Ni kawaida ya watu kulaumu pale mambo yanapoenda vibaya. Kulaumu kunampa mtu kuona jambo lilotokea hahusiki au kujiondoa katika wajibu fulani. Kulaumu ni kwa watu wasiojua ukweli wa maisha kuwa katika mambo wanayolaumu nao ni sehemu ya matokeo hayo. Kukosa kujua hili kunafanya kundi kubwa la watu mambo yanapotokea vibaya basi kutafuta wa kuwatwika lawama na wao wawe salama kuwa hawahusiki kwa chochote.
Jamii yetu ina watu wachache ambao mambo yakitokea yameenda vibaya basi wanajua kwa namna moja wamesababisha yawe hivyo na wana wajibu wa kufanya kitu kurekebisha, kukubali na kuandaa mpango wa kuchukua hatua ili kuepusha matatizo kama hayo wakati mwingine. Kufanya hivi ni kipimo cha ukomavu na ukuaji ndani ya mtu anapoachana na lawama bali kuwajibika na kuchukua hatua fulani dhidi ya jambo liliotokea.
Mara ngapi umekuwa mtu wa lawama na kulaumu watu ?, umejikuta katika kulaumu hujaongeza chochote zaidi ya kuharibu zaidi au pengine kutochukua hatua zozote zile maana anayelaumu hutaka kuonewa huruma na wengine. Ni mara ngapi tumekua hatuchukui hatua fulani katika maisha kwa kubaki kulaumu asingekuwa mtu fulani ningekuwa sehemu fulani, asingekuwa mtu fulani ningekuwa nimefanikiwa. Kulaumu kunafanya mtu awe mzembe na mvivu kufanya kazi akifikiria kwa kulaumu mambo yatabadilika yenyewe.
Lolote linalotokea jifunze kuangalia ni kwa namna gani na wewe umechangia utokeaji wake. Usibaki upande mmoja kulaumiwa bila kujua na wewe unachangia vipi hali hiyo hadi imejitokeza. Kuna sehemu ukitulia na kufikiria utaona na wewe unahusika katika utokeaji wa mambo mengi. Usiishie tu kulaumu haraka haraka bali angalia upande wako na kuwa tayari kuchukua hatua stahiki. Hili litakusaidia kuvuka vikwazo vya watu wengi wanalaumu tu bila kujua wajibu wao ni upi.
NA KOCHA MWL. JAPHET MASATU
WhatsApp + 255 716 924136 / + 255 755 400128
EMAIL : japhetmasatu@gmail.com
No comments:
Post a Comment