Sunday, March 14, 2021

MAPUMZIKO NI KAMA KUJICHAJI KAMA BETRI , ILI UREJEE TENA KAZINI.

Maisha yana matukio mengi ambayo yanatuchosha na kufanya miili yetu iwe imeishiwa nguvu wakati mwingine. Tunapopata mapumziko au kulala basi tunajikuta kama tumeongezewa nguvu tena ya kuendelea na kazi. Nafasi ya mapumziko imekuwa ni njia inayofanya watu wapate kuchangamka na kuwa na ari mpya tena. Tunaona namna vipindi vya mapumziko vipo mashuleni, semina, michezo mbalimbali na hata sehemu za kazi ili watu wapate kurejea tena mara baada ya kazi au kufanya jambo kwa muda mrefu.

Watu wanapotoka kutoka katika mapumziko huwa na nguvu za kuendelea na nafasi nyingine ya mambo. Huwa nafurahia sana ninapoona wachezaji wa mpira wanapopata dakika chache za mapumziko na marejeo yao ya dakika nyingine 45 huwa na ari mpya, nguvu na kasi mpya. Hivi ndivyo ilivyo nguvu ya mapumziko inapofanywa kwa kiasi ili kurejesha nguvu.

Zama tuishizo sasa watu huzidisha mapumziko na kufanya zaidi ya mapumziko. Mapumziko haya hupelekea uzembe na uvivu ambao watu hujisahau kuwa faida ya mapumziko ni muda mfupi kisha unarejea kazini. Wengine wamefanya mapumziko ya kazi hadi wamepoteza kazi, wapo ambao wamefanya mapumziko hadi wamesahau tena kurejea kusoma na wapo ambao walifunga biashara wakaishia katika mapumziko ambayo yaliwaletea hasara baada ya faida.

Mapumziko ni sawa na pale ambapo betri limeishiwa chaji basi linachajiwa na likishajaa basi linatumika kufanikisha tena kazi. Likijaaa halafu lisitumike kuna nafasi ya kuharibika baada ya muda kupita. Kitu kinachopumzika muda mrefu huanza kuharibika. Jaribu kuangalia vitu kama magari yakiachwa muda mrefu bila kufanyiwa chochote huanza kuharibika tairi na kutu huwa inaanza kushambulia maeneo ya gari. Mapumziko yakidumu bila kuangalia muda ni kutayarisha kufa kwa kitu.

Fanya kazi kweli kweli ila jipe nafasi fulani ya muda kupumzika kwa lengo kuikuza afya na nguvu na si kufanya ulevi wa mapumziko. Mstoa Marcus anasema “Rest is for recharging, not for indulgence. Take only what is sufficient for your health and vitality. Too much rest—like too much food or drink—defeats its purpose, weakening the body and dulling the spirit”. Ikiwa na tafsiri “Mapumziko ni kwa kujichaji, sio ulevi. Chukua mapumziko kwa kutoshea afya na nguvu. Mapumziko ya kuzidisha ni sawa na ulaji au unywaji ulopitiliza moja kwa moja huondosha fokasi, hudhoofisha mwili na kuitia kiza roho”.

Muda wa mapumziko husisha kutuliza akili yako, kulala kwa muda wa kiasi, kuwa mbali na mitandao, tafuta eneo zuri la asili au fanya matembezi ya maeneo tulivu. Utulivu huu husaidia mapumziko yawe imara na kumsaidia mtu kumaliza likizo au muda wake wa mapumziko akiwa na nguvu na ari mpya ya kurudi ulingoni. Maisha ni mapambano kuna wakati unatoka kidogo kupumzika kupata amsho jipya la kupambana.

KOCHA   MWL.  JAPHET   MASATU , DAR  ES  SALAAM.

WhatsApp + 255 716924136  /  + 255  755 400128

 

 

No comments:

Post a Comment