Sunday, March 28, 2021

KUWA TAYARI KUISHI UHALISIA WAKO , UACHE ALAMA NJEMA.

Maisha yetu mengine huanza pindi tunapomaliza maisha haya ya mwili. Awamu hii ya pili ya maisha ni kuishi katika mioyo ya watu wakikumbuka namna tulivyogusa maisha yao kipindi uhai wetu ulipokuwepo. Nafasi hii ya kushuhudia kila kitu ambacho kimeachwa kama alama tuachayo huchipua pindi ukomo wa maisha yetu ufikapo na hivyo huwa hatuoni namna alama iloachwa bali waloachwa hushuhudia.

Maisha yetu ni alama na nyayo tunazoacha kuwa tulikuwepo wakati fulani wa maisha. Alama za maisha yetu zinabebwa na kumbukumbu ambazo zinaachwa mioyoni mwa watu ambao huwa tayari kubeba masimulizi kwa vizazi vingine. Watu wenye alama njema alama ya matendo yao huchipua na kuendelea kuishi kwa muda mrefu.

Kuishi katika vipawa na vipaji ulivyopewa kwa ukubwa au kutojibakiza ndivyo alama njema inavyoacha katika mioyo ya watu. Jina la mtu atendaye mambo mema hudumu na kukua zaidi. Mtu hukumbukwa kwa vile alivyowagusa watu kwa namna mbalimbali

Moja ya mambo niaminiyo kuwa uwepo wetu wa maisha ni kuacha alama ya vipawa, vipaji, ujuzi na uzoefu kwa kuandaa njia kwa ajili ya watu wengine. Tulipo leo ni kwa sababu ya majitoleo ya watu wengi ambao majitoleo yao hawakuweza kuona matokeo ya mbegu walizopanda, majitoleo yao ndio unafuu ambao tunao sasa na majitoleo yao ni njia ambazo leo tunapita kwa sababu yao. Tupo tuishi na kuacha Dunia katika nafasi nzuri zaidi tofauti na vile tulivyoikuta.

Kuishi bila kujibakiza ni maisha yatakayo moyo, ni maisha ya kujitoa sadaka, ni maisha ya kujisahau wakati mwingine ili uwe daraja kwa watu wengine. Kuacha alama njema ni gharama na hugharimu hata watu maisha yao. Kujitoa usiku na mchana kuishi kikamilifu ni kujikana kuwa hutafanya kila kitu katika maisha haya bali utawekeza nguvu maeneo muhimu katika maisha ili kuandaa njia njema kwa wengine. Yataka moyo, yataka moyo thabiti, yataka ustahimilivu kujitoa na kuishi kitoshelevu.

Alama njema unayoweza kuitengeneza na kutoa zawadi yenye manukato kwa dunia ni kuwa tayari kuishi uhalisia wako, u tayari wa kujimimina kwa vipaji ulivyojaliwa, mawazo, ujuzi, uzoefu, maarifa kuisaidia jamii kujitambua, kukua na kuendelea. Hii alama huyapa maisha ya mtu kuwa marefu hata baada ya kufa kwake. Maisha ya mashujaa ambao tunawasoma na kuwakumbuka ni kwa sababu ya alama za matendo yao yasofutika mioyoni mwetu. Mimi na wewe tuna nafasi sasa tukiwa hai kuendelea kufanya mambo bila kujibakiza tukijitoa kadri tuwezavyo kuifanya Dunia kuwa sehemu salama ya kuishi.

KOCHA   MWL. JAPHET   MASATU , DAR   ES SALAAM

WhatsApp + 255 716924136  /    + 255 755 400128 / + 255 688 361 539

 

No comments:

Post a Comment