Saturday, March 13, 2021

HUWEZI KUYAPINGA MABADILIKO , LAZIMA YATOKEE NA NDIO ASILI TANGU KALE NA WAKATI UJAO.

Unapoangalia maisha ya ukuaji wa mtoto au mmea utaona namna ukuaji wake ukienda kubadilika kadri muda upitavyo. Mtoto hubadilika umbile lake, hubadilika fikra na kutoka utoto mtu huwa mtu mzima na akawa tegemezi ya watu wengi. Kwa mtu anayeangalia juu juu tu akafikiria alivyomuona mtoto basi hubakia hivyo kumbe mtoto ndani yake ana ujana, utu uzima na uzee ni suala la muda tu mambo hubadilika.

Huwa tunachukulia mambo au matukio yanayotokea kana kwamba ndio mwisho wake kuwa hivyo tusijue asili inafanya vitu vibadilike na hakuna kinachoweza kuwa hivyo hivyo wakati wote. Hili linafanya kuonekana kuwa kile ambacho tunakiona kimekamilika kumbe baada ya muda hakikukamilika ila kina mwelekeo wa kuendelea kubadilika. Mfano kama leo wazee walowahi kuishi miaka ilopita na hawakuwa na mitandao ya kijamii basi kwa wakati wao waliishia kuona njia za kizamani za mawasiliano zingebakia hivyo miaka yote kumbe vitu huenda kubadilika.

Yote ambayo tunayaona sasa iwe ni mifumo ya mitandao, mifumo ya uongozi na kuishi ipo katika ngazi ya ukuaji kama alivyo mtoto na haijakamilika ila inaenda ikibadilika. Miaka 100 ijayo mambo mengi yatakuwa yamebadilika mno kuanzia watu wanavyoishi, mifumo ya mawasiliano, mifumo ya uongozi hadi mifumo ya kidunia inavyojiendesha. Hata itakapotokea watu wa miaka 300 ijayo wakawepo wataona mabadiliko makubwa ambayo huenda sisi tusipate nafasi ya kushuhudia hayo mabadiliko.

Zamani njia za kuwasiliana zilikuwa chache na njia kama ya kusafiri sehemu moja uende kupeleka habari sehemu nyingine sidhani kama walidhani kuwa ipo siku njia za mawasiliano kurahisishwa na kuwa nyingi kama sasa. Siku hizi mawasiliano au kupeleka ujumbe umefanyika kirahisi zaidi kwa njia ya simu, barua pepe, mitandao ya kijamii, luninga na redio. Ikitokea wengine wakirudi sasa na kuishi watashangaa mno kuona dunia imebadilika na si kama walivyoishi huko zamani. Ni somo la asili namna hakuna kitu kimeishia hapo isipokuwa kipo katika ukuaji na mabadiliko.

Kwa kujua hili basi tunahimizwa pia kuona kila mtu ambaye anatuzunguka tusimkatie tamaa yoyote ile awapo hai maana nafasi ya kubadilika ni kubwa kuliko kuona ni hitimisho la yale anayoyafanya. Kuna mifano mingi katika jamii zetu ambapo watu walipoanguka au kufeli kitu fulani tukadhani ndio mwisho wa kufanikiwa kwao ila sivyo ilivyo. Wengi ambao wamepitia kufeli, kushindwa na magumu ndio wenye mafanikio makubwa zaidi katika jamii zetu.

Unapitia magumu ila jua ni magumu yanayopita na hayakumalizii hapo tu isipokuwa yanakuandaa kukupa mabadiliko makubwa. Magumu ni njia nzuri inayozalisha watu bora, imara na wenye nguvu zaidi katika jamii zetu. Mabadiliko lazima yatokee na ndio asili ilivyo tangu kale na wakati ujao. Mabadiliko hayana budi kuja kwa chochote kinachokuwepo sasa. Wengi huwa wanaogopa mabadiliko ila huja hivyo hivyo kwa sababu ni asili inasema hilo. Huwezi kuyapinga mabadiliko maana hakuna kitu kinachoweza kukamilika bila kuendelea kubadilika kila siku. Asili ni mabadiliko na inajitahidi kujiendeleza. Maendeleo na mabadiliko ni mapacha katika asili.

Everything that exists now is a seed of what is to come. Nothing around you is in its final form- Marcus Aurelius

KOCHA  MWL.  JAPHET  MASATU

WhatsApp + 255 716924136 /  + 255 755 400128


 

No comments:

Post a Comment