Friday, April 2, 2021

WEWE NI WA PEKEE SANA , ISHI UHALISIA WAKO.

Falsafa ya Ustoa inatualika sote kuishi kulingana na asili yetu. Kuogopa, kutokujiamini, kutojikubali ni mambo ambayo falsafa haiyaruhusu yawe ndani ya mtu anayetaka kuishi uhalisia wake alivyo. Kutojiamini ni zao la kutokujikubali. Maisha ya kijasiri huzaliwa pale ambapo mtu anatambua namna ana nguvu, kujikubali kupitia vipawa vyake, vipaji vyake na kuwa tayari kuishi bila kupepesa macho yoyote yale akiiga maisha ya watu wengine. Ukiiga maisha ya watu wengine ni kujivua uhalisia wako na huwezi kukutana na utoshelevu wa kile unachokifanya.

Wengi wanaogopa kuruhusu kuishi vipawa, vipaji vyao, ujuzi wao na msukumo wowote ule wenye tija kuonesha dunia. Hofu imekuwa kikwazo kwa wengi wakiona wakiishi au kuonesha uwezo walionao kwa watu wanaowazunguka watavunjwa moyo. Watakatazwa, watasemwa au kuchekwa.

Katika maisha yangu ya kujifunza, kuandika, kusoma vitabu na kutunga mashairi sijawahi kupata ukinzani wowote toka kwa wazazi wangu. Wao walikuwa watu wa kwanza kunikubali kuwa nimeamua kuishi maisha hayo. Hili limeacha alama kubwa sana maishani kuishi au kutoogopa kujifunza, kuandika na kutunga mashairi sehemu yoyote ile maana naona kufanya hili napata utoshelevu mkubwa ndani yangu.

Watu wote wenye ushawishi mkubwa duniani wametokana na wao kuishi kwa uhalisia, wamejikubali kuwa wao kama wao na kwa njia hiyo imewatengeneza wawe watu wenye nguvu katika maeneo ya taaluma zao, vipaji, biashara, mahusiano na uongozi. Unapoishi ishi kulingana na kitu kilivyopaswa kuishi moja kwa moja nishati au nguvu huzalishwa.

Jitoe na idhihirishie Dunia kuwa una kitu ndani yako cha tofauti ambacho upo tayari kukionesha, kutoa, kuchangia dunia iwe bora kuliko vile ulivyoikuta. Wale wanaojitoa, wanaotoa mchango wao mkubwa ndio wenye kufikia njia ya kuona ni watoshelevu ndani yao. Kubali kuwa halisi, kubali kuvipa vitu ulivyonavyo thamani na kuwa tayari kuishi bila kujibakiza. Maisha haya yana maana kubwa kuliko maisha ya kujikimbia uhalisia wako, au kuviacha vipaji vyako bila kutumiwa. Tumia vyote ulivyojaliwa kuifanya dunia sehemu salama ya kuishi.

NA  KOCHA  MWL.  JAPHET  MASATU , DAR  ES  SALAAM.

WhatsApp + 255 716 924136 / + 255 755 400128 /   + 255 688 361 539

 

No comments:

Post a Comment