Saturday, September 22, 2018

KILA MTU APAMBANE NA HALI YAKE,USINUNUE MATATAIZO YA WATU.

Chukua mfano una ndugu wa karibu au mtoto ambaye bado hajaweza kutengeneza maisha yake vizuri, lakini wewe maisha yako yameshakaa vizuri. Yeye hana kazi na ni mlevi. Hivyo unaamua kumsaidia awe na kipato, kwa sababu maisha yake siyo mazuri. Unampa mtaji wa kuanzisha biashara, anatumia vibaya na biashara inakufa. Unaona kwa kuwa una uwezo, basi unaweza kuwa unampa fedha ya kujikimu, lakini ukimpa fedha anaenda kulewa. Unakwama, usipompa fedha maisha yake yanakuwa magumu na unaonekana umemtenga ndugu yako, ukimpa anaenda kulewa na kuzitumia vibaya.

Wawezeshe watu kutatua matatizo yao wenyewe, na usisukumwe kufanya vitu kwa sababu unataka kuonekana una roho nzuri. Wale utakaowawezesha kutatua matatizo yao, utawasaidia hata wakati wewe haupo. Ila wale unaobeba matatizo yao, utawaandaa kuanguka vibaya pale ambapo wewe hutakuwepo. Na nikukumbushe tu, haijalishi unampenda mtu kiasi gani, hutakuwa naye kwa maisha yako yote, hivyo mpende kwa kumfanya aweze kutatua matatizo yake mwenyewe.

Katika kukazana kwetu kuwasaidia wengine, hasa wale wa karibu kwetu, watoto, wenza, ndugu tuliozaliwa nao, tumekuwa tunakazana kuwaibia matatizo yao. Tunayachukua kabisa matatizo yao na kuyafanyia kazi na wao wanabaki hawana cha kufanya.



Hii ni njia mbovu sana ya kutaka kumsaidia mtu, kwa sababu unakuwa humsaidii, badala yake unamsababishia matatizo zaidi. Kwa sababu unapomchukulia matatizo yake, anabaki hana cha kufanya, hivyo anaenda kutengeneza matatizo zaidi.

Kwa sababu ukikimbilia kuyabeba ili uonekane una roho nzuri, utaishia kumharibu zaidi yule mwenye matatizo. Kwa sababu maisha yetu yanatoa maana kwenye matatizo na changamoto tunazokutana nazo mara kwa mara na kuzitatua.

Na  Mwl  Japhet  Masatu , Dar  es  salaam , Tanzania,  Afrika Ya  Mashariki ---Mwl  wa  Maisha Na  Mafanikio, Mshauri, Public Speaker(MC), Mwandishi, Mjasiriamali /
Tuwasiliane kwa :+ 255 755 400 128 / + 255 716 924136(WhatsApp ).  EMAIL: japhetmasatu@gmail.com

No comments:

Post a Comment