Sunday, March 28, 2021

UWEZEKANO WA KUISHI MUDA MFUPI NA KUTENDA MAKUBWA UPO , TUMIA RASILIMALI MUDA VIZURI.

Muda ni rasimali muhimu sana katika kuleta mchango mkubwa duniani. Mtu hupimwa katika muda aloishi na namna katika kuishi alivyohusika katika kuleta mchango au athari fulani katika maisha ya watu. Si urefu wa maisha unaoweza kuleta mchango mkubwa ila ni katika uchache wa siku tuishizo mtu anavyozitumia vizuri kuwa mtu mwenye mchango au athari fulani inayobakia alama ya kudumu kunakothaminiwa.

Historia imebeba maelfu ya watu ambao hawakuishi muda mrefu ila alama walizoacha kwa vitu walivyofanya zimeendelea kudumu vizazi hadi vizazi. Ufupi wa maisha yao ulijenga uhai wa majina yao yaendelee kuishi daima. Muda haukuwa kikwazo kwao ila ilikuwa ni lulu ambayo walijua kuitumia vizuri kama nafasi inayoisha bila habari. Hili liliwasukuma sana kuchukua hatua, kuanzisha vitu na kufanya vitu vingi vinavyoendelea kuwasemea mema na alama njema walizoacha.

Napenda sana kufuatilia muziki wa Reggae na ninaposikiliza nyimbo hizi huwa najifunza kwanza kwa ujumbe uliomo hususani za Lucky Dube na Bob Marley, pili zinatengeneza utulivu wa akili na tatu zimeimbwa na watu ambao walipenda walichokifanya. Bob Marley anahesabika moja ya miamba mikubwa ya waanzilishi walokuwa na ushawishi kupitia muziki huu wa Reggae. Ushawishi wa muziki huu umeenea duniani kote licha Bob Marley kufariki dunia mwaka 1981 akiwa ni kijana wa miaka 36 tu. Unapozungumzia muziki huu huwezi msahau kumtaja huyu mwanamuziki

Maisha yetu ni mafupi na wakati mwingine katika ufupi wa hizi siku huwa hatuzitumii kwa uzito au utoshelevu. Ila watu wenye kupata ufahamu mapema kuwa maisha haya hukatika haraka kama kamba basi hufanya mambo makubwa kwa muda mfupi kwa njia ya kutumia muda wao vizuri kwa utoshelevu wakiweka akili zote kufanya mambo yaachayo alama. Ndivyo hutufundisha na sisi kutumia hii nafasi ya maisha tusojua inaweza kukoma lini kutumia kwa utoshelevu, kujisukuma, kufanya zaidi ya pale ambapo tumekwisha kufanya awali na kuandaa mazingira mazuri kwa ambao watakuja nyuma yetu.

Ili tuweze kutumia nafasi ndogo ya maisha kufanya makubwa kipindi kifupi ni kuanza kujifunza kuchukua hatua mapema, kutoghairisha, kutekeleza haraka iwezekanavyo. Haya mambo matatu ndio yanayofanywa na watu wote ambao huacha alama kubwa ndani ya kipindi kifupi cha maisha yao. Ni watu ambao huchukua hatua mapema, hawaghairishi mambo na tatu ni watu ambao wanatekeleza wanachosema haraka iwezekanavyo iwe mchana au usiku hutaka kuona matokeo.

Maisha tunaweza kuyafanya yawe marefu pale ambapo tunatumia nafasi ndogo hii ya maisha kufanya vitu kwa ukubwa. Tunapojifunza kutopoteza muda katika rasimali hii adimu ndivyo ambavyo tunatengeneza matokeo makubwa kadri siku zinavyoenda. Urefu wa maisha unawezekana kwa kutumia kila dakika na saa kwa kufanya mambo yatakayodumu na kufaidisha wengine kwa wakati wa sasa na ujao.

NA   KOCHA   MWL.  JAPHET   MASATU , DAR  ES  SALAAM , TANZANIA.

WhatsApp + 255 716 924136  /  + 255 755 400128  /  +  255 688 361  539

 

No comments:

Post a Comment