Sunday, October 7, 2018

KABLA YA KULALA IPIME SIKU YAKO

Kila siku tunayoishi ni nafasi nzuri kwetu kuwa bora zaidi, kwa sababu kuna mengi tunakutana nayo ya kujifunza, kuna makosa tunayoyafanya na yapo mazuri tunayafanya pia. Wengi wamekuwa wanakosa nafasi ya kuzitumia siku zao kuwa bora zaidi kwa sababu hawapati muda wa kutafakari kila siku yao.
Kupitia Ustoa, tunashauriwa kuipima na kutafakari kila siku yetu kabla ya kulala. Na hapa ndipo tunapata nafasi ya kujifunza na kujiandaa kuwa bora zaidi kwenye siku inayofuata.
Jioni unapoimaliza siku yako, usikimbilie tu kulala na kuona siku imeisha, badala yake unahitaji kuwa na tahajudi ambayo utaipitia siku yako yote.
Kwenye tahajudi hii, pitia siku yako nzima, kwa kufikiria kila ulichofanya kwenye siku yako, kila uliyekutana naye na mawazo na hisia ulizokuwa nazo siku nzima.
Kisha jiulize na kujijibu maswali haya matatu;
Moja; vitu gani umefanya vibaya? Katika yale uliyofanya kwa siku nzima, je vitu gani umefanya kwa ubaya au kwa njia ambazo siyo sahihi?
Mbili; vitu gani umefanya vizuri? Katika vitu vyote ulivyofanya kwa siku nzima, vipi ambavyo umevifanya kwa uzuri, ni kwa namna gani umeishi misingi na tabia za ustoa?
Tatu; Vitu gani utakwenda kufanya tofauti? Ni vitu gani unahitaji kuvifanya kwa utofauti ili kuweza kuishi kulingana na msingi na tabia za ustoa?
Kwa kujiuliza na kujipa majibu ya maswali hayo matatu, utaweza kujipima kwa kila siku yako, na pia kujiandaa vyema kwa siku inayofuata. Pia utaepuka kurudia makosa uliyofanya kwa siku husika.
Kauli ya Epictetus kwenye tahajudi ya jioni;
“Allow not sleep to close your wearied eyes, Until you have reckoned up each daytime deed: “Where did I go wrong? What did I do? And what duty’s left undone?” From first to last review your acts and then Reprove yourself for wretched [or cowardly] acts, but rejoice in those done well.”
(Discourses, 3.10.2–3)
Anasema usikubali usingizi ufumbe macho yako kabla hujahesabu kila tendo ulilofanya kwenye siku yako. kipi umekosea, kipi umefanya vizuri na kipi ambacho hujakamilisha. Kuanzia tendo la kwanza mpaka la mwisho, jikaripie kwa yale uliyofanya vibaya na jisifie kwa yale uliyofanya vizuri.

No comments:

Post a Comment