Tunaishi katika wakati ambao vyombo vya habari vimepata nafasi kubwa ya kutoa taarifa, matangazo au habari ambazo zinasababisha watu wengi kuhemka au kujengewa hofu dhidi ya mambo yanavyoendelea katika jamii. Utaona au kusikia matangazo iwe katika vyombo vya habari au mtandaoni yote yameshajua namna yanavyoweza kufanya watu washindwe kujidhibiti kuamua mambo au kufuatilia vitu. Hili limechangia sana watu wengi waendeshe maisha yanayokosa utulivu kabisa.
Utaona naona ambavyo matukio mengi yakitokea iwe ni jambo linalovuma mtandaoni basi kila mtu hatataka kutulia limpite bali afuatilie. Kufuatilia huko hakujasaidia zaidi kumeleta usumbufu mkubwa kwa maisha ya watu wengi pale ambapo hata wameweza kuwa wamejiunga kupewa taarifa ya mambo ikitokea basi waarifiwe almaarufu “notifications”. Hili limesababisha watu muda wote wakae mitandaoni au kushika simu kuhakikisha hapitwi na matukio yoyote yale. Hili limesababisha watu wengi wakose muda binafsi wa kukaa wenyewe kutafakari maisha.
Si ajabu kuona leo hii watu wakishindwa kudhibiti hisia zao za furaha au huzuni kwa kushirikisha kila kitu katika mitandao ya kijamii. Mfano mtu kagombana na mpenzi wake basi hilo tukio atataka watu wote wajue kuwa mahusiano yao yapo katika migogoro. Wengine hata wameweza kuthubutu hata kuanika mambo yao ya siri mtandaoni na baadaye wanajutia juu ya maamuzi hayo waloyatenda sababu tu ya mihemko au hasira.
Bado kuna kundi la watu wachache ambao wana uwezo wa kudhibiti mihemko yao licha wanaweza kuonesha kwa wengine namna walivyoguswa na matukio au hali wazipitiazo. Mtu anajenga udhibiti wa mihemko akijua katika mihemko kuna maamuzi ya ovyo hufanyika na mwisho wake ni fedheha. Mtu ambaye pia anashindwa kujidhibiti kifalsafa ni kudhihirisha uchanga wa kuielewa falsafa. Udhibiti wa mihemko au hisia ni ukomavu ambao katika shule ya falsafa unahimizwa sana maana kuna manufaa makubwa katika udhibiti wa mihemko kuliko hasara zake.
Njia ni ile ile katika udhibiti wa mihemko kwa kujiuliza je nitakalo kulifanya ni lazima kulifanya ?. Kadri unavyojiuliza na kujihoji juu ya ulazima wa kushirikisha kitu, kusema kitu, kufanya kitu ndivyo unavyoweza kuamua kitu kwa hekima na bila majuto siku za usoni.
Karibu Ujiunge na " DARASA ONLINE " kujifunza zaidi
Tuwasiliane
No comments:
Post a Comment