedha kwa shughuli mbalimbali anazofanya.
( 3 ). KILIMO NA UFUGAJI.
Uhitaji wa chakula ni mkubwa kwenye nchi yetu na nji za jirani.
Nchi yetu imejaliwa kuwa na eneo kubwa la ardhi ambayo bado haijatumika kabisa.
Hayo yanatoa fursa kubwa ya vijana kuweza kujishughulisha na kilimo na ufugaji.
Lakini
changamoto kwenye eneo hilo ni kubwa mno. Kuanzia kwenye uzalishaji
mpaka kufika sokoni, kijana anakumbana na mengi yanayomuangusha kabisa.
Vijana wengi wamejaribu kilimo na ufugaji na hawajaweza kurudia tena kutokana na anguko ambalo wamepitia.
Kukosa miundombinu bora, kama kutegemea mvua badala ya kuwa na nyezo za umwagiliaji imekuwa inaathiri sana uzalishaji.
Na
hata pale kwa bahati nzuri kijana anapoweza kuzalisha vizuri, akifika
sokoni bei inakuwa siyo rafiki kwake, anapata hasara na kushindwa kurudi
tena shambani.
Kutengwa
kwa maeneo ya kilimo na ufugaji ambayo yamewekewa miundombinu muhimu
hasa ya upatikanaji wa maji ya uhakika itasaidia sana kwenye hili.
Pia kufungua masoko hasa ya nje itampa kijana wigo mpana wa kuuza kile anachozalisha.
( 4 ). SAYANSI NA TEKNOLOJIA.
Sayansi na teknolojia vinakua kwa kasi kubwa mno na hakuna anayeweza kuvizuia.
Ukuaji huu wa kasi wa teknolojia umefungua fursa za vijana kuweza kujiajiri kwa urahisi kabisa kwa kutumia mtandao wa intaneti.
Lakini kijana wa Tanzania bado anakutana na vikwazo vingi anapojaribu kutumia fursa ya teknolojia kujiajiri.
Changamoto ya kwanza ipo kwenye urasimishaji wa biashara ambazo kijana anaweza kufanya mtandaoni akiwa hata nyumbani. Hilo linawafanya washindwe kukua kwenye biashara hizo na hata kupata huduma nyingine muhimu.
Changamoto
nyingine kubwa ni kulipwa kutoka nje ya nchi. Teknolojia imerahisisha
mtu kuweza kuuza huduma mbalimbali za kidijitali kwa mtu yeyote aliye
popote duniani.
Lakini kupokea malipo kutoka nchi za nje, jasa nje ya Afrika Mashariki ni kitu kigumu sana.
Kuna mifumo ya kupokea malipo mtandaoni kama Paypal na Stripe, lakini haifanyi kazi kwa hapa Tanzania.
Ni wakati sasa wa kufungua mifumo hii ya malipo ili vijana waweze kutumia teknolojia kuuza huduma zao na kupokea malipo popote duniani.
( 5 ). ELIMU NA UBUNIFU.
Mfumo wetu wa elimu pamoja na mapungufu yake mengi umeweza kuzalisha wahitimu wengi kwenye ngazi mbalimbali.
Kuna changamoto kubwa mbili zinazomkabili kijana kwenye eneo hili.
Changamoto
ya kwanza ni kuhitimu huku akiwa hana uwezo wa kufanya chochote. Elimu
yetu kwa sehemu kubwa imekuwa ni ya kukariri na kujibu mitihani. Vijana
wanahitimu wakiwa na ufaulu mkubwa lakini hakuna wanachoweza kufanya.
Ni
wakati sasa wa kufanya mapinduzi kwenye mfumo wetu wa elimu, ili
uzalishe vijana wenye uwezo wa kufanya vitu vyenye tija kwa jamii.
Elimu
ikuze ubunifu wa vijana katika kuyatumia mazingira yao kuzalisha
thamani zaidi kwao na kwa wengine pia. Iwajengaa kujitambua na kujiamini
kwenye yale wanayofanya.
Changamoto ya pili ni mzigo mkubwa wa deni la elimu ya juu kwa wale waliopata nafasi ya kusoma elimu hiyo kwa mkopo.
Mikopo ya elimu ya juu imekuwa na msaada mkubwa, kwani wengi tusingeweza kugharamia elimu hiyo bila mkopo.
