Kitu kimoja ambacho watu wengi hatuandaliwi mapema kufahamu basi ni kuambiwa ukweli wa maisha. Ukweli wa maisha ni kuwa maisha yatakuwa na changamoto siku zote. Changamoto hizi hazitaondoka hata tukifanikiwa kwa baadhi ya mambo tutakayo. Tutakapofanikiwa basi tutakutana na muundo mwingine wa changamoto.
Unaweza kutamani maisha yasingekuwa na changamoto ili yawe mazuri, imara au maana. Ila ukiangalia kwa kina uwepo wa changamoto ndio uletao ladha nzuri ya maisha, ndio unaofanya uzalishe wabunifu, wagunduzi na wanafalsafa. Changamoto zimefanya turejee ndani yetu na tugundue tuna uwezo mkubwa ambao tunapotumia tunavuka na kutatua hali mbalimbali ambazo zinajitokeza tunapoendelea kuishi.
Usipokuwa imara kihisia katika zama tunazoishi basi matukio yanayoendelea kutokea maishani yatakudhoofisha, yatakunyima furaha na yakufanya uishi na wasiwasi wakati wote. Ukomavu wa kihisia ni uwezo wa namna usivyoweza kutetereka na chochote kinachotokea maana unakuwa umejiandaa kuwa hata mabaya ni sehemu ya maisha, magumu ni njia ya maisha na changamoto ni fursa ya kukua na kukomaa. Watu wengi wasojiandaa kwa lolote kutokea ni rahisi hisia zao kuumizwa.
Kadri unavyoweza kukabiliana na changamoto na kuzivuka ndani yako unajenga utulivu, nguvu, uimara na ukomavu. Mtu ambaye anapitia changamoto nyingi ni mtu aliye imara kuliko mtu ambaye hapitii magumu au changamoto zozote. Uzuri wa changamoto ni kuwa unamsaidia mtu kutumia akili, kustahimili na kujituma ili avuke hapo. Kupitia mchakato wote wa kukabiliana na changamoto basi mtu anajenga uzoefu, hekima, ujuzi na uimara wa kukabiliana na changamoto nyingine mpya.
Simama imara katika wakati ambao maisha yatakutana na changamoto. Huu ni wakati ambao unapaswa kuwa tayari kukabiliana na changamoto ili zikusaidie ukomae, ukue na uwe imara zaidi kwa ajili ya changamoto nyingine mpya zitakazojitokeza maishani.
NA KOCHA MWL. JAPHET MASATU , DAR ES SALAAM
WhatsApp + 255 716 924136 / + 255 755 400128
No comments:
Post a Comment