Wednesday, July 17, 2019

UKOSEFU WA ELIMU YA MSINGI YA FEDHA HUTUPELEKEA KUWA MASKINI . JIFUNZE HAYA USIYOYAJUA KUHUSU ELIMU YA MSINGI YA FEDHA.

( 1 ).FEDHA SIYO MAKARATASI.
Watu wengi wamekuwa wanafikiria fedha ni yale makaratasi au sarafu ambazo tunazishika. Na hapa ndipo wengi wanapokwama, kwa sababu wanakosa ule msingi muhimu kuhusu fedha. Kwa kukosa msingi muhimu kuhusu fedha, watu wanashindwa kuzipata kwa wingi na hata kuzitumia vizuri.
Fedha ni wazo ambalo lina thamani. Fedha ni matokeo ya mtu kuwa na wazo ambalo linaongeza thamani kwa wengine. Bila ya thamani hakuna fedha. Hivyo kama unataka fedha zaidi, lazima ujue thamani gani unatoa kwa wengine.

( 2 ).KIPATO KIMOJA NI UTUMWA.
Kuwa na chanzo kimoja cha kipato pekee ni utumwa. Huwezi kuondoka kwenye umasikini kama unategemea kipato chako kitoke sehemu moja pekee. Kama umeajiriwa pekee, hata kama unalipwa kiasi kikubwa cha fedha, bado unabaki kwenye umasikini. Kama unafanya biashara na unategemea wateja wachache nayo pia inakuweka kwenye umasikini.
Utaondoka kwenye umasikini kwa kuwa na vyanzo vingi vya kipato. Bahari huwa haikauki kwa sababu mito mingi inaishia kwenye bahari. Hiyo kama unataka usikaukiwe na fedha, kuwa na vyanzo vingi vya kipato.

(3) MATUMIZI NI BOMU.
Watu wengi wamekuwa wanaanza maisha na kipato kidogo, na yanaenda. Kipato kinaongezeka na matumizi yanaongezeka, kila kipato kinapoongezeka na matumizi pia yanaongezeka. Matumizi ni bomu kama hayatadhibitiwa. Matumizi yana tabia ya kuongezeka pale tu kipato kinapoongezeka.
Huwezi kuondoka kwenye umasikini kama huwezi kuyadhibiti matumizi yako. Haijalishi unatengeneza kipato kikubwa kiasi gani, matumizi ni bomu, usipolitegua litakulipua.

( 4 ).MADENI NI UTUMWA.
Umesikia hapo, na najua huenda kimoyomoyo unakataa, unajiambia siyo kweli, kwa sababu huenda umeshalishwa sumu kwamba bila madeni maisha hayawezi kwenda. Unajua nini, wale wanaonufaika na madeni ndiyo wanasambaza propaganda za aina hiyo. Madeni ni utumwa, na huwezi kuondoka kwenye umasikini kama huwezi kuondokana na madeni.
Kuna madeni mazuri na mabaya, na masikini wote huwa wapo kwenye madeni mabaya. Madeni mabaya ndiyo yanawafanya watu kuwa watumwa, wanajikuta wanafanya kazi sana kulipa madeni, halafu wanakopa tena. Kwa hiyo maisha yao yote yanakuwa mzunguko wa kopa, lipa, kopa tena.

( 5 ).BIASHARA NI MKOMBOZI.
Zile zama za nenda shule, soma kwa bidii, faulu na utapata kazi nzuri na inayolipa zimeshapitwa na wakati. Kila mtu anaona wingi wa watu wenye sifa za kuajiriwa, lakini hakuna nafasi za ajira. Na hata walioajiriwa, mazingira ya kazi na hata kipato wanachoingiza hakiridhishi.
Kwa zama tunazoishi sasa, mkombozi pekee, kitu pekee kitakachokuwezesha kuwa na maisha mazuri ni kuwa na biashara yako. Hivyo ni muhimu sana uwe na biashara kama unataka kutoka kwenye umasikini.

