Friday, April 2, 2021

MAISHA BORA HUJENGWA KATIKA SUBIRA , HEKIMA , NA ULIMI MWEMA.

Maisha yanahitaji nini kama si uwezo mkubwa wa mambo matatu. Maisha ni mapambano ambayo yanahitaji moyo wa subira, ubongo wa hekima na ulimi mwema. Haya mambo matatu unapokuwepo nayo maishani basi ni njia ya kuyaishi maisha bora katika dunia hii. Maisha yatatupa magumu, mateso na matatizo hivyo ili uwe imara lazima uwe na moyo wa subira, uwe na hekima na udhibiti wa ulimi au uneni wako.

Magumu mengi yanayojitokeza katika maisha yanazidi kuwa makubwa pale ambapo tunakosa kuwa ni watu wenye subira, kukosa hekima na udhibiti mdogo wa kauli zetu. Unapokuwa na moyo wa subira unaweza kuvumilia na kukabiliana na hali zozote katika maisha. Unapokuwa na ubongo wa hekima unajiepusha na maangamivu yaletwayo na ujinga na tatu unapokuwa na udhibiti wa kinywa chako unajiepusha migogoro na watu wanaokuzunguka.

Jifunze kuwa na subira katika maisha haya. Ili umeanzisha kitu basi jua hakiweza kukupatia matokeo leo leo bali unapaswa kuvuta subira ukiwa unaendelea kuweka juhudi hadi ufike kuyapata matokeo yake. Moyo wa subira utakusaidia ukomae katika kuyakabili mambo maishani. Ukikosa subira utakuwa ukipata changamoto nyingi za kuumizwa hisia maana hakuna kitu kilicho bora maishani kisichohitaji moyo wa subira.

Itafute hekima ili uweze kuyaongoza maisha. Hekima ni lulu katika maisha ya mtu. Walio na hekima hutafutwa kila sehemu maana kupitia hekima maisha huenda, maisha huwa salama na kuwa imara. Hekima huzaliwa katika kujifunza kutokana na maisha ya watu wengine, kukaa na watu wenye hekima, kusoma vitabu na kadhalika.

Mwisho zuia ulimi wako usiseme hila, usisambaze habari zisizo za kweli na ruhusu ulimi wako usambaze upendo na nuru kwa wengine. Hili litakuepusha na mambo mengi maishani.

Maisha yanaweza kuwa imara uwapo katika jitihada ya mambo haya matatu. Kuwa na moyo wa subira, ubongo wa hekima na udhibiti wa ulimi. Yaishipo ndani ya mtu humpa mtu kuwa na maisha bora.

NA  KOCHA  MWL.  JAPHET   MASATU

WhatsApp + 255 716 924136 /   + 255 755 400128

EMAIL : japhetmasatu@gmail.com

 

No comments:

Post a Comment