Lakini mkopo huo umekuja kuwa kikwazo kikubwa kwa kijana kujinasua kiuchumi.
Anayepata
ajira anakatwa kiasi kikubwa kulipa deni hivyo hawezi kubaki na fedha
ya kutosha kumwezesha kufanya shughuli za kiuchumi.
Ambaye hajapata ajira deni lake linaendelea kukua zaidi na zaidi.
Mabadiliko yafanyike kwenye sera ya urejeshaji wa mikopo ya elimu ya juu ili impe kijana ahueni ya kuweza kushiriki shughuli nyingine za uchumi.
( 6 ). AJIRA NA KUJIAJIRI.
Pamoja
na kwamba serikali haiwezi kuwaajiri vijana wote, bado ina uwezo wa
kutengeneza fursa za ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja
kwa vijana.
Bado taifa lina uhitaji wa wafanyakazi na watoa huduma
zaidi kwenye jamii zetu. Jamii bado haijapata wahudumu wa kutosha hasa
kwenye sekta za afya na elimu.
Hivyo serikali inapaswa kuwekeza kwenye kuajiri vijana zaidi na kupitia kufanya hivyo inajenga nguvu kazi kubwa zaidi.
Lakini
pia serikali inapaswa kuweka mazingira mazuri kwa sekta binafsi kuweza
kuwaajiri vijana wengi. Kadiri mazingira ya kibiashara yanavyokuwa
mazuri, ndivyo sekta binafsi zinavyostawi na kutoa nafasi zaidi za
ajira.
Na kwa wale ambao wanakosa nafasi za kuajiriwa serikalini au
kwenye sekta binafsi, wawe na mazingira mazuri ya kuweza kujiajiri
wenyewe kama tulivyoona kwenye sekta mbalimbali hapo juu.
( 7 ). UONGOZI NA USIMAMIZI.
Vijana
wanahitajika sana kwenye nafasi mbalimbali za uongozi. Hili linaleta
damu mpya kwenye uongozi lakini pia linatengeneza viongozi wazuri kwa
ajili ya siku zijazo.
Hakuna njia bora ya kujifunza kitu chochote kile kama kufanya. Hivyo vijana watajifunza uongozi kwa kupewa nafasi za uongozi.
Kwa
bahati mbaya sana kizazi cha sasa cha vijana kimepita kwenye vyuo vikuu
ambavyo havijaweza tena kutengeneza viongozi kama zamani.
Serikali
za wanafunzi wa vyuo vikuu hazipo tena huru kama zamani, hivyo vijana
hawajifunzi kuwa viongozi huru wanaofanya maamuzi yao wenyewe.
Tunakokwenda tunatengeneza taifa la viongozi wasiokuwa na msimamo wao
wenyewe hasa kwa maslahi ya taifa.
Kumekuwa
na mabaraza ya vijana ndani ya vyana vya siasa, lengo lake yamekuwa ni
kutengeneza viongozi. Lakini hayawezi kufanya vizuri kwa sababu ndani ya
vyama vijana wanaegemea zaidi kwenye itikadi. Na hata kupata nafasi
hauangaliwi uwezo, bali kuonekana na kujipendekeza.
Ni muhimu nafasi
za uongozi na usimamizi zitolewe kwa vijana kwa kuangalia uwezo wao. Na
siyo tu uwezo kwenye ufaulu wa kielimu, bali kuangalia mambo ambayo
kijana ameweza kufanya mwenyewe bila ya kusimamiwa na yeyote.
Uwezo ukitumika katika kuwapa vijana uongozi, itawezesha kupata viongozi wazuri, na pia kuwajenga kuwa viongozi bora zaidi.
( 8 ). VIWANDA NA UZALISHAJI.
Hakuna
nchi inayoweza kupiga hatua kiuchumi bila ya uzalishaji. Serikali
imekuwa inaimba wimbo wa viwanda lakini mtazamo umekuwa zaidi kwenye
viwanda vikubwa vinavyolenga wawekezaji kutoka nje.
Nchi yetu inazalisha kila aina ya malighafi, lakini bidhaa nyingi tunaingiza kutoka nje.
Kuna fursa kubwa ya vijana kuweza kujiingiza kwenye shughuli za viwanda na uzalishaji ili kuchangia kwenye ukuaji wa uchumi.
Mambo yanayohitajika katika kuwezesha hili ni elimu ya uzalishaji na viwanda itolewe kwenye vyuo vyetu vya ufundi.
