Sunday, September 16, 2018

ILI UFANIKIWE KIBIASHARA KUNA WATEJA NI LAZIMA UACHANE NAO,

Ili biashara yako ikue vizuri na uweze kupata faida, lazima ufukuze baadhi ya wateja.
Kwanza kabisa unahitaji kuwapanga wateja wako kwenye makundi A, B, C, na D.
Kundi A ni wale wateja ambao wanalipa fedha nyingi na siyo wasumbufu.
Kundi B ni wale wateja ambao wapo tayari kulipia, lakini siyo walipaji wa fedha nyingi, ila ni wateja wenye msimamo, ambao unaweza kwenda nao muda mrefu, na hawana usumbufu mkishakubaliana.
Kundi C ni wale wateja ambao wanataka punguzo kwenye kila kitu, na watakusumbua sana, wanaweza kununua kwa bei ya punguzo na bado wakarudi tena kulalamika kwamba haikuwa sawa kwao.
Kundi D ni wale wateja ambao ni matatizo kwa biashara yako, kwanza hawalipi kwa wakati, na kwenye kila kitu wanatafuta njia ya kubishana au kugombana. Hawa ni wateja ambao wanakuja wakiwa wamejipanga kukusumbua, ili wanufaike zaidi wao.
Ukishawagawa wateja wako kwenye makundi hayo manne, wahudumie vizuri wateja wa kundi A na B, na fukuza wateja wa kundi C na D, kwa sababu hawa ni wateja mabao hawana faida, na pia wanakuzuia usiwahudumie vizuri wateja wa kundi A na B.
Swali ni unawafukuzaje wateja hao?
Zipo njia mbili;
Ya kwanza ni kuwapa utaratibu mpya wa kufanya biashara na wewe, kwamba yale waliyozoea hayapo tena. Bei ni moja na haipungui na malipo ni kwanza na siyo baadaye. Kama hawawezi hilo wanaweza kwenda kwenye biashara nyingine.
Njia ya pili ni kuongeza bei ya bidhaa au huduma unayouza, na moja kwa moja watakimbia wenyewe.
Ukishaachana na wateja hao wasumbufu, nguvu zako peleka kwa wale wateja wazuri wa biashara yako.
Pia unapotangaza biashara yako, hakikisha unatumia lugha inayowavutia wateja wa kundi A na B, badala ya kundi C na D. Kwa mfano kama tangazo lako linasema kuna punguzo la bei au zawadi ya bure, utajikuta unavutia C na D wengi, maana ndiyo wanaopenda rahisi na bure.

 Na  Mwl  Japhet  Masatu , Dar  es  salaam , Tanzania,  Afrika Ya  Mashariki ---Mwl  wa  Maisha Na  Mafanikio, Mshauri, Public Speaker(MC), Mwandishi, Mjasiriamali /
Tuwasiliane kwa :+ 255 755 400 128 / + 255 716 924136(WhatsApp ).  EMAIL: japhetmasatu@gmail.com

No comments:

Post a Comment