Friday, September 21, 2018

JE, WAIJUA AKAUNTI YA FEDHA YA SAIKOLOJIA ?

Unahitaji kujizoesha kifikra na kisaikolojia kuwa na fedha nyingi, hata kama bado hujazishika kwenye mikono yako au kuwa nazo kwenye akaunti yako ya benki. Na unaweza kuanza kwa kufikiria mara kumi ya kipato unachopata sasa, kisha kufikiria kipato hicho mara kwa mara, kukiwekea mipango na kuweka lengo lako la kipato liwe ni kukua kufikia mara kumi ya kipato chako cha sasa. Kwa njia hii utaongeza kiwango chako cha fedha kisaikolojia.

 Watu wengi wanajua aina moja ya akaunti ya kifedha, ambayo ni akaunti ya benki, au akiba na uwekezaji ambao wamekuwa wamefanya. Hivyo ukitaka kuangalia utajiri wa mtu, unaangalia ni kiasi gani cha fedha anacho kwenye akaunti zake za benki na uwekezaji kiasi gani amefanya.

 Aina ya pili ya akaunti ya kifedha, ukiacha akaunti ya benki, ni akaunti ya fedha ya kisaikolojia. Kila mmoja wetu, ana kiwango chake cha kifedha kwenye fikra zake, ambacho ndiyo ameshajiambia anapaswa kupata kiwango hicho. Yaani kila mmoja wetu, kuna kiwango chake cha fedha, ambacho ameshakiweka kwenye fikra na mawazo yake, na akishapata kiwango hicho basi akili yake inatulia na hakazani tena kupata fedha zaidi.

Waangalie watu wote ambao wamepata fedha nyingi kwa mkupuo, kiasi kikubwa cha fedha ambacho hawajawahi kukishika kwenye maisha yao. Waangalie watu ambao wameshinda bahati nasibu, waangalie watu ambao wamerithi mali, waangalie watu ambao wamepokea mafao. Wengi haiwachukui muda wanakuwa wameshapoteza fedha nyingi walizopata na kurudi kwenye maisha yao ya kawaida.
Wanakuwa wamepata fedha nyingi kwenye akaunti ya benki, lakini akaunti yao ya kisaikolojia inasoma kiwango cha chini. Hivyo wanaacha kufikiria kabisa kuhusu fedha, wanaanza kupoteza fedha, mpaka zinapofika kwenye kile kiwango chao cha kisaikolojia ndiyo wanastuka na kuanza kufikiria kuhusu fedha.

 Pia unaweza kufikiria mara 100, mara 1000 na hata zaidi ya kipato unachopata sasa. Fikra zote hizo zitaiandaa akili yako kupokea fedha zaidi na kuweza kutulia na fedha zaidi unazopata. Unapofikiria mara elfu moja ya kipato unachopata sasa, ongezeko kidogo halitakusumbua kama linavyokusumbua sasa.


Na  Mwl  Japhet  Masatu , Dar  es  salaam , Tanzania,  Afrika Ya  Mashariki ---Mwl  wa  Maisha Na  Mafanikio, Mshauri, Public Speaker(MC), Mwandishi, Mjasiriamali /
Tuwasiliane kwa :+ 255 755 400 128 / + 255 716 924136(WhatsApp ).  EMAIL: japhetmasatu@gmail.com

No comments:

Post a Comment