Sunday, October 7, 2018

FANYA KILICHO SAHIHI, LAKINI USITEGEMEE CHOCHOTE.

Moja ya sababu zinazopelekea wengi kukosa furaha ni kufanya vitu ambavyo wanajua siyo sahihi, lakini kwa sababu wengine wanafanya au wanawategemea wafanye, basi wanafanya ili kuwaridhisha wengine. Hatari nyingine kubwa ni watu kufanya kitu wakitegemea matokeo fulani yatokee. Yaani unachukua hatua, ukitegemea matokeo fulani ili uwe na furaha. Hii ni njia ya kujitengenezea kushindwa na kujinyima furaha.
Cicero ana haya ya kutuambia kuhusu kufanya na kutegemea;
The wise person does nothing that he could regret, nothing against his will, but does everything honourably, consistently, seriously, and rightly; he anticipates nothing as if it is bound to happen, but is shocked by nothing when it does happen …. and refers everything to his own judgement, and stands by his own decisions. I can conceive of nothing which is happier that this. – Cicero, Tusculan Disputations 5.81
Mtu mwenye hekima hafanyi chochote atakachoweza kujutia, hafanyi chochote kinyume na matakwa yake bali anafanya kila kitu kwa heshima, msimamo, umakini na usahihi; hategemei chochote kitatokea kwa yeye kufanya, lakini pia hashangazwi na chochote kinachotokea, na anarejea kila kitu kwa maamuzi yake mwenyewe na kusimamia maamuzi hayo. Hakuna kitu chenye furaha kama kuishi kwa namna hii.
Kama ambavyo Cicero anatuambia, furaha siyo kitu unachokipata kutokana na kupata vitu fulani au kuwa kwenye hali fulani kama wengi wanavyofikiri.
Bali furaha ni matokeo ya maisha unayoishi na namna unavyofanya mambo yako. Kama unafanya kile kilicho sahihi mara zote, ukawa na msimamo na kufanya kwa umakini na usahihi, utapata matokeo mazuri. Na kama hufanyi ukitegemea matokeo mazuri, matokeo yoyote yatakayotokea hayatabadili chochote kwenye furaha yako, kusudi lako wewe ni kufanya kwa usahihi na siyo kulazimisha matokeo unayotaka wewe. Fanya maamuzi yako na yasimamie kwenye maisha yako, hili litakupa furaha kuliko kuhangaika na kukosa msimamo.

No comments:

Post a Comment