Mchakato wa kuanzisha kiwanda ufanywe kuwa rahisi hasa kwa wazawa ili kupunguza urasimu unaokuwa kikwazo kwa wengi.
Upatikanaji wa mitaji na miundombinu mengine muhimu kwa ajili ya viwanda.
Sehemu kubwa ya bidhaa tunazoagiza nje zinaweza kuzalishwa hapa nchini na vijana kama wakiwekewa mazingira mazuri.
( 9 ). AFYA NA USTAWI.
Bila afya ya vijana taifa haliwezi kustawi. Afya ndiyo mtaji wa kwanza na muhimu kabisa kwa maendeleo ya taifa.
Vijana
wana changamoto nyingi za kiafya, kuanzia afya ya uzazi, ulevi na
uraibu, kushindwa kumudu gharama za afya na kukosekana kwa huduma bora
za afya hasa maeneo ya vijijini.
Elimu ya afya ya uzazi na afya kwa ujumla inapaswa kutolewa kwa vijana ili wajue thamani ya afya zao na kujikinga na maradhi.
Elimu
ya afya ya akili inapaswa kupewa kipaumbele kikubwa, kumekuwa na
ongezeko kubwa la magonjwa ya akili na ambayo hayashughulikiwi vizuri
kutokana na watu kukosa uelewa wa magonjwa hayo.
Vilevi na madawa ya kulevya vinapaswa kudhibitiwa sana ili visiharibu nguvukazi ya taifa.
Bima za afya kwa kila kijana ni muhimu ili kuweza kupata huduma za afya bila kuwepo kwa kikwazo cha gharama.
Na huduma za afya zinapaswa kuwa bora kwenye kila eneo ili kijana aweze kuzipata pale anapozihitaji.
( 10 ). TAFAITI NA MAANDIKO.
Kila
kijana ambaye amefika elimu ya juu na kupata shahada, kuna utafiti
amefanya. Lakini tafiti zote hizo huwa hazina manufaa yoyote kwa taifa.
Zinachukuliwa kama sehemu tu ya mtu kupata shahada yake.
Hili siyo sawa, taifa linahitaji tafiti nyingi mno ili kujua nini kinaendelea kwenye kila eneo na nini kinaweza kufanyika.
Tafiti zinasaidia sana kuweza kufanya maamuzi sahihi kwenye mambo mbalimbali.
Vijana
wanaweza kufanya tafiti na kuandika mambo yenye manufaa kwa taifa letu.
Badala ya kuiga kila kitu kutoka kwa wengine, tunaweza kufanya tafiti
kwa mazingira yetu na kujua kipi tunaweza kufanya na kikawa na tija.
Uwepo
wa takwimu sahihi zinazohusu vijana pia ni hitaji muhimu katika kupima
maendeleo ya vijana na ufanisi wa hatua mbalimbali zinazochukuliwa.
Mfano
kujua vijana wangapi wenye elimu za ngazi mbalimbali na taaluma
mbalimbali, kujua wangapi wameajiriwa serikalini, sekta binafsi au
kujiajiri wenyewe. Kujua wangapi wapo kwenye kilimo, teknolojia na sekta
nyingine.
Kwa kuwa na taarifa sahihi itasaidia kufanya maamuzi yenye tija kwa vijana.
Maeneo haya kumi yamegusa karibu kila eneo la maisha ya kijana na hata Mtanzania kwa ujumla. Tafiti zaidi zinahitajika kwenye kila eneo ili kuweza kufanya maamuzi bora na yenye tija kwa vijana na taifa.
Imani
yangu kubwa ni vijana wakiwezeshwa kwa kujengewa uwezo wa kuweza
kuzitumia fursa nyingi zilizo kwenye jamii zetu, taifa letu litanufaika
kwa kiasi kikubwa mno.
Taifa liwekeze kwa vijana, matokeo ya baadaye yatakuwa makubwa sana.
Je , unawaza ufanye nini ? Ungana na " DARASA ONLINE " ujifunze mengi ya kukuwezesha kutoka katika hali ya utegemezi na kuweza kusimama peke yako na kufanikiwa.
NA KOCHA MWL. JAPHET MASATU , DAR ES SALAAM
Tuwasiliane kwa WhatsApp + 255 716924136 / 0755 400 128
No comments:
Post a Comment