Monday, October 8, 2018

TARAJIA MABAYA NA MAGUMU, KUWA MSTAHIMILIVU.

Maisha siyo rahisi, hakuna chochote kwenye maisha yako kitaenda kama ulivyopanga. Utakutana na magumu na changamoto ambazo zitakuangusha na kujaribu kukukatisha tamaa. Ili uweze kufanikiwa, ili uweze kupata chochote unachotaka, unapaswa kuwa mstahimilivu, unapaswa kuwa mgumu, unapaswa kuwa kinga’ang’anizi na unapaswa kutokujua kabisa msamiati unaoitwa kushindwa au kukata tamaa.
Falsafa ya ustoa inatujenga tuwe wastahimilivu kwa kutuandaa kukutana na magumu na hata kuweza kuyavuka bila ya kukata tamaa.

Ili kuzuia mabaya yanayotokea yasituvuruge, tunapaswa kuwa na maandalizi ya mabaya na magumu yanayoweza kutokea.

Kama wastoa tunaweza kujiandaa na magumu kwa njia mbili. Njia ya kwanza ni kuishi magumu yenyewe, kujiweka katika nyakati ngumu hata kama hujafikia ugumu huo. Kufanya kama vile huna kitu fulani, hata kama tayari unacho. Kwa njia hii, hutashtushwa pale kile ulichokuwa unategemea kitakapokuwa hakipatikani.
Njia ya pili ni kujijengea taswira ya magumu kabla hayajatokea. Unapopanga chochote, usiangalie tu yale mazuri unayotegemea yatokee, bali pia jenga taswira ya mabaya yanayoweza kutokea. Jiulize kipi kibaya kabisa kinachoweza kutokea, kisha pata picha kwamba kitu hicho kimetokea na ona utawezaje kukabiliana nacho. Zoezi hili la kujijengea taswira ya mabaya linakufanya usipatwe na mshangao pale unapokutana na magumu, kwa sababu ulishapata picha ya magumu hayo. Pia kwa sababu  hutapata magumu makubwa kabisa, utajiambia ulishaona magumu zaidi ya uliyokutana nayo, hivyo hayakusumbui.
Marcus anatuambia;
Be like the headland, on which the waves break constantly, which still stands firm, while the foaming waters are put to rest around it. ‘It is my bad luck that this has happened to me.’ On the contrary, say, ‘It is my good luck that, although this has happened to me, I can bear it without getting upset, neither crushed by the present nor afraid of the future.’ This kind of event could have happened to anyone, but not everyone would have borne it without getting upset. – Marcus Aurelius, Meditations, 4.49
Kuwa kama ukingo wa mto au bahari ambao unapigwa na mawimbi ya maji kila mara lakini unaendelea kusimama imara na kuyatuliza mawimbi ya maji. Chochote kibaya kinapotokea, usijiambie nina bahati mbaya hiki kimetokea kwangu, badala yake jiambie nina bahati nzuri hiki kimetokea kwangu kwa sababu nitaweza kukikabili bila ya kukasirika au kuumizwa nacho kwa sasa au wakati ujao. Kitu kama hicho kingeweza kutokea kwa yeyote, lakini siyo kila mtu anaweza kukipokea kwa utulivu.

Pia Seneca anatukumbusha kuishi kila siku yetu kama ndiyo siku ya mwisho kwenye maisha yetu;
Glad and cheerful, let us say, as we go to our rest: ‘I have finished living; I have run the course that fortune set for me’. If God gives us another day, let us receive it with joy. The happiest person, who owns himself more fully, is the one who waits for the next day without anxiety. Anyone who can say, ‘I have had my life’ rises with a bonus, receiving one more day. – Seneca, Letters, 12.9.

Kila unapoimaliza siku yako jiambie kwa furaha na uchangamfu nimemaliza kuishi, nimemaliza mwendo ambao asili imenitengenezea. Kama Mungu atanipa tena siku nyingine, nitaipokea kwa furaha. mtu mwenye furaha anajimiliki yeye kwa ujumla, anaisubiri siku nyingine bila ya wasiwasi. Yeyote anayejiambia nimeyamaliza maisha yangu, anapata zawadi ya siku nyingine tena ya kuishi.

1 comment: