Tuesday, October 16, 2018

WAZAZI HUKWAMISHA AU KUENDELEZA VIPAJI VYA WATOTO WAO.

9 Oktoba 2018
Mzazi ana nafasi kubwa sana katika kuendeleza kipaji cha mtoto

Kipaji ni uwezo wa kuzaliwa nao wa kufanya jambo fulani kwa ngazi ya juu bila kufundishwa au baada ya kufundishwa kidogo tu. Kipaji kinaweza kuwa cha kimwili au cha kiakili lakini pia kinaweza kuendelezwa au kudumazwa.
Mzazi ni mtu wa kwanza anayeweza kutambua uwezo ama kipaji cha mtoto wake. Hata hivyo ana fursa ya kuendeleza au kutokukiendeleza kipaji cha mtoto.

Baadhi ya wazazi hutambua vipaji vya watoto mapema na kuanza kuviendeleza kwa kuwapatia nyenzo mbali mbali ambazo huwasaidia katika kuboresha uwezo walio nao.

Lakini pia wapo wazazi ambao wanamalengo yao juu ya ni kitu gani wanapenda watoto wao wafanye. Ama yamkini hawana ufahamu wa nini cha kufanya ili kumwendeleza mtoto mwenye kipaji .Hata hivyo vipo baadhi ya vipaji ambavyo wazazi huona ni upotevu tu wa maadili mfano kuimba na kucheza mziki.

BBC imezungumza na mama Ritha, mama mwenye watoto wanne. Anasema kwa kiasi kikubwa baadhi ya wazazi na hata yeye mwenyewe kipindi cha nyuma walikwamisha sana watoto sababu walikuwa hawatambui kama kipaji pia ni njia salama ya kumwezesha mtoto kimaisha.
"Wazazi wengi huwa hawajuagi tena zamani tulikuwa tunaona watoto wanapotea kabisa. Mi binti yangu wa kike alikua anapenda kuandika nyimbo za wasanii wa marekani na hata za kwake mwenyewe kwenye daftari lake afu kukiwa na sherehe yeye ndo mwimbaji. Nikaona anapotea nlikua na mchapa na nlimwambia akifika chuo kikuu ndo afanye uo mziki lakini si nyumbani kwangu maana hata baba yake alikuwa hapendi kabisa," Mama Ritha anaiambia BBC
Hata hivyo ameongeza kuwa wazazi pia huwanyima fursa za kujifunza watoto kwani kila akishika kitu mzazi hupiga kelele mtoto aache kwa madai kwamba ataumia.
Hata hivyo wapo baadhi ya watoto ambao wamepewa msaada mkubwa na wazazi wao katika kuboresha na kuendeleza vipaji vyao.

BBC imezungumza na mwanadada mpambaji Plaxeder Jumanne au baby precious kama anavyojulikana katika kazi zake za upambaji, anasema mama yake ndio mtu wa kwanza kumshauri ageuze kipaji chake kuwa biashara huku akimnunulia vifaa orijino vya urembo.

"Mie nlikuwa nawachukua watoto wenzangu nawapamba nlikua napenda sana urembo kama mama yangu. Hata nilipo kuwa nikaanza kuwapamba watu. Nilikuwa natumia vifaa feki hivi vya bei rahisi lakini mama yangu alianza kwa kuninunulia vifaa orijino kabisa. Na huwezi amini nilikua nampamba yeye na kumfuta kabla sijapata wateja tena nimejifunza kufunga maremba ya kinaijeria kichwani kwa mama na alikuwa ananisaidia sana, sasa hivi nasafiri hadi mikoani na kupamba watu mbali mbali hadi watu maarufu na nimepata pesa nikanunua vifaa vingi sana Orijino," Plaxeda anaiambia BBC.

Hata hivyo manadada huyo anasema kwa sasa mama yake ametangulia mbele za haki tangu mwaka jana ila bado anamshukuru kwa sababu hivi sasa kazi ya upambaji inampa pesa kuliko ajira yake na imemwezesha kufungua biashara zingine.

"Mimi sijajitangaza sana ila kupitia vifaa alivyonianzishia navyo mama yangu nikawa napamba hadi maharusi na wasimamizi wao. Na kipaji hiki kimenipa pesa ninafanya biashara ya kutengeneza nywele hasa mawigi na pia kufungua biashara ya nguo. Mama yangu angekuwepo angefurahi sana ila naamini anaona. Nimewaremba baadhi ya wasanii wa Tanzania. Safari ndo inaanza," Plaxeder anaiambia BBC.


Mwanaharakati wa masuala mbali mbali ya kibinadamu Shahista Alidina maarufu kama Shaykaa, anasema baadhi ya wazazi hupenda kutimiza ndoto zao kupitia watoto na mwishowe huwakwamisha.

"Unakuta mzazi kama alishindwa kuwa mwanasheria au daktari kama alivyotaka huko nyuma atataka mtoto wake afuate ndoto hiyo. Hawataki kuwapa uhuru watoto wafuate wanavyopenda. Unakuta kipaji cha mtoto kinaweza mletea kipato cha kutosha tu ila mzazi anampa mtoto shinikizo la kufaulu tu shule awe namba moja, mbili au tatu na ndiomaana unaona watoto wengine hadi wanajiua. Wanawanyima fursa watoto kufanya vitu wanavyovipenda," Shaykaa anaiambia BBC.

Hata hivyo anaongeza kuwa kunachangamoto nyingine kwa wazazi kupangia kazi watoto kuwa hii ni ya wanawake au hii ni ya wanaumena kujenga uoga kwa watoto na kuwanyima fursa ya kujituma zaidi.

"Kusoma kwa mtoto ni muhimu ila kuna muda wa ziada na kuna maisha nje ya darasa. Unakuta mtoto wa kike anapenda kucheza mpira, lakini mzazi atapinga kuwa huu ni mchezo wa wanaume mwanamke hatakiwi, sasa hapo moja kwa moja mzazi atakuwa ameua kabisa kipaji cha mtoto kama mtoto atakosa fursa ya kujiendeleza huko mbele," anasema Shaykaa
Mwanaharakati huyo pia amewaasa wazazi kuhakikisha wanawasaidia watoto kujiendeleza kijamii.

"Mtoto ni muhimu awe na maisha yake pia, na tutambue kuwa na wao ni binadamu wala si wafungwa. Ni muhimu ndio kufuata dini na misingi bora ya maisha pamoja na mila na desturi lakini tusisahau kuwa mtoto anapofikia umri wa kujielewa anahaki ya kufanya maamuzi kuwa anapenda nini ilimradi ni jambo jema kisheria, kidini, kiafya na kijamii. Tuwe marafiki kwao lakini tusiwapotoshe watoto wetu, Shaykaa anaiambia BBC.

No comments:

Post a Comment