Friday, March 26, 2021

NYUMA YA PAZIA , KUNA MAUMIVU MAKALI , SI VILE ULIVYOKUWA UKIFIKIRIA.

Jambo lolote lile unaloweza kuliona kwa wengine unaweza kufichwa uhalisia wake na ukachukulia huenda ni jepesi au watu hao wanaofanya hivyo hawapitii changamoto zozote zile. Ni rahisi sana watu kutamani kuishi kama wengine ila wanapoanza kuishi kama hao watu wanakuja kugundua ukweli kuwa si vile walivyofikiria itakuwa. Unachokiona na unachokutana nacho huenda visiwe vinafanana kabisa na hili limefanya watu wengi wagundue kuwa maisha si vile wanavyoona kwa juu juu bali yana siri kubwa mno.

Unaweza kuona ni rahisi kusikia mtu ambaye kila siku anaamka asubuhi na mapema na kufanya mazoezi bila kuacha ukadhania kujenga nidhamu ya namna hiyo ni vyepesi. Ikiwa huna utamaduni huo na ukajisemea siku basi ngoja nianze kufanya mazoezi kila asubuhi bila kuacha utakuta umeanza siku ya kwanza vizuri, ya pili vizuri, ya tatu unaanza kukutana na vikwazo, ya nne unasema ngoja leo nipumzike, ya tano unapendezwa na mapumziko, siku zinapita hufanyi tena mazoezi. Unapotafakari haya unakuja kugundua kuwa wale wanaofanya mazoezi ya mwili au akili kila siku kwa kufanya matendo kama kukimbia au kusoma vitabu kila siku si rahisi na si wa kubezwa hata kidogo.

Unapopitia mwenyewe kufanya kitu ndivyo unavyoweza kuwa na uzoefu na kuweza kukielezea vizuri katika ugumu wake tofauti na unaposema mambo kwa nadharia au kuyasikia sikia tu. Jamii zetu nyingi hupenda kuona mambo rahisi huku hakuna ambaye ana uzoefu nayo bali ni kwa kusikia au kujifanya kujua ila inapotokea mtu inabidi ahusike kuyapitia ndipo anapokuja kugundua si rahisi kama alivyodhani au kuambiwa na watu wengine.

Wengine wanaweza kusema hiyo biashara unayofanya mbona ni rahisi au kama ni jambo la kuandika au kusoma kitabu mtu anaweza kuona anayefanya ni rahisi. Ila inapotokea mtu huyo aingie kuandika, kusoma au kufanya biashara ndipo anapokuja kugundua namna ilivyo ngumu kufanya hivyo vitu. Kuna msemo unaosema kama ingekuwa mambo rahisi basi watu wengi wangekuwa wameyapata isitoshe ni asili ya binadamu kuishi vizuri na kwa furaha. Ndivyo ambavyo hata njia ya kufanikiwa inavyotamaniwa na wengi ila si rahisi kama vile watu wanavyoingia katika mitego ya kuambiwa toa fedha sasa na utapata mara mbili yake au toa fedha na utajirike haraka. Wengi wameingia katika matatizo kwa kutamani kupita njia rahisi au wakijaribu kurahisisha mambo huku kiuhalisia mambo huwa si rahisi kama yanavyodhaniwa na wengi.

Usiwe mwepesi kuvunja moyo watu au kuchukulia vitu kirahisi hasa kama hujawahi kuvipitia au huvijui kiuzoefu wake. Inawezekana ukijaribu hutaweza kuvifanya kama wengine wanavyofanya.

KOCHA  MWL.  JAPHET   MASATU.

WhatsApp + 255 716924136 /  + 255 755 400128

EMAIL :  japhetmasatu@gmail.com

 

No comments:

Post a Comment