Monday, October 8, 2018

ACHA KUWA KARANI WA FEDHA ZAKO, JILIPE WEWE KWANZA

 Wapo watu wengi ambao wanakuwa na mipango mizuri sana kabla hawajawa na fedha, wanajua kabisa wakipata fedha watafanya nini na nini. Na tena watawashangaa sana wale wanaopata fedha na kuzitumia vibaya. Lakini subiri watu hao hao wazipate fedha, mipango yote inayeyuka, fedha zinatumika hovyo na mpaka zinapoisha ndiyo akili zinawarudia.

Kitu kimoja ambacho nataka kushauri leo kwa wale wote wenye shida ya kukaa na fedha, ni hiki; ACHA KUWA KARANI WA FEDHA ZAKO.
Watu wengi linapokuja swala la fedha, hawana tofauti na makarani, ambao wanapokea fedha na kuzipelekeka zinapopaswa kwenda. Ukienda benki kuweka fedha na ukamkabidhi karani wa benki fedha zako, utaona kama anashika fedha nyingi, lakini mwisho wa siku fedha hizo habaki nazo yeye, bali anakabidhi zinapohusika.

Sasa watu wengi wamekuwa wanayaishi maisha yao kama makarani wa fedha zao. Kinachotokea ni hiki, mtu anafanya kazi au biashara na analipwa mshahara au kupata faida kama kipato chake. Anachukua kipato hicho na kwenda kulipia vitu na kununua vitu mbalimbali. Mwisho anabaki hana fedha kabisa.

Alichokifanya mtu huyu ni kuchukua fedha kwenye kazi au biashara na kwenda kuitoa kwa wale wanaomdai au wanaouza vitu mbalimbali. Mwisho wa siku anabaki hana hata senti moja.

Acha mara moja kuwa karani wa fedha zako, kwa kuzihamisha kutoka unakozipata na kuzipeleka kwenye matumizi na wewe kubaki huna kitu.
Na ipo njia moja rahisi kwako kuacha kuwa karani wa fedha zako, njia hiyo ni KUJILIPA WEWE MWENYEWE KWANZA.

Kwa kila kipato unachoingiza kwenye maisha yako, kabla hujapeleka kwenye matumizi yoyote, toa sehemu ya kipato hicho na iweke pembeni. Sehemu hiyo ya kipato uliyoitoa ndiyo malipo yako kwako na hupaswi kuitumia kwa shughuli nyingine yoyote ya matumizi. Hichi ni kipato ambacho utakiwekeza zaidi ili uweze kufanikiwa zaidi.

Sasa najua ni vigumu kukaa na fedha, kwa sababu kama wanavyosema watu, fedha huwa hazikosi matumizi. Ukishakua na fedha, dunia itahakikisha unazitumia kwa namna yoyote ile. Hivyo vitu vitaharibika, watu wataumwa utashangaa unapokuwa na fedha ndiyo unapokea simu nyingi zikitaka utoe msaada fulani.

Hivyo kuna njia nyingine bora kabisa ya kuhakikisha kile unachojilipa hakipati matumizi na ukakipoteza. Njia hiyo ni KUJENGA GEREZA LA AKIBA YAKO. Kile kiasi ambacho unajilipa wewe mwenyewe, kitengenezee gereza, ambapo ukishaingiza, huwezi kutoa tena, hata itokee nini. Hata uwe na dharura kiasi gani, gereza hilo halikuruhusu uondoe fedha ulizoweka.

Gereza la fedha zako ni mfumo wowote unaokuruhusu kuweka fedha lakini kutoa inakuwa siyo rahisi. Na unaweza kufanya hivyo kwa kuwa na akaunti maalumu ya benki ambayo inakuruhusu kuweka lakini siyo kutoa. Unaweza pia kufanya uwekezaji wa moja kwa moja ambao utafanya kupata fedha yako kuchukue muda. Lakini pia unaweza kuweka mpango na mtu au watu wengine, na mkawa mnaweka fedha lakini hamtoi.
Angalia njia inayokufaa wewe, ambapo ukiweka fedha, inakuwa vigumu sana kwako kuitoa, na hilo litakusaidia kujiwekea fedha zako kulingana na mipango uliyonayo.

Hivyo nimalize kwa kukumbusha mambo muhimu sana tuliyojadili hapa;
ACHA KUWA KARANI WA FEDHA ZAKO.
JILIPE WEWE MWENYEWE KWANZA.
TENGENEZA GEREZA LA FEDHA ZAKO.
Fanya hayo matatu na fedha yako itaweza kutulia, na utaweza kufanya makubwa. Ukishaweza kuituliza fedha yako, utaweza kuiwekeza na kupitia uwekezaji ndiyo utaweza kufikia utajiri na uhuru wa kifedha.

No comments:

Post a Comment