Sunday, March 14, 2021

WAZA SASA , FANYA SASA , IJAYO HAIPO ISIKUSUMBUE SANA.

Wasiwasi au hofu ambazo huingia ndani ya maisha yetu ni pamoja na kufikiria wakati ujao utakuja na mambo gani tusoyajua. Mabadiliko yanayoweza kujitokeza wakati ujao ni chanzo kikubwa cha kutawaliwa na hofu na wasiwasi. Tunajawa na wasiwasi namna maisha yetu ya baadaye namna uchumi utakuwa, afya, magonjwa na mabadiliko mbalimbali ya mambo.

Si rahisi kusema usiwazie wakati ujao ikiwa sasa una mambo magumu unapitia, kipato ni kidogo, misiba inatokea, biashara zinaanguka, umaskini na habari za kutisha kama milipuko ya magonjwa na maeneo mengine yanakabiliwa na vita na njaa. Ni ngumu sana mtu kukuelewa kuwa achana kuifikiria kesho wakati hofu na wasiwasi upo juu ya hali zitakavyokuwa baadaye. Wakati wa sasa huachwa hivi hivi kwa wasiwasi ambao mtu anakuwa anatarajia namna mambo yatakavyokuwa mabaya siku zijazo.

Hofu na wasiwasi ni hali za kawaida zinazotutokea maishani ila zinapokuwa zimezidi hili ni tatizo la udhibiti wetu wa kujua mambo yepi yapo katika uwezo wetu na yepi yalo nje ya uwezo wetu. Habari kuhusu wakati ujao ni jambo usiloweza kulizuia kutokea ila una nafasi ya kuitumia sasa ikaweza kusaidia kukabiliana na mambo yatakavyotokea baadaye. Inawezekana mtu akawa na wasiwasi juu ya maisha yake kiuchumi yatakavyokuwa ila unaloweza kufanya sasa ni kufanya maandalizi ya uchumi wako, kuweka akiba, kuweka dharura na kufanya uwekezaji. Ijayo itakuja na tusiwe na udhibiti nayo ila nafasi ya sasa au wakati wa sasa tunaweza kufanya kitu au jambo.

Kujifunza jambo ambalo hujazoea kulifikiria siku za awali jua itakuwa ngumu sana kuliweza. Hivi ndivyo inavyokuwa ngumu kwa watu wengi kutoacha kuiwazia baadaye na wakapoteza kuitumia kabisa leo. Unajifunza kuipa uzito sasa kwa kujifunza kuituliza akili yako yote kufanya kitu kwa umakini wako wote bila kufikiria kuwa ipo kesho. Weka umakini katika maisha yako ya sasa, furahia mchakato wa maisha sasa bila kufikiria hadi upate kitu fulani siku moja. Ishi kwa wakati wa sasa na ijayo usiiwazie bali ije ikukute unaendelea kuishi kwa kuipa uzito sasa. Wakati ujao ni kiini macho maana unaposema utaikuta ijayo au kesho hutaikuta bali utaihesabu ijayo kama sasa. Kwanini upoteze uzito wa nafasi ya muda ulonayo sasa kwa kuwazia hali isiyo ya kweli bali kiinimacho ?.

Unapoacha kuiwazia ijayo unapata muda wa utulivu wa kufanya kitu kwa umakini na ufanisi. Unapokuwa na wasiwasi mkubwa wakati mwingine hufanyi chochote kile, wengine utakuta hali ya hofu inawafanya washindwe kutuliza akili, wanatetemeka, wanapoteza hamasa maana muda wote wanashindwa kufanya chochote wakitawaliwa na namna mambo siku za baadaye yatakavyokuwa mabaya au hatari. Ukiishinda hii hali unajenga nafasi ya kutumia wakati wa sasa vizuri na unakuwa imara zaidi.

Jifunze kuanzia leo kuwa kwa kila utakachokuwa unakifanya weka akili yako iwe sasa. Hili litakujengea nguvu na kuondoa hofu na wasiwasi wowote kuhusu wakati usio sasa. Mstoa Marcus anasema “Don’t worry about the future. By doing your best today, you’ll build the strength and resources to handle whatever tomorrow may bring”. Hii ikiwa na tafsiri “Usiwe na wasiwasi kuhusu ijayo. Ila Fanya kwa uzuri sasa, hili litakujengea nguvu na rasimali za kutosha kukabiliana na kesho itakavyokuja.

KOCHA  MWL.  JAPHET  MASATU , DAR  ES SALAAM.

WhatsApp + 255  716924136 /   + 255 716  924136


 

1 comment: