Wednesday, June 12, 2019

JE, WAJUA BIASHARA NI KAMA KIUMBE ?? HUZALIWA , HUKUA , HUDUMAA NA KUFA ?

" BIASHARA "  ni kiumbe hai, ambacho kinazaliwa, kinakua au kudumaa na mwishowe kinakufa. Biashara ni kitu ambacho kina maisha yake ya kujitegemea na jinsi ambavyo kinapewa uhuru wake ndivyo inavyofanikiwa zaidi.
Lakini pia biashara huwa inakuwa na tabia zake, ambazo zinaweza kuifanya ifanikiwe zaidi au kuizuia isifanikiwe. Tabia hizi za biashara huwa zinatokana na tabia ambazo mwanzilishi wa biashara hiyo anazo

Na hii ndiyo maana kwenye kila biashara kuna utaratibu na utamaduni fulani uliopo, ambao huwa ni mgumu sana kubadilisha. Hata wafanyakazi wapya wanapokuja kufanya kazi kwenye biashara hiyo, baada ya muda hujikuta wameshavaa utamaduni huo wa biashara.

Utaratibu na utamaduni uliojengeka kwenye biashara nyingi huwa ni matokeo ya tabia za mwanzilishi wa biashara, huwa siyo kitu ambacho kimetengenezwa kwa makusudi ambacho kinaweza kuwa na msaada kwenye biashara hiyo.

Hivyo unakuta biashara imejijengea tabia ambazo siyo nzuri na zinakuwa kikwazo kwa maendeleo ya biashara hiyo. Ukiangalia tabia za biashara hiyo, zinakuwa zinaendana sana na tabia za mwanzilishi wa biashara hiyo.

Mfano kama mwanzilishi wa biashara ni mzito kwenye kufanya maamuzi, basi ufanyaji wa maamuzi wa kila mtu kwenye biashara unakuwa ni mzito sana. Maamuzi hayafanyiki kwa wakati na biashara inazikosa fursa nzuri za kukua zaidi.

Kama mwanzilishi wa biashara hawezi kupangilia vitu vyake vizuri kwenye maisha yake binafsi, unakuta biashara nayo haina mpangilio mzuri, vitu vipo hovyo hovyo na hakuna utaratibu wowote unaotumika kwenye kufanya vitu.

Kama mwanzilishi wa biashara ana tamaa, biashara nzima inaendeshwa kwa tamaa, kila aliyepo kwenye biashara hiyo anakuwa na tamaa na kujali mambo yake zaidi kiliko ya biashara.

Hivyo popote ambapo biashara imekwama, kwa hakika ndipo ambapo mmiliki wa biashara hiyo amekwama. Biashara haiwezi kukua zaidi ya ukuaji wa mmiliki wa biashara hiyo.

1 comment:

  1. Suluhisho pekee la changamoto hii ya biashara kuwa na tabia zinazoizuia kukua, ambazo zimetoka kwa mwanzilishi wa biashara hiyo ni kuwa na mfumo sahihi wa kuendesha biashara.

    Biashara inapoendeshwa kwa mfumo, inakuwa na tabia zake yenyewe ambazo ni bora na haziathiriwi na tabia binafsi za mmiliki wa biashara au mfanyakazi anayefanya kazi kwenye biashara hiyo.

    Mfumo unaweka nafasi za kazi na majukumu ambayo mtu anapaswa kuyatekeleza. Lakini pia mfumo unaeleza jinsi ambavyo mtu anapaswa kutekeleza majukumu hayo.

    Hivyo mtu yeyote anapokuwa kwenye biashara hiyo, anategemewa kufanya na kuzalisha matokeo ya aina moja, ambayo yanasimamiwa na mfumo.

    Rafiki, kama unataka biashara yako isiathiriwe na tabia zako binafsi, kama unataka kuacha kuwa kikwazo kwenye ukuaji wa biashara yako kama ulivyo sasa, suluhisho ni mfumo.

    ReplyDelete