Moja; anza na chochote unachojali sana.
Watu
wengi wamekuwa wanafikiria kwamba ili uweze kuleta mabadiliko makubwa
kwako na kwa wengine basi inabidi uwe na wazo kubwa na la kipekee sana.
Wazo ambalo wengine hawajawahi kuwa nalo. Huo siyo ukweli, unaweza
kuanza na wazo lolote na ukaweza kulijenga kwa utofauti na
ukajitofautisha sana.
Anza
na chochote unachojali, unachopenda, unachoamini, unachojua, ulichozoea
au ambacho umesomea. Chochote kile ambacho unaona kinaweza kuwa bora
zaidi ya kilivyo sasa, unaweza kukichukua kama wazo lako la kufanyia
kazi.
Mbili; uliza maswali ambayo hayaulizwi.
Watu
wamekuwa wanafanya mambo kwa mazoea kwa sababu wanafanya kile ambacho
kila mtu anafanya, na hawathubutu kujaribu vitu vya tofauti. Sasa kwa
wazo unalotaka kufanyia kazi kuliboresha zaidi, anza kwa kuuliza maswali
ambayo watu wengine hawaulizi.
Maswali
hayo yanaweza kuwa, vipi kama.... vipi kinyume cha... Hapa unajaribu
kupata picha ya tofauti na wengi walivyozoea, kwa kuona upande wa pili
wa vitu au kwa namna ya tofauti.
Tatu; angalia uzoefu wako binafsi.
Baada
ya kujiuliza maswali ya tofauti kwenye wazo unalotaka kufanyia kazi,
angalia uzoefu wako binafsi kwenye wazo hilo. Usijidharau kwa sababu
labda huna elimu kubwa au uzoefu mkubwa kwenye jambo hilo. Labda siku za
nyuma umewahi kujaribu kufanya tofauti na ukapata matokeo ya tofauti,
hiyo inatosha kukuonesha kwamba kuna uwezekano wa kupata matokeo tofauti
na ambayo watu wanapata sasa.
Nne; chagua eneo la ubobezi kwenye wazo lako.
Wazo
unalokuwa nalo linaweza kuwa pana, sasa unahitaji kuchagua eneo ambalo
utabobea kwenye wazo hilo ili kujitofautisha kabisa na wengine. Badala
ya kutaka kufanya kila kitu, unachagua eneo moja ambalo utaweka muda na
nguvu zako na kuweza kutengeneza ubobezi mkubwa. Ni kupitia ubobezi huu
ndiyo unaweza kupiga hatua kubwa kwenye wazo hilo.
Tano; fanya utafiti.
Watu
wengi wamekuwa wanapata mawazo mapya ya kuboresha zaidi, lakini
hawanufaiki nayo kwa sababu huwa hawaweki kazi inayopaswa kuwekwa ili
mtu kubobea kwenye kitu hicho. Moja ya kazi kubwa unayopaswa kuweka ni
kufanya utafiti. Siyo kusoma tafiti, badala yake kufanya utafiti mpya,
kwa kuangalia yale maeneo ambayo unataka yawe bora kisha kuja na njia
bora za kuyaboresha kutoka kwenye tafiti mbalimbali zinazogusa wazo
hilo.
Sita; unganisha mawazo.
Kuna
maeneo mengine ambayo yameweza kupiga hatua kubwa, ambayo ni tofauti na
wazo unalofanyia kazi wewe. hii haikuzuii wewe kujifunza kutoka maeneo
hayo. Jifunze kupitia maeneo mbalimbali kwa hatua ambazo watu wameweza
kupiga, kisha unganisha mawazo hayo na wazo unalofanyia kazi kuweza
kuona jinsi gani ya kuboresha wazo unalofanyia kazi. Kumbuka misingi ya
mafanikio kwenye kila eneo inafanana, hivyo kwa kuangalia jinsi ambavyo
mawazo mengine yamefanikiwa, utaweza kufanikisha wazo lako pia.
Saba; tengeneza nguzo ya kubeba wazo lako jipya.
Baada
ya kuchagua wazo unalotaka kuboresha, ukauliza maswali ya tofauti,
ukatumia uzoefu wako, ukafanya utafiti na hata kujifunza kutoka maeneo
mengine, unakuwa umejifunza mambo mengi sana kuhusiana na wazo lako
jipya. Hapa unakuwa na maarifa na taarifa nyingi ambazo mtu mwingine
siyo rahisi kuyaelewa. Hivyo ili wazo lako la kuboresha liweze kueleweka
na kutumiwa na wengine, unahitaji kutengeneza nguzo ya kubeba wazo
lako. Hapa unatengeneza mfumo unaobeba wazo lako jipya, kwa namna ambayo
watu wengine wanaelewa jinsi linavyofanya kazi na matokeo ya tofauti
yanavyopatikana.
Kwa
hatua hizo saba, unakuwa umekamilisha wazo lako la tofauti, ambalo
linaleta matokeo bora kuliko yale ambayo yamezoeleka. Baada ya hapo sasa
unakwenda kwenye hatua ya pili ambayo ni kujenga wafuasi kwenye wazo
lako.
No comments:
Post a Comment