Sunday, September 16, 2018

JE, WAJUA NJIA ZA KUTENGEHEZA FAIDA KATIKA BIASHARA YAKO ? JIFUNZE HAPA ,

 Njia hizi zinategemeana na zinaenda kama ngazi, hivyo ili kunufaika lazima uzifanyie kazi kwa pamoja.

Njia ya kwanza ni kuongeza idadi ya watu wanaoijua biashara yako. Na hapa ndipo zoezi zima la kununua wateja linapofanya kazi. Kadiri watu wengi wanavyojua kuhusu biashara yako, ndivyo inakuwa rahisi kwako kuwageuza watu hao kuwa wateja. Kama watu 1000 ndiyo wanaojua kuhusu uwepo wako, ukiongeza watu 100 unakuwa umeenda mbele zaidi.

Njia ya pili ni kuwageuza wanaojua kuhusu biashara yako kuwa wateja halisi. Mtu kujua biashara yako haimaanishi ndiyo mteja wa biashara hiyo. Mteja ni yule ambaye ametoa fedha na kununua kitu kwenye biashara yako. ili kuongeza wateja wa biashara yako, unahitaji kuwashawishi wale wanaojua kuhusu biashara yako wanunue kile unachouza.

Njia ya tatu ni kuwafanya wateja warudi kununua tena na tena. Kama umetumia gharama kumfikisha mteja kwenye biashara yako, jua kabisa akinunua mara moja ni hasara kwako. Unapata faida pale mteja anaponunua tena na tena na tena. Na unachopaswa kujua ni kwamba, ni rahisi kumuuzia mteja ambaye alishanunua kwako kuliko kumuuzia mteja mpya kabisa. Hivyo weka juhudi katika kuwafanya wateja waendelee kununua kwako zaidi na zaidi.

Njia ya nne; kuongeza kiwango cha manunuzi. Kama mteja akija kwako ananunua kitu kimoja, unahitaji kumshawishi anunue kitu kingine ambacho kinaendana na kile alichonunua. Hapo unaongeza mauzo na kuongeza faida pia. Kwa mfano kama unauza vifaa vya ujenzi, akaja mteja kununua rangi, unahitaji kumshawishi anunue na brashi za kupakia rangi na vitu vingine vinavyoendana na hili. Kadhalika kwenye mavazi na hata vifaa vya kielektroniki, mpe mteja wigo wa kununua vitu vinavyoendana na kile anachotaka.

Njia ya tano ni kuongeza bei, hii ndiyo wengi huwa wanaikimbilia, lakini ukitumia hizo nne na hii kwa pamoja, utanufaika sana. kwenye njia ya tano, unaongeza bei ya kitu ili upate faida zaidi. Kama utafanyia kazi hatua hizi tano kwa pamoja, ongezeko dogo, kama la asilimia 10 kwenye kila hatua, litaleta ongezeko la asilimia 61 kwenye faida. KAZI  KWAKO  NDUGU .

 Na  Mwl  Japhet  Masatu , Dar  es  salaam , Tanzania,  Afrika Ya  Mashariki ---Mwl  wa  Maisha Na  Mafanikio, Mshauri, Public Speaker(MC), Mwandishi, Mjasiriamali /
Tuwasiliane kwa :+ 255 755 400 128 / + 255 716 924136(WhatsApp ).  EMAIL: japhetmasatu@gmail.com

No comments:

Post a Comment