( 6 ). UWEKEZAJI NI KIJAKAZI WAKO.
Inapokuja kwenye fedha, kuna mambo mawili, kuna kuifanyia kazi fedha, pale ambapo inabidi ufanye kazi ndiyo fedha iingie. Halafu kuna fedha kukufanyia kazi wewe, ambapo fedha inaingia hata kama hufanyi kazi moja kwa moja.
Ili kuondoka kwenye umasikini na kufikia uhuru wa kifedha, ni lazima fedha ziwe zinakufanyia kazi wewe. Na hapa ndipo unapohitaji kuwa na uwekezaji, ambao unafanya kazi ya kuuzalishia fedha, hata kama wewe umelala.
( 7 ). KODI NI UWEKEZAJI.
Kodi ni gharama unayolipa kwa kuishi kwenye jamii iliyostaarabika. Ni kodi tunazolipa ndiyo zinazoleta huduma mbalimbali tunazozitegemea kwenye jamii. Huduma za afya, huduma za elimu, ulinzi na usalama, miundombinu kama barabara na mengineyo ni matokeo ya kodi tunazolipa.
Hivyo kodi ni uwekezaji ambao kila mmoja wetu anapaswa kuufanya ili tuwe na jamii bora. Tunapaswa kuondokana na dhana potofu kwamba kodi ni kitu kibaya. Kwa sababu hebu pata picha, umekazana kutafuta fedha na ukawa tajiri, halafu unaishi sehemu isiyo salama, je utaweza kufurahia utajiri wako?
(  8 ).BIMA NI MKOMBOZI.
Kuna hatari mbalimbali ambazo zinatuzunguka kwenye maisha, na kadiri unavyopiga hatua kifedha, ndivyo hatari zinakuwa kubwa zaidi. Hili limekuwa linazua hofu kwa wengi na wakati mwingine kuwazuia hata kufanikiwa.
Ili kuondokana na hatari zinazokuzunguka na kukuzuia kuanguka pale unapokutana na changamoto kubwa, unapaswa kuwa na bima. Kwa bima unachangia kiasi kidogo cha fedha, lakini unapopata tatizo, unalipwa kiasi kamili cha fedha au mali ulizopoteza.

( 9 ). WATOTO WAKO HAWAHITAJI FEDHA ZAKO.
Wazazi wengi wamekuwa wanakazana kutafuta fedha na mali kwa wingi, ili kuwaachia watoto wao urithi na wasiwe na maisha magumu. Lakini wote tumekuwa tunaona nini kinatokea baada ya wazazi hao kufariki, utajiri na mali zote zinapotea, kwa kutumiwa vibaya na watoto walioachwa.
Watoto wako hawahitaji sana fedha wala mali zako, bali kikubwa wanachohitaji ni msingi muhimu wa kufuata na kusimamia inapokuja kwenye swala la fedha. Kuliko uwape watoto fedha bila ya misingi, ni bora uwape misingi bila ya fedha. Kwa sababu misingi itawawezesha kupata fedha zaidi wakati fedha pekee bila misingi zitapotea.

( 10 ). KUTOA NI UWEKEZAJI.
Mmoja wa watu matajiri sana kuwahi kuwepo hapa duniani, John D. Rockefelar amewahi kunukuliwa akisema unatumia nusu ya kwanza ya maisha yako kukusanya fedha, halafu nusu ya pili unaitumia kuzigawa fedha hizo kwenda kwa wengine.
Moja ya vitu vinavyowafanya matajiri kuendelea kuwa matajiri ni utoaji. Matajiri wengi wamekuwa watoaji wa misaada mbalimbali ya kijamii na hilo limekuwa linawasukuma kufanikiwa zaidi kifedha. Hivyo kutoa ni uwekezaji ambao unamlipa sana mtu baadaye.

No comments:

Post a Comment