Sunday, March 28, 2021

ISHI SASA , ISHI KAMA HUTAISHI TENA.

Kuishi tunaishi mara moja na nafasi hii tunapoipoteza ndivyo tunavyopoteza dhahabu katika mikono yetu. Wakati ambao tunao sasa ni wa thamani mno kiasi kwamba ingetokea ni nafasi ya kupatikana tena basi watu wengi walokwisha yaaga maisha ya dunia wangeomba warudie kuishi tena. Ila haitokei tena hii nafasi ifikapo ukomo wake endapo hatutaweza kuipa uzito kuwa ni fursa ya muda mfupi mno.

Tunapokuta wengine wakiyapoteza maisha huwa tunakumbuka kuwa kumbe maisha yetu ni mafupi na yanakimbia mno kuisha. Ila ikitokea hakuna taarifa zozote za watu kufariki basi huwa tunasahau hilo na kuendelea kuyapoteza maisha yetu kwa vitu ambavyo havitupi nafasi ya kuishi vizuri au kutumia nafasi ya kuwa hai kwa utoshelevu. Maisha huendelea na hukatika kama kamba ilochakaa na kuanzia hapo hakuna tena marudio kuwa utaishi tena au upya.

Nafasi ya kuishi ni adimu mno na ya kuthaminiwa zaidi kuliko chochote kile. Maisha yana maana endapo mtu yu hai ila baada ya hapo mtu husahaulika. Nafasi hii ya kuishi inatupa mwaliko wa kuanza, kuthubutu, kupenda, kusaidiana na kuwa tayari kuandaa njia kwa ajili ya watu wengine ambao watakuja badala yetu sisi. Kila mmoja ambaye huwaza hili kuwa maisha huisha basi hupata mwamko na hamasa kubwa ya kuishi akijiandaa au akiandaa mazingira mazuri kwa watakaokuja nyuma yake.

Unaweza ukawa unapitia mambo magumu katika maisha ila ukitulia na kugundua bado moyo unadunda, pumzi bado unavuta huu ni utajiri mkubwa mno. Maana licha magumu umeyapata ila kama hayaondoi uhai wako basi ni njia bora ya kuimarika, kuwa mstahimilivu na mtulivu ukiwa na falsafa ya kuyaongoza maisha yako kuwa hakuna kitu kitakuwa kigumu wakati wote au hakiharibiwa na muda.

Furahia kila nafasi unayopata ya kuamka na kukuta bado unapumua na mwili unafanya kazi. Furahia hii zawadi kwa kuishi kwa ukubwa, kuishi kwa uzito na kuishi kana kwamba muda ulonao ni mdogo na pengine unachokifanya ndo unakifanya kwa mara ya mwisho haitakuja kutokea tena. Maisha ni haya haya yaendayo yasodumu hivyo thamini kila nafasi ya wewe kuwa hai.

NA KOCHA  MWL.  JAPHET   MASATU , DAR  ES  SALAAM , TANZANIA.

WhatsApp + 255 716 924136 /  + 255 755 400128 /  + 255 688 361 539

 

No comments:

Post a Comment