Friday, June 14, 2019

KILA HATUA UNAYOPIGA HUZALISHA KIKWAZO

Kwenye fizikia, kuna kanuni tatu kuu za mwendo ambazo mwanasayansi Isaac Newton alizigundua.
 
Kanuni ya kwanza inasema kitu kilichopo kwenye mwendo kinaendelea kuwa kwenye mwendo mpaka nguvu ya nje itakapotumika kukizuia.
 
Kanuni ya pili inasema nguvu ya kitu kilichopo kwenye mwendo inategemea uzito wake na mwendokasi wake.
 
Na kanuni ya tatu inasema kila mwendo huwa unazalisha upinzani.
 
Ni kanuni ya tatu ambayo tunakwenda kuijadili hapa kwenye dakika moja ili uelewe kwa nini baadhi ya vitu vinatokea kwenye maisha yako na hatua sahihi kwako kuchukua.
 
Kila mwendo unaoanzisha, kuna mwendo mwingine utakaoanzishwa kuzuia mwendo huo.
 
Unapojaribu kwenda mbele, kuna mtu atajitokeza kukurudisha nyuma.
 
Hii ndiyo inasababisha mafanikio kuwa magumu. Kwa sababu siku unayoamua kwamba unataka kufanikiwa, zitaibuka kila aina ya nguvu kukupinga, kutaibuka kila kikwazo kwenye njia yako ya mafanikio.
 
Unapojua hili, unajipanga kwa upinzani kwa kila hatua unayopanga kupiga na hujidanganyi kwamba mambo yataenda vizuri yenyewe kama wengi wanavyofanya.
 
Usishangae pale ambapo marafiki ulionao sasa watageuka kuwa maadui zako pale unapotangaza kwamba unataka kufanikiwa sana. ulipokuwa kawaida mlikuwa marafiki, unapopanga kupiga hatua zaidi wanakuwa maadui, hiyo ni kanuni ya asili, huwezi kupingana nayo.
 
Usikubali kipingamizi chochote kikuzuie wewe kupiga hatua zaidi kwenye maisha yako, jua kwa kila hatua utakayopanga kuchukua kuna kipingamizi kitaibuka na hivyo jiandae kukivuka.

No comments:

Post a